Philippines: Mti wa Dita Waokoa Maisha ya Watu 36 Wakati wa Mafuriko


Mti wa aina ya m-dita wenye futi 40 ulikuwa kimbilio la hifadhi kwa watu 36 wa familia saba huko Barangay Bagong Silangan (kijiji cha New East), kwenye mji wa Quezon, Metro Manila wakati maji yalipofurika tarehe 26 Septemba. Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa iliyovunja rekodi iliyotokana na kimbunga cha Ketsana kilichoikumba nchi ya Ufilipino mwezi Septemba. Ilikuwa ni gharika mbaya zaidi kutokea nchini katika miaka 40 iliyopita.

Kuna miti michache ya mi-dita iliyobaki kwenye maeneo ya Manila mjini. Barangay Bagong Silangan ni jamii masikini ya mjini iliyo sehemu ya kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa nchi. Zaidi ya watu 30 walipoteza maisha yao katika jamii hii wakati wa janga la mafuriko haya.

Arkibong Bayan anatoa undani zaidi wa tukio hili:

Watu 36 wa familia 7 walipanda mti huu wa m-dita wakati maji yanayofurika yalipokuwa yanaongezeka na waliokoka. Walibaki kwenye matawi ya mti huu kuanzia saa 4 asubuhi ya terehe 26 mpaka saa 9 alfajiri ya siku iliyofuata walipoteremka, na maji yakiwa usawa wa kiuno kwa sababu walipatwa na baridi kali na njaa kwa masaa 17. Kati yao mkubwa kuliko wote alikuwa na miaka 60 na mdogo zaidi alikuwa na umri wa majuma mawili tu.

Somo la kimaadili: Usikate miti, inaweza kuyaokoa maisha yako siku moja. (Katika suala hili, kwa maana ya moja kwa moja.)

Walionusurika wanasema kwamba kulikuwa pia na majoka makubwa yaliyokuwa yakitafuta hifadhi kwenye mti huo.

Ukiacha mti huo wa m-dita, kulikuwa na mti mwingine ambao wakazi wengine walidai kuwa nao pia uliokoa maisha ya wanakijiji wengine.

Sabi ng mga taong nakausap namin nung magpunta din kami dun, maliban sa dita tree, may isa pang puno dun na mas manipis pero mataas din. doon daw sumabit yung isang pamilyang nakasakay sa yero. Meron ding 2 month old baby na natangay ng agos sa puno kaya sinungkit din nila.

Kwa mujibu wa baadhi ya wanakijiji, kuna mti mwingine (mdogo kuliko m-dita) ambao ulitumiwa na familia kama hifadhi ya muda. Kulikuwa na mtoto wa miezi miwili aliyebebwa na mafuriko ya maji karibu na mti. Mtoto aliokolewa pia.


KIKOSI MAALUM CHA KAZI: watu wa ‘children of the storm’ waliweza kutembelea kijiji na kundi lingine liliweza kuuona ‘Mti wa Uzima’

Tulionyeshwa pia tunaouita sasa ‘Mti wa Uzima’, m-Dita ambako familia 7 (watu 36) walitafuta hifadhi wakati wa mafuriko na wakaokoka na mafuriko ya maji.

Wakazi walionusurika, waliokuwa wanakagua nyumba zao kwa ajili ya ukarabati, walizungumzia namna walivyopanda kutoka paa hadi paa kutafuta eneo lililoinuka zaidi. Walielezea namna waliovyoweza kumwokoa mtoto wa umri wa miezi miwili kwenye paa la bati lililokuwa linaelea.

Arkibong Bayan alipokea maoni kutoka kwa msomaji aliyesimulia kuhusu jinsi mti wa mwembe ulivyookoa maisha wakati wa janga mitatu iliyopita.

Wakati wa Kimbunga kabambe kilichoitwa Reming Novemba 30, 2006, mwembe uliokoa maisha ya watu watano huko Padang, mjini Lagazpi (mkoa wa Bicol katika kisiwa cha Luzon). Mtu mmoja aliyenusurika alikuwa na machaguo mawili: Mwembe ama paa la nyumba. Akachagua mti; wale waliokuwa kwenye paa walisombwa na mafuriko kuelekea baharini.

Somo: Panda mti. Unaweza kuyaokoa maisha yako

Baada ya kunusurika na mafuriko mabaya ya mwezi Septemba, wakazi wa Barangay Bagong Silangan wanakabiliwa na changamoto kubwa zaidi: kujenga upya nyumba zao na maisha yao. Jamii imekuwa jamii iliyobadilika. Nyumba zilisombwa na maji na miundo mbinu iliharibiwa vibaya.

Tuliambiwa kwamba kabla ya Ondoy (Kimbunga cha Ketsana) eneo hilo lilikuwa lina msongamano mkubwa wa watu kama maeneo mengine ya kimasikini mijini.

Sasa, nyumba bora tu ndizo zilipona. Na eneo linaonekana kuwa wazi na kuwa na nafasi zisizo na kitu –yote kwa sababu nyumba zilisombwa na gharika ya maji iliyoleta athari mbaya.

Picha zote kwa hisani ya Arkibong Bayan

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.