Cuba: Maandamano yafanyika Mara Mbili, Wengi Wakamatwa

Kikundi cha wanawake kijiitacho ‘wanawake wavaliao mavazi meupe’ (Ladies in White) kwa mara nyingine wametawala fikra za wanablogu wa Cuba waishio nje ya nchi. Maandamano ya amani ya kikundi hicho ambacho ni moja wapo ya vyombo vya upinzani vinavyoheshimika zaidi katika visiwa hivyo –pamoja na kukamatwa kwao mara kwa mara na vyombo vya dola –yanaendelea kuvuta hisia za watu. Mapambano ya hivi karibuni yalitokea mwishoni mwa juma lililopita wakati ambapo wanachama wa kikundi hicho walipojaribu kufanya maandamano mara mbili mjini Havana.

Pedazos de la Isla, ambaye aliorodhesha matukio hayo hatua kwa hatua kwa kutumia picha , alibaini kwamba:

Pamoja na ukandamizaji uliofanywa na serikali, zaidi ya wanawake 40 wa kikundi hicho cha ‘Ladies in White’ walishiriki maandamano kuelekea kwenye kanisa liitwalo Santa Rita mjini Havana siku ya Jumapili, tarehe 17 Juni, kuadhimisha Siku ya Baba. Mara tu baada ya ibada kuhitimishwa, akina maana hawa waliamua kuwazidi werevu polisi na kuandamana kwa mara ya pili ndani ya siku moja, mara hii wakitokea mtaa wa Infanta kuelekea mtaa wa Neptune.

Blogu hiyo pia iliweka posti mbili nyingine kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya wanachama wa kikundi hicho cha ’Ladies in White’. Posti ya kwanza iliweka taarifa nyingi kuhusu namna Caridad Caballero Batista, mume wake na mtoto wao wa kiume walivyopekuliwa na kuwekwa kizuizini:

Baada ya kuwatembelea ndugu kadhaa…walijikuta wakizungukwa na polisi wanaotumika kisiasa mara tu walipowasili kwenye jimbo la Holguin. Kwa mujibu wa Cabellero, afisa wa polisi aliyelizuia gari ambalo familia yake ililitumia kusafiria…alimwamuru dereva kumkabidhi nyaraka zake.

Hata hivyo, wanaharakati wanaeleza kwamba ‘lengo lilikuwa zaidi ya kuomba kuona nyaraka za dereva, kitendo hicho kilipangwa kwa makusudi ya kumpekua mume wangu Esteban pamoja na begi alilokuwa amelibeba, lililokuwa limejaa nguo’. Afisa huyo wa jeshi alimwamuru Esteban kushuka garini ili afanyiwe upekuzi, kitendo ambacho Esteban alikipinga akisema asingeruhusu kufanyiwa hivyo, akisema kwamba ‘yeye si mhuni’. Caballero anasema kwamba ‘maafisa hao walipandwa na ghadhabu na kumwambia Esteban kwamba alikuwa anatenda kosa la jinai’.

Matokeo yake maafisa hao wa polisi walimlazimisha Esteban Sandez kupanda gari la Polisi wamlete kituo cha polisi, ambako alipekuliwa na kushikiliwa. Kwa kuona hayo, Caridad Caballero na mwanae Eric Sandez alishuka garini na kuanza kupingana na unyama huo, akiwaambia polisi hao kwamba kama wangemchukua Esteban, basi ingebidi wawachua na wao (yeye na mwanae) pia.

Katika dakika chache, wanaharakati hao watatu walichukuliwa kwenda kituo cha polisi kilichopo nje ya mji wa Holguin.

Baada ya masaa kadhaa, familia hiyo iliachiliwa huru, lakini mara tu baada ya kuwasili nyumbani kwao mjini Holguin walibaini kuwa polisi hao wanaotumika kisiasa walikuwa wamepanga kufanya operesheni ya kawaida ya mwisho wa juma ili kuwazuia kuhudhuria Ibada ya Jumapili.

Kitendo cha kuwazuia kuhudhuria Ibada Takatifu kilikuwa mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na idara ya usalama wa nchi hiyo kuzibana harakati za kikundi hicho.

Posti ya pili ilisimulia kukamatwa kwa mwanachama ajuza wa kikundi hicho:

Katika Siku ya Baba mwaka huu, wanachama wa kikundi cha “Ladies in White” kote nchini Cuba walihamasika kufanya harakati za amani za kusherehekea siku hiyo. Matokeo yake, vikosi vya polisi vya nchi hiyo vilijibu mapigo kwa operesheni maalumu ya kikandamizi iliyoanza siku chache kabla, na kusababisha kukamatwa kwa idadi kubwa ya wanawake hawa katika majimbo yote ya kisiwa hicho. Katika waliokamatwa alikuwepo Blanca Hernández Moya , ajuza wa miaka 75, aliyeteseka kwa kipigo cha kinyama akiwa mikononi mwa polisi…

Ajuza huyo…alikuwa akielekea yalipo makao makuu ya kikundi hicho cha Ladies in White akitokea nyumbani kwake mitaa ya Havana Kati –alikozaliwa kiongozi wa kikundi hicho aliyeuawa, Laura Pollan, mtaa wa Neptune –ambapo alibughudhiwa sana na polisi.

‘Walinishambulia’, anasema Moya, ‘walinilazimisha kuingia garini, na polisi mmoja wa kike alinikunja mkono wangu na kunipiga’.
Baada ya dakika kadhaa, gari lililokuwa limembeba ajuza huyo liliegeshwa na alilazimishwa kutoka, akatelekezwa pembeni mwa bwawa karibu tu na eneo lisilo na watu liitwao Penalver, nje ya mtaa wa Cotorro.

Blogu ya Capitol Hill Cubans pia iliandika habari za ‘kamata kamata’ hiyo iliyofanyika mwisho wa juma.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.