Thailand: “Tumechoshwa na Wizara ya Utamaduni”

“Tumechoshwa na Wizara ya Utamaduni ya Thailand”

Ukurasa huu wa Facebook ulianzishwa na raia wa mtandaoni wanaokosoa njia na sera za Wizara ya Utamaduni ya Thailand. Wizara hiyo imekuwa ikidhibiti sana uhamasishaji na usimamizi wa utamaduni wa asili wa Ki-Thai katika tovuti za vyombo vya habari vya kizamani na hata vile vya kisasa. Mpaka kufikia hivi punde (11.01.2010), ukurasa huo tayari umetembelewa na mashabiki wapatao 2,857.

Ukurasa huo wa Facebook pia ulikuwa ni kama jibu kutokana na mwitikio uliotiwa chumvi uliofanywa na wafanyakazi wa wizara hiyo kuhusu mtiririko mmoja wa mijadala ulioanzishwa na mfanyakazi mmojawapo wa wizara hiyo katika tovuti moja maarufu iitwayo Pantip. Lengo la mfanyakazi huyo lilikuwa kupata maoni kutoka kwa watu kuhusu utendaji wa wizara hiyo. Jukwaa hilo la mtandaoni liliamsha majadiliano ya kusisimua, ambapo kulikuwa na ukosoaji wa kujenga kuhusu utendaji wa wizara hiyo. Lakini watendaji wa Wizara hawakupendezwa na maoni yaliyokuwa hasi. Kwa hiyo, wizara hiyo ilimwamuru mfanyakazi wake huyo kujitambulisha yeye ni nani na kutoa tamko hadharani la kuomba radhi.

Mfanyakazi huyo aliyeanzisha mtiririko huo wa mtandaoni na aliyejitambulisha kama Sampan Ruksa aliandika barua ya kuomba msamaha kwa kitendo chake. Alianza kwa kusema kwamba halikuwa kusudio lake kujenga hisia za kutoiheshimu wizara hiyo kwa kuanzisha kwake majadiliano hayo ya mtandaoni katika Pantip, hasa ukizingatia kwamba tovuti hiyo ni maarufu na yenye kuheshimika.

Pantip ni tovuti yenye ubora wa hali ya juu na yenye kusimamiwa na bodi inayotambulika. Wale walio kwenye bodi hiyo ni wanachama ambao hawana budi kupeleka vitambulisho vyao vya kitaifa na kuonyesha anwani za kompyuta zao. Majadiliano katika tovuti hii ni ya kiungwana zaidi kuliko katika tovuti nyingine yoyote.

Sampan aliwaomba radhi wakubwa wake na wenzake katika wizara.

Mimi, Bw. Samphan Ruksa, nilianzisha mtiririko wa majadiliano mwanzoni mwa mwezi uliopita katika tovuti ya bodi ya Pantip.com, Larn Dham Sewana, na MThai. Niliwasiliana na msimamizi wa Dham Sewana mwanzoni mwa mwezi uliopita ili kuomba kwamba mtiririko huo uondolewe kwenye tovuti.

Naamini kwamba vitendo vyangu hivi havikuwa na manufaa yoyote kwa Ofisi Inayosimamia Utamaduni, na mbaya zaidi, nimesababisha kuvunjika moyo na kukosa raha kwa wafanyakazi wa kitengo hicho. Ninakubali kwamba vitendo vyangu hivi vilikuwa kwa sababu ya kutojua, kukosa uzoefu, ujinga, na kukosa uelewa kabisa wa kazi zinazofanywa na wenzangu. Kwa kuongezea, nilifanya yote hayo pasipo kuwashirikisha wakubwa zangu, nilifanya kazi isiyo yangu, bila kupima vizuri, na pasipo usahihi, hasa kwa kuruhusu watu walio nje ya ofisi hii kukosoa kazi za ofisi kwa kina kiasi hata cha kukosoa watendaji binafsi.

Kwa hiyo, ambaye ndiye niliyesababisha uharibifu huu nakubali kuwajibika nikikiri kwamba vitendo vyangu havikuwa makini. Ninamwomba msamaha kila mfanyakazi katika Ofisi ya Wizara Ya Utamaduni. Natambua wazi kwamba kuna sera inayoelekeza kuwa kila mfanyakazi afanye kazi ili kuinufaisha jamii na taifa letu. Wafanyakazi hao ni watu wanyoofu na wavumilifu kwa usumbufu na mambo mengi magumu, na wamejitoa kabisa katika kulitumikia taifa. Nimehuzunishwa sana na yote haya.

Kwa upande wake, Kong Rithdee, katika makala aliyochapisha kwenye blogu inayoitwa Bangkok Post, alishambulia vikali vitendo vya watendaji wa Wizara hiyo.

Kadiri mrengo wa kihafidhina wa wizara hii – ambao kwa bahati mbaya ndiyo ulio na nguvu zaidi – unavyozidi kuonyesha kushindwa kwake vibaya kuelewa yale yanayotokea nje ya magamba waliyojijengea wenyewe kuhusu “maadili” na “mambo ya kuthaminiwa”, ndivyo kadiri hiyohiyo wanavyozidi kukoleza moto wa kuchanganyikiwa na siasa kali. Kadiri wanavyojitahidi kudhiti na kubana, ndivyo kadiri hiyohiyo watakavyowachochea watu kujiingiza kupitia njia za chini kwa chini ili kukabiliana na hali hiyo – na mwishowe nguvu ya teknolojia itakuwa upande wao.

Maskini Wizara hii. Bado hawajui kwamba utamaduni wa muhimu zaidi ni ule ulio wa kufanya ukosoaji wa kujenga na kuruhusu fikra huru.

Akitoa maoni yake kuhusu ukurasa wa Facebook, Natnaree Uriyapongson anatoa ushauri huu:

Wizara ya Utamaduni haina budi kufanya kitu kuhusu tatizo la ongezeko la makahaba wanaozidi kuigubika nchi yetu badala ya kulifumbia macho na kulitumia “eti kuhamasisha” uchumi wetu!!

Nchini Thailand, raia wanaweza kupiga simu ya moja kwa moja na kulalamikia picha, maonyesho, na matukio yasiyowakilisha vema utamaduni wa Ki-Thai. Jarida la Filamu la Thailand linaripoti:

Piga simu namba 1765. Nchini Thailand kuna namba ya simu unayoweza kupiga pale unapoona kitu chochote ambacho pengine hakiko sawa – warembo waliovaa mavazi yasiyo ya Ki-Thai, kupotoka, nyimbo au filamu zenye ujumbe mkali wa matusi – chochote kile unachofikiri kwamba kinarudisha nyuma maendeleo ya kijamii, Taifa na “utamaduni mzuri usio na doa wa Ki-Thai”.


“Kikosi cha polisi cha utamaduni”
cha Thailand kina jumla ya watu milioni 1.3 wanaojitolea na ambao wanatoka katika mitandao ipatayo 4,825 kutoka kote nchini humo. Hawa wana kazi kubwa ya kufuatilia maonyesho ya Televisheni, tovuti, na matukio ya vyombo vya habari ambayo yana nafasi ya kusababisha uharibifu au upotoshaji wa utamaduni wa Ki-Thai.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.