Video Ioneshayo Mtoto Akiokolewa Kutoka Kwenye Kifusi cha Jengo Lililolipuliwa kwa Bomu Nchini Syria

A screenshot of a YouTube video by Nour Media Center showing the rescue operation

Picha iliyopigwa kutoka kwenye video ya YouTube na Kituo cha Habari cha Nour inayoonyesha operesheni ya uokoaji

Kwa siku za hivi karibuni, imekuwa nadra sana kusikia habari nzuri kutoka Syria, nchi iliyokumbwa na vita vikali. Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa mpya ya idadi ya vifo inayofikia zaidi ya watu 191,000. Vifo hivi vinatokana na ugomvi uliopo baina ya vikosi vya wanajeshi vinavyomtii Rais Bashar Al-Assad na vikundi vinavyopinga uongozi wake. Mkuu wa Tume Kuu ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Navi Pillay, alionesha kutoridhishwa na hali kwa kusema kuwa “hakuna dalili ya kusitisha vita.”

Hali ikiwa bado ni tete, hebu turejee mojawapo wa matukio haya nadra sana ya mwaka uliopita iliyowahi kutokea nchini Syria.  Kwa wale wasioamini katika miujiza, huu hapa ni mmoja.

Video hii, ambayo imeshatazamwa zaidi ya mara milioni moja katika mtandao wa YouTube kupitia akaunti mbali mbali, inamuonyesha mtoto mdogo akiokolewa mara baada ya kufukiwa kabisa na kifusi kufuatia kushambuliwa kwa nyumba yake kwa bomu huko Aleppo, jiji la pili kwa ukubwa nchini Syria.

Video hii, ambayo hapo awali ilikuwa imepakiwa na Kituo cha Habari cha Nour katika lugha ya Kiarabu, ilisambazwa na tovuti ya habari ya euronews pamoja na mtumiaji wa YouTube, Cometotruth, mnamo tarehe 24, mwezi wa Januari, mwaka wa 2014.

Habari njema zilisikika wiki moja baada ya kuokolewa kwake, mnamo tarehe 29, mwezi Januari, mwaka wa 2014. ATJEH CYBER WARRIOR alisambaza video iliyoambatanishwa na maneno katika lugha ya Kiingereza, ambayo ilionyesha kuwa msichana huyo mdogo alifahamika kwa jina la Ghina:

Ghina ni mzima tena mara baada ya kuokolewa kutoka chini ya kifusi. Ndege za kivita zinalipua majengo, lakini watu na watoto wadogo ndio waathirika wakubwa. Ghina alimpoteza mama yake kwa kufukiwa kwenye kifusi kufuatia nyumba yao kulipuliwa kwa mabomu. Ghina alikuwa na bahati, tofauti na mama yake, ambaye bahati haikuwa kwake. Kwa sasa Ghina anaishi na baba pamoja na ndugu zake 6 katika nyumba iliyo na upungufu mkubwa wa mahitaji muhimu ya maisha.

Ghina ni mmoja wa maelfu ya watoto Wasyria wanaokabiliana na madhara makubwa yatokanayo na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa katika mwaka wake wa tatu sasa.  Zaidi ya watu 191,000 wameshapoteza maisha  yao katika ugomvi unaohusisha umwagaji damu wa kugombania kuiongoza nchi ya Syria, ugomvi uliopo baina ya vikosi vya wanajeshi vinavyomtii Rais Bashar Al-Assad na vikundi vinavyopinga uongozi wake. Ugomvi huu uliibuka kwa mara ya kwanza wakati wa vuguvugu la maandamano ya Waarabu katika eneo hilo. Ghina amekuwa mhanga wa mabomu ambayo yamekuwa yakitupwa na serikali kwenye maeneo ya raia licha ya kulaaniwa na mataifa mbalimbali.

Je, ungependa kuwasaidia watoto wa Syria??  Ifuatilie makala yetu “Janga la Watoto Nchini Syria” ili ufahamu jinsi unavyoweza kuwasaidia. 

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.