Uanaharakati na Umama Barani Asia

Je, mwanamke anatoa sadaka zipi ili kupigania jambo analiamini? Je, watoto wake wanaathiriwa vipi na mateso yanayoelekezwa kwake? Makala hii inachambua kwa kifupi maisha ya wanawake wanaharakati katika Asia ambao pia ni ma-mama (wazazi).

Irene Fernandez ni mwanamke na mwanaharakati anayepigania haki za wahamiaji nchini Malaysia. Kwa zaidi ya miaka kumi, Irene amekuwa akikabiliwa na mashtaka ya ‘uhalifu wa kuvunjia heshima” (ambayo kwa sasa yamefutwa) baada ya kuchapisha memoranda akiihimiza serikali ya Maylasia kuchunguza tuhuma za mateso yanayofanywa katika kambi za wakimbizi nchini humo.

Licha ya kuwa mwanaharakati, jambo ambalo limempatia tuzo ya Right Livelihood mwaka 2005, Irene pia ni mama wa watoto watatu, Camverra Jose Maliamauv, Tania Jo na Katrina Jorene, mlezi wa watoto wengine kadhaa. Ni vigumu kufikiri kuhusu yale yanayopita kwenye vichwa vya wanaharakati kama Irene, hasa pale anapowawaza watoto wake. Wakati alipokuwa akisomewa hukumu mwanzoni mwa mashtaka mwaka 2003, Irene aliripotiwa kusema:

Nataka watoto wangu na watoto wa watu wote ninaofanya kazi nao kama kiongozi wa Tenaganita kufurahia na kuishi katika jamii iliyo na amani, ambapo hatuogopi misukosuko inayosababishwa na dola.

Pengine dhima ya Irene kama mama inaelezwa vizuri zaidi katika macho ya binti yake, Katrina Jorene, ambaye aliandika katika blogu inayoitwa Micah Mandate (blogu ya Kikristu inayolenga kuamsha utetezi wa umma):

Ninampongeza mama yangu ambaye alinilea niwe mstahimilivu katika maisha na kuwa wazi na king'ang'anizi wa kutafuta ukweli na katika haki, kweli na haki. Ninawapongeza mashujaa wasio na idadi ambao nimekuwa nao maishani mwangu, hasa wanafamilia yangu na familia ya Tenaganita [Taasisi anayoongoza Irene Fernandez]. Ninawapongeza wote waliofanya kazi kimya kimya, pasipo kuchoka na kwa umakini mkubwa kwa miaka yote hii ili kupigania manufaa ya umma mpana zaidi.

Yaelekea mafunzo ya Irene yamemvuta walau mmoja wa watoto wake kuchukua mrengo wa uanaharakati kama alivyo yeye mwenyewe. Hivi sasa Katrina huandika makala mbalimbali zinazohusiana na haki na utetezi wa walio wachache katika jamii.

Tofauti na ilivyo kwa Katrina Jorene, kwa bahati mbaya, Alexander na Kim Aris, watoto wa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi, hawakupata bahati ya kujifunza kutoka kwa mama yao kwa zaid ya muongo mmoja sasa. Mapenzi ya Bibi Suu Kyi kwa nchi yake ya Myanmar yamekuwa makubwa kiasi kwamba ametumikia kifungo cha nyumbani kwa takribani miaka kumi na nne katika nyumba iliyo kandokando ya ziwa huko Yangon, ambapo amechagua kuishi kwa kuhofia kwamba huenda utawala wa mabavu wa kijeshi hautamruhusu tena kurudi ikiwa atatoka. Blogu inayohusu wanawake ya Womensphere inaandika:

Mume wa Bibi Suu Kyi, aliyekuwa raia wa Uingereza na mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Oxford, Michael Aris, alifariki kwa kansa mwaka 1999 akiwa na umri wa miaka 53. Mama huyu hakuweza kumwona mumewe wakati alipokuwa anafariki – serikali ya kijeshi ilimkatalia mume huyo viza ya kuingia nchini, wakati kwa upande wake mama huyo naye alihofia kutoka Burma, kwamba pengine asingeruhusiwa kurudi tena nchini humo. Kwa hiyo hajakutana na watoto wake wawili, ambao hivi sasa wana umri wa zaidi ya miaka thelathini, kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Kuna machache sana yaliyoandikwa juu ya (au kuandikwa na) Alexanderson au Kim. Hata hivyo, mnamo mwaka 1991, mtoto mkubwa wa Bibi Suu Kyi, Alexander, alipokea tuzo ya Amani ya Nobel huko Oslo kwa niaba ya mama yake. Hapa tena, tunaweza kutumia lensi za mtoto huyu ili kupata kumwelewa vema zaidi Bibi Suu Kyi kama mama:

Nikizungumza kama mtoto wake, ningependa kuongeza kwamba mimi binafsi naamini kwamba kwa kujitolea kwake na kutoa sadaka yake binafsi, ametokea kuwa alama yenye thamani ambapo kupitia kwake, mateso ya watu wote wa Burma yametambulika. Na, hakuna aliye na haki ya kuyapuuza mateso hayo.

Pia tukumbuke kwamba, mapambano yake akiwa katika upweke wake huku akiwa chini ya ulinzi mkali katika makazi yake ya huko Rangoon ni sehemu ya mapambano mapana zaidi, ulimwengu kote, katika kutafuta kuikomboa roho ya kibinadamu kutoka katika tawala za kimabavu za kisiasa na manyanyaso ya kisaikolojia.

Ingawa mama yangu anaelezwa mara nyingi kama mpigania haki za kisiasa na ambaye anajaribu kwa njia za amani kuleta mabadiliko ya kidemokrasia, hatuna budi kukumbuka kwamba mapambano yake, kimsingi, ni ya kiroho.

Ni matumaini yangu kwamba hivi karibuni mama yangu ataweza kuwashirikisha hisia zake na kuzungumza moja kwa moja yeye mwenyewe badala ya kuzungumza kupitia kwangu.

Wakati huo huo, wanawake wengi wanaharakati barani Asia wanaendelea kukabili mateso. Kwa mfano, Fan Guijuan, ambaye nyumba yake iliamriwa kubomolewa sababu ya Mradi wa Shangai World Expo, alikamatwa huko Beijing na kurejeshwa Shanghai, na kisha kuwekwa kizuizini. Mtoto wake wa kiume hana mahali pa kuishi, kwa sababu ya bomoabomoa hiyo. Wakati huohuo, huko Ufilipino, Dkt Edita Burgos, ambaye ni mama wa Jonas Burgos, anapigania haki ya mtoto wake huyo mwanaharakati, ambaye inasemekana “ametoweka“. Dkt Burgos ni mwenyekiti wa chama cha haki za Familia za watu Waliotoweka, yaani asasi inayotafuta haki za watu waliopoteza maisha yao pasipo kujulikana, jambo ambalo linasemekana ni kielelezo cha utawala wa Arroyo.

Hivi sasa, huko Irani, akina mama wanaharakati wa haki za binadamu, wanazidi kuwa alama za ulimwengu katika kupigiania haki za binadamu ulimwenguni kote. Katika mgomo baridi wa kimyakimya ulioshirikisha umma, ‘Akina Mama Wanaoomboleza wa Irani‘, ambao wanajulikana huko Tehran kama “Akina Mama wa Laleh”, kwa njia za amani wanatafuta haki kwa ajili ya watoto wao waliokufa au waliofungwa.

Mama ni mama ili mradi tu aishi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.