Irani: Kampeni ya Kutaka Mwanablogu-Mpiga Picha Hamed Saber Kuachiwa Huru

Zaidi ya wanafunzi 70 waliohitimu elimu ya chuo kikuu na wasomi wa nchini Irani wametoa wito [fa] wa kuachiwa kwa Hamed Saber, ambaye ni mwanablogu-mpiga picha na mwanasayansi wa kompyuta wa nchini humo aliyekamatwa pasipo sababu za kuelewekea mnamo tarehe 21 Juni 2010 jijini Tehran. Rafiki yake ametueleza kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Hamed kukamatwa. Chanzo hicho hicho kimeeleza pia kwamba picha kadhaa za Hamed za maandamano ya upinzani nchini Irani zimechapishwa katika magazeti kadhaa ya kigeni pasipo yeye mwenyewe kuwa na habari.

Hamed vilevile ndiye aliyebuni na kutengeneza “Access Flickr“, kiperuzi cha mtandao wa intaneti ambacho huvuka vikwazo vyote vinavyochuja habari za picha katika mtandao wa ubadilishanaji picha wa Flickr katika nchi za Irani, Muungano wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, China na kwingineko ambako mtandao huo umepigwa marufuku. Mmoja wa marafiki wa Hamed alituma barua katika jukwaa la majadiliano la kwenye mtandao wa Flickr akitaka Hamed kuungwa mkono:

Kama ambavyo baadhi yenu pengine tayari mnafahamu, karibu mwezi mzima umepita tangu Hamed Saber, rafiki yetu kipenzi, na mwanasanaa na mwanzilishi wa kundi la Irani la Flickr, akamatwe pasipo sababu zilizo bayana.

Kumekuwa hakuna taarifa zake isipokuwa kwa simu mbili zilizopigwa kutoka mahali kusikofahamika.

Kundi la marafiki zake wa zamani, wanafunzi wenzake wa chuo kikuu na maprofesa kutoka katika vyuo vikuu vinavyofahamika vema mahali mbalimbali duniani wametoa baura inayoomba Hamed aachiwe huru.

Sisi sote tunamfahamu kwa muda mrefu, tangu siku zile za mwanzo tulipojiunga katika kundi hili au walau katika safari tulizofanya pamoja naye.
Wengi wetu tulianza shughuli ya upigaji picha na kuzituma katika Flickr na hasa kundi hili na pengine kujipatia marafiki wa kudumu maishani humuhumu. Mimi mwenyewe najihisi kuwa na deni kubwa kwake hasa baada ya kuwa nimepata marafiki wengi wanasanaa hapa katika kundi hili.

Leo ametupwa mahabusu pasipo sababu zilizo bayana na hii ndiyo fursa ya kuonyesha urafiki wetu na kuthamini kwetu mchango wake.

Nafikiri tungeweza kuandika barua au tamko na kutetea nafasi yake kama mwanasanaa na rafiki yetu wa zamani na kudai kuachiwa kwake huru.

Mimi si hodari katika kuandika, kama kuna yeyote mwenye maoni au wazo au pendekezo la kuonyesha ishara ya mshikamano wetu, tafadhali saidia, andika hata mstari mmoja kwa marafiki, hatuna budi kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.

Marafiki wa Hamed kwenye blogu ya “Free Hamed Saber”, yaani “Hamed Saber Aachiwe Huru” waliandika [fa]:

Saber, ambaye ni mshindi wa tuzo ya medali ya Shaba katika mashindano ya sayansi ya kimataifa, alikuwa na fursa ya kuhamia nchi nyingine lakini yeye mwenyewe alichagua kubaki Irani na kufanyia kazi kwa ajili ya “uhuru na ustawi wa kiuchumi” (wa Irani).”

Tamko linawataka viongozi nchini Irani kumpa Saber hukumu iliyo ya haki.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.