Urusi: Simulizi Tatu za Umaskini Uliokithiri

Mwandishi wa habari mpiga picha wa Urusi, Oleg Klimov, hivi karibuni alitumia saa mbili kusubiri treni katika kituo cha treni cha Syzran, ambalo ni jiji katika eneo la Samara la Urusi. Wakati akiwa pale, aliingia kwenye mazungumzo na baadhi ya wenyeji pale na kisha kuandika simulizi zao za umaskini uliokithiri kwenye blogu yake.(RUS)

Kisa #1:

[…] Mama mtu mzima, binti yake, na mjukuu mwenye miaka kama 5 hivi. Hawa wamekuwa wakiishi katika kituo cha treni kwa siku mbili. Wamekosa kiasi cha rabo 400 (kama dola za Marekani 13) ili kutosheleza kiasi (cha kununulia tikiti) kuwawezesha kufika katika kijiji chao, siyo mbali na [Penza]. Wametoka msibani. Sasa wanamsubiri ndugu yao mwanamke awasili ili kuwaletea rabo hizo 400. Ndugu huyo naye ameonekana kuchelewa, huenda ni kwa sababu yeye pia hana kiasi hicho cha fedha. Basi, waliniomba [mimi] kutuma ujumbe mfupi wa maandishi [kwa kutumia simu yangu ya mkononi]. Hawa ni watu wa kawaida wa vijijini. Labda siyo watu wenye akili nyingi na hawana elimu kubwa, lakini wako wawazi sana na wanyoofu. Sifa zenye thamani isiyo ndogo siku hizi. Pensheni ya mama huyu ni kiasi cha rabo 4,500 [kama dola za Marekani 148] kwa mwezi. Binti huyo mara nyingine hufanya kazi huko Penza, na mara nyingine huwa hana kazi. Mtoto huyo waliye naye hajaanza shule ya awali. [Sababu yake] hakuna shule ya awali. Ndugu wa kike alikuwa amefariki, walikusanya fedha zote walizokuwa nazo na kwenda kumzika. “Je, tungefanyaje? – ni muhimu kushiriki katika kumuaga binadamu mwenzenu kwa njia inayofaa …” […]

Kisa #2:

[…] Wanawake wanne kutoka jamii ya Tatar husafiri kila juma kutoka katika kijiji chao kwenda Syzran ili kutafuta fedha za kujikimu. Wakijitahidi sana wanapata walau rabo elfu moja [kama dola za Marekani 33] yaani wote pamoja, wakifanya kazi za kusafisha suhula za umma na mahali kwingineko. Hakuna kazi kabisa katika kijiji chao. “Kuna kazi, lakini hakuna hata moja inayolipa.” Hufika wakati wakakosa hata fedha ya kununua mkate. Kwa hiyo, hulazimika kununua unga wa ngano na kujiokea wenyewe mikate yao. Yote ni katika kubana matumizi. Pia wana viazi mbatata vyao wenyewe. Na kabeji na pilipili hoho. Lakini hawana fedha. “Ni vigumu kuishi, ni vigumu sana. Ni rahisi kufa…” […]

Kisa #3:

[…] Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 55 au zaidi kidogo. watoto wake walimfukuza kutoka kwenye nyumba yake mwenyewe. Yaani walichomwambia ni: “Toka hapa, kwenda zako … Mara nyingine huwa ninakaa na watu niliowazoea, na mara nyingine katika kituo cha treni. Nafanya kazi za hapa na pale …” Hajichukulii kuwa hohehahe, kwa sababu “hakuna watu hohehahe katika mji mdogo. Watu husaidiana.” Amebeba chai iliyopoa katika chupa ya plastiki. Mkate na vipande vya nyama iliyosagwa vinavyotoa harufu ya ajabu vimefungwa kwenye tambara. Baada ya kula nyama hiyo na kuishusha na chai ile iliyopoa, analala usingizi kwenye benchi la kukalia lililo pale kwenye kile kituo cha treni. Yaani alichofanya ni kuinamisha tu kichwa chake na kupitiwa na usingizi mara. […]

Klimov anamalizia makala yake kwa hisia kali, anaandika kusema “Inasikitisha mno kuona mambo yote haya,” na kwa kusema ukweli simulizi kama hizi ni nyingi hasa katika “‘Urusi hii ya Putin’ yenye muonekano wa kilimbwende’”:

[…] Wewe pia unaweza kutumia walau saa mbili kukaa pale na kuandika simulizi yako. Bila kutoa maoni. Unachopaswa kufanya ni kusikiliza na kuandika mambo mbalimbali ambayo watu wanaelezana. Ni rahisi sana. Mwandishi yeyote wa habari anaweza kufanya jambo hilo. Lakini, hakuna ubishi kwamba uchambuzi yakinifu wa kiakili ni jambo la lazima. […]

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.