Bendi Kutoka Ukraine Yatikisa You Tube kwa Video ya Muziki Ionekanayo katika Mfululizo wa Vifaa Vingi vya Apple

The "Knock Knock" video was shot in one take and uses 14 different screens to tell its story. Image from YouTube.

Video ya wimbo wa “Knock Knock” uliorekodiwa mara moja na kutumia simu 14 tofauti katika kuionesha. Picha kutoka You Tube.

Kampuni ndogo ya kujitegemea ya utayarishaji wa muziki wa mahadhi ya dansi nchini Ukraine imekonga nyoyo za watumiaji wa You Tube pamoja na wale wa Apple kupitia kwenye video fupi ya muziki ambayo hadi sasa imeshatazamwa na watu zaidi ya nusu milioni.

Brunettes Shoot Blondes, bendi ya kujitegemea ya mahadhi ya dansi ya taratibu kutoka Kryvyi Rih, mji wa viwanda ulio katikati ya Ukraine ya Mashariki, iliamua kutoa video ya muziki unaokwenda kwa jina “Knock Knock” kwa namna ya tofauti kabisa. Video hii ya dakika mbili na nusu inaonesha mfululizo wa matukio ya wimbo huu kupitia vifaa 14 tofauti vya vya Apple: simu zenye uwezo mkubwa, tableti na ngamizi mpakato. Wahusika katika video, kama miujiza vile, wanaonekana kuhama kutoka katika kifaa kimoja kwenda kingine.

Pasi na shaka video hii itakuwa iliwachukua muda mwingi kuiandaa, kwani watayarishaji walisema kuwa video hii ilirekodiwa katika muda ule ule na kwa wakati mmoja, kwa kutumia kamera moja na haikuhusisha marekebisho mengine mara baada ya kurekodiwa. Kazi hii imeishia kuwa simulizi ya kimapenzi yenye kuvutia na iliyoandaliwa vyema kwa kuwianishwa barabara na wimbo wa kimahaba ulioambatanishwa na video hii. Kisichofahamika, bila shaka, ni muda uliotumiwa kubuni na katika uundaji wa katuni, na pia upangiliaji wa vifaa vilivyokuwa juu ya meza. Na pia, kupangilia muda sahihi.

Wakati watumiaji wa Youtube wakiendelea kusambaza video hii ya bendi kutoka Ukraine iliyoandaliwa kwa ustadi mkubwa, baadhi ya watu wanahisi kuwa, yawezekana video video hii imeandaliwa kwa siri kama namna ya kutangaza bidhaa za Apple kufuatia vifaa hivi vya Apple kutumika katika kazi hii iliyotukuka. Tunafikiri kama kampuni ya Apple itaweza kulitazama hili: wimbo na video ingaliweza kutumika kama namna muhimu sana ya kuitangaza kampuni ya Apple.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.