Haiti: Pesa Zinazotumwa na Ndugu na Jamaa Zasaidia Kabla ya Misaada Rasmi

Huku simu zikiwa zinaanza kufanya kazi tena nchini Haiti, pesa zinazotumwa na ndugu walio nje ya nchi “kwa waya” zinaanza kuwasili tena, na kusaidia ujenzi hata kule ambako mashirika ya kimataifa bado hayajafika. Pesa zinazotumwa na wanafamilia wanaoishi nje ya nchi, kwa uchache, zilikuwa kama asilimia thelathini ya Mapato ya Taifa ya Haiti kabla ya tetemeko la ardhi la Januari 12.

Jamii kubwa mbili za kiHaiti zilizo nje ya nchi hiyo ni zile za katika Jamhuri ya Dominika na Marekani. Kati ya Wahaiti laki 4 na laki 6 wanaishi katika mataifa hayo jirani. Wengine 80 elfu – laki 1 wanaishi katika mataifa mengine ya Karibea au Ufaransa. Jedwali hili kutoka Benki ya Maendeleo ya Mataifa ya Marekani, ambalo linatoka kwenye utafiti wa mwaka 2006, linadai kuwa Wahaiti wanaoishi Marekani walituma Karibu ya dola bilioni 1.9 za Kimarekani kiola mwaka kwenda nyumbani.

Kuanguka kwa mfumo wa huduma za simu, na katika kesi nyingine majengo yalikuwa na ofisi za benki au huduma za kutuma pesa, kulikata njia ya pesa. Lakini wiki hii foleni ndefu zilionekana nje ya ofisi za kutuma na kupokea pesa, kama vile katika ofisi hii ya CAM katika Carrefour, kusini-mashariki ya Port au Prince, kama ilivyopigwa picha na Georgia Poppelwell.

Japokuwa mji mkuu uliangaliwa zaidi na vyombo vya habari, pesa zinazotumwa na wanafamilia si lazima ziwasili hapo. Jumuiya ya Kimataifa ya Mitandao ya Kutuma na Kupokea Pesa, jumuiya ambayo inawakilisha makampuni yayosafirisha pesa kwa njia ya umeme (au waya) inasema kuwa Karibu ya nusu ya fedha zilizotumwa kwenda Haiti kutokea Marekani, ambayo ni chanzo kikubwa cha pesa zinazotumwa, zilitumwa kwenda vijijini. Hilo ni jambo muhimu kwani maeneo hayo yamekuwa na ongezeko la watu, kwani watu waliopoteza makazi kutokana na tetemeko la ardhi wanakwenda kuishi na familia pamoja na marafiki katika miji waliyotoka na sehemu ambazo hazikuharibika sana.

Dilip Ratha, Mchumi wa Benki ya Dunia, anadai kwenye blogu ya benki hiyo kuwa pesa zinazotumwa zinaweza kufanya kazi muhimu pamoja na ile hadhi ya uhamiaji ya dharura iliyoongezwa ya “kinga ya muda” (TPS) kwa Wahaiti laki 2 wanaoishi nchini Marekani .

Ikiwa TPS imepelekea ongezeko la asilimia 20 kwa wastani wa pesa zinazotumwa na kila mhamiaji, tunaweza kutarajia ongezeko la dola 360 za pesa zinazotumwa kwenda Haiti katika 2010. Na zaidi ya hilo, kama hadhi ya TPS itaongezwa muda wa zaidi ya miezi 18 ambayo imewekwa sasa – kuna uwezekano mkubwa wa kuongezwa muda wa (TPS) tukiangalia historia ya kuongezwa muda wa TPS kwa ajili ya El Salvador, Honduras, Nicaragua, Somalia na Sudani – ziada katika fedha zinazotumwa nchini Haiti itavuka dola bilioni katika miaka mitatu. Huo utakuwa msaada wa fedha wa dola bilioni moja ambao umeambatana na imani pamoja na ushauri, kadri ya mahitaji ya mpokeaji. Misaada ya fedha yaani zile zinazotumwa na ndugu walio nje ya nchi huwa ni ya kwanza kuwasili wakati wa shida. Pesa zinazotumwa na ndugu na marafiki kwenda Haiti zitaongezeka mwaka huu, kama ambavyo imewahi kutokea kila wakati na kila sehemu zilizopatwa na majanga.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.