Kadri Liberia inavyotulia, vijana waanza kuzungumzia ngono

“Ninataka watoto wengine wote waliozaliwa Liberia –na duniani kote–kuishi maisha makamilifu yasiyo na maumivu na yaliyojawa na maua ya upendo, kama yangu,” anaandika Mahmud Johnson kwenye blogu ya vijana kuhusu VVU/UKIMWI kwenye jukwaa la Global 40. Ana umri wa miaka 18 mtangazaji mwenza wa zamani wa kipindi cha redio kwa vijana nchini Liberia, “Na Tuzungumzie Ngono”, ambacho kinachoshughulika na masuala yanayohusiana na maambukizi ya VVU/UKIMWI na kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Taratibu Liberia inapitia hatua kwa hatua kutoka kwenye karibu miaka 15 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilimalizika mwaka 2003 na kusonga mbele kuelekea kwenye maendeleo. Vizingiti vilivyobaki ni vikubwa. Karibu watu 250,000 waliuawa wakati wa vita, na malaki kadhaa walikimbilia nchi jirani au Ulaya na Marekani kama wakimbizi.

Madhara ya vita kwa vijana
Madhara ya vita kwa vijana yamewekwa vizuri kwenye kumbukumbu. Mapigano yalipoanza, vikundi mbalimbali vya kijeshi vilitafuta wanajeshi kutoka kwenye rika la watoto. Pengine watoto wengi kiasi cha 250,000, wengine wadogo wa miaka 6, waliandikishwa, mara nyingi kwa nguvu. “Walilazimishwa kuwaua rafiki zao na wanafamilia wao ikiwa ni pamoja na wazazi, walibaka na kubakwa, walitumika kama watumwa wa ngono na Malaya, walifanya kazi nguvu, walitumia madawa ya kulevwa, walijihusisha na ulaji wa nyama za binadamu, utesaji na kuiibia jamii”, inasema taarifa ya tume ya Ukweli na Maridhiano ya Liberia. Wanawake na wasichana waliteseka sana. Tume hiyo ilipokea karibu visa 7,000 vya ngono ya nguvu. Wasichana na wanawake wa umri wa miaka 15 mpaka 19 walikuwa kundi kubwa zaidi lililoathirika na visa hivyo vilivyotaarifiwa.

Pamoja na miaka saba ya amani, habari mbaya bado zinaweza kutmiminika kutoka Liberia kama maporomoko ya maji. Waliberia watatu kati ya kumi wanaishi chini ya dola moja kwa siku, nusu tu ya watoto wa nchi hii wanahudhuria shule; asilimia hamsini ya kaya katika mji mkuu wa Monrovia wanaangukia kwenye kundi lenye uhakika wa chakula. Mwelekeo wa uchumi hauleti matumaini na vijana wanaorejea nchini mwao–baadhi yao wakiwa ni wanajeshi watoto wa zamani – katika uchumi unaoendelea kusababisha matatizo kwa serikali. Hili linaweza kusumbua sana hasa kwa sababu nusu ya idadi ya watu Liberia ni wenye umri chini ya miaka 20.

Katika blogu ya Ceasefire Liberia, mradi wa Rising Voices, Stephen R. Johnson anaandika:

Vijana wa Liberia wanakabiliwa na changamoto nyingi katika kupata elimu ambayo itawapatia amana ya ujuzi na ufahamu kuwa wazalishaji katika soko la leo la ajira. Matokeo yake, mpito kutoka shule kwenda kazini mara nyingi zaidi huwa bila mafanikio na vijana wanaishia kuwa ama wasio na kazi au wenye kazi duni zisizo rasmi katika maeneo ya vijijini, mijini midogo na mijini.

Bado, nchi hiyo na watu wake wameazimia kuiacha nyuma historia yao. Uchumi wa nchi hiyo umekuwa ukikua na serikali inaimarisha miundombinu. Makundi kama YMCA yamekuwa yakiwafunza wapiganaji wa zamani kwa ajili ya ajira au kuanza biashara zao wenyewe.

Umasikini na maamuzi magumu
Hata hivyo, matatizo yanayoendelea ya uchumi yamesababisha madhara mengi katika maeneo mengine. Umasikini umewalazimisha wanawake kufanya maamuzi magumu na ya hatari kuhusiana na maisha yao ya kimapenzi, anasema Jerry B. Tarbolo Jr, kutoka Umoja wa Vijana wa Liberia. Anasema mchanganyiko huu umesaidia kukuza kiwango cha maambukizi ya VVU/UKIMWI katika maeneo ya mijini nchini Liberia. Kama hali hii itaendelea, ugonjwa huu utaathiri vibaya kizazi kipya, anasema, ambacho ni moja ya vyanzo vikuu vya Liberia.

Uhusiano kati ya kujikimu kiuchumi na ngono za nguvu vina kumbukumbu ndefu nchini Liberia. Utafiti wa UNFPA wa mwaka 2008 kwa wanawake wa jimbo la Lofa nchini Liberia uligundua kwamba wakati wa vita, wanawake tisa kati ya kumi walipoteza njia zao zinazowawezesha kuishi, asilimia 96 walipoteza malazi na karibu asilimia 75 waliwapoteza ndugu zao. Zaidi ya nusu ya wanawake walikuwa waathirika wa ngono za nguvu, na kati ya hao, nusu waliripotiwa kutoa ngono kama namna ya kupata upendeleo wa namna fulani.

Imani potofu za VVU/UKIMWI
Paulie Wleh, muuguzi mnasihi wa Kituo cha vijana cha YMCA mijini Monrovia, anasema kitu kimoja ambacho Waliberia vijana leo wanakihitaji ni elimu kuhusu afya ya ngono. Alizungumza na mwandishi wa Merlin, AZISE ya kimataifa inayojenga huduma za afya katika mazingira magumu.

“Miaka ya migogoro hapa iliharibu mfumo wetu wa zamani wa elimu na kubomoa huduma za afya ndio maana vijana leo wanajua kidogo sana kuhusu VVU/UKIMWI. Kwa sababu ya kutokuwa na uelewa, kuna unyanyapaa wa hali ya juu na mikanganyiko kuhusiana na UKIMWI sasa. Vijana wanaogopa kuzungumza na wazazi wao na hakuna upatikanaji wa taarifa. Lakini wanaweza kunijia wenyewe wakati wa michezo ya mpira wa kikapu au baada ya ziara ya kutembelea maabara ya tarakilishi kuniuliza maswali, kupata huduma na ushauri. ”

Anasema mabadiliko mengine katika dhana yamekuwa dhahiri.

“Katika kipindi cha miaka miwili tangu kituo kifunguliwe, nimeona maelfu ya vijana lakini kati yao 291 walipata vipimo vya VVU. Ingawa watu wanahitaji sana kuongea nami, ni nadra sana kushawishika kuchukua vipimo vya VVU kwa sababu wanaogopa.”

Wengi wao wanaochagua kutokupima afya zao, wanadai ‘watakuja siku nyingine,’ au kwa ukweli zaidi ‘sipendi kujua hali yangu, kwa sababu sitaki kuhofu.’

Vita vya uelewa
Ukwepaji huu wa jamii ni kile kilichofanya vipindi kama “Na tunzungumze kuhusu ngono” vibuniwe kuwaelimisha kinyume chake. Kipindi hicho cha kila wiki cha urefu wa dakika 30, kwa ufadhili wa UNFPA, kinawapa wasikilizaji wake dakika 30 za taarifa na mazungumzo kuhusu ngono na masuala ya afya ya uzazi, vyote vikiwa vimelengwa kwa vijana. Kila kipindi kinatafitiwa na kuandikwa na watangazaji wanne, wanaodhibiti utaratibu mzima, ikijumuisha utafiti, kuandika na kuigiza kila kipande.

“Kazi yangu kama mtangazaji mwenza wa kipindi cha ‘Na tuzungumze kuhusu ngono’ imenipa ufahamu wa namna ya kufanya kazi kwenye uhalisia unaokabiliwa na vijana wenzangu wa Kiliberia katika vita dhidi ya VVU,” Mahmud Johnson anaandika. Anasema huwezi kutenganisha matatizo ya kiuchumi ya Liberia na masuala yanayohusu afya ya ngono.

Kama timu ya kivuko ya kipindi hicho kwa kawida hutembelea kwenye maeneo ya makondeni na vijiji kwa ajili ya kipindi kuwafundisha vijana kuhusu VVU, nimeelewa sasa, kwa uzoefu wangu wenyewe, kuhusu masuala ya kiuchumi na kiutamaduni wanayokabiliana nayo watu wengi, na namna masuala hayo yanayochangia kusambaza virusi vya UKIMWI nchini Liberia. Nimeelewa pia imani potofu ambazo vijana wanazikumbatia kuhusu usambazaji virusi vya UKIMWI na matibabu yake. Asilimia kubwa kabisa ya vijana nchini Liberia haina ufahamu kuhusu uambukizaji na kukabiliana na VVU, na dhana hii imetokana si kwa sehemu ndogo, na kiwango kinachotisha cha ujinga (wa kutokujua kusoma na kuandika.) Hata vijana wanaokwenda shule wana taarifa kidogo sana kuhusu VVU, kama mfano masuala ya afya ya uzazi hayafundishwi kabisa katika shule za Liberia. Matokeo yake, imani potofu zinawafunika vijana kuhusu VVU na magonjwa mengine yanayoenezwa kwa ngono, zaidi ni imani kwamba kuvuta bangi kunazuia maambuzi ya VVU. Kwa sababu ya imani hizi zenye hatari, kipindi cha redio kilianzisha sehemu ya “Imani zikipambanishwa na Ukweli wa mambo”, ambapo (katika lugha ya mtaani ya Kiliberia) tunazizungumzia imani hizo kwa mtindo wa kila wiki.

Kipindi kinatoa nafasi muhimu kwa vijana kujifunza kuhusu virusi. Na, bila ya shaka, kuzungumzia ngono.

Leo, kipindi cha redio cha “Na tuzungumze kuhusu ngono” kinarushwa kote nchini Liberia, na kinatumia namna nyinginezo za kusisitiza kama vile vipeperushi, maigizo, maonyesho ya barabarani, majadilioano ya makundi lengwa, na elimu rika kusambaza ujumbe kuhusu maambukizi ya VVU na namna ya kuepuka mimba zisizotarajiwa. Kipindi hiki ni maarufu kiasi kwamba Walaiberia wengi hata wamekitumia kipindi kutania juu ya upungufu wa hivi karibuni wa wayai ya kuku katika masoko ya Liberia: Kuku wa Liberia sasa wanasikiliza kipindi cha “Na tuzungumze kuhusu Ngono!” na wanafanya ngono salama! Ninajua uhalisia kwamba si kila kijana nchini Liberia atafanyia kazi jumbe zinazotolewa kwenye kipindi. Lakini hata kama maisha ya mtu mmoja tu yatabadilika katika mchakato huo, hilo litakuwa ni fanikio kwangu kama mtangazaji mhanga wa kipindi cha “Na tuzungumze kuhusu Ngono.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.