Afrika: Obama Atumia Nyenzo Mpya za Habari Kuzungumza na Waafrika

“Umeshawahi kutaka kumuuliza kijana wetu wa Nyangoma maswali yoyote? Kwa maneno mengine, je ungependa Rais wa Marekani, Barack Obama ajibu maswali yako?,” ndivyo inavyoanza makala kwenye blogu ya Hot Secrets inayohusu matumizi ya Obama ya zana mpya za habari ili kukutana na kuongea na Waafrika wa kawaida.

Barack Obama anazuru Ghana tarehe 10 mpaka 11 Julai. Hii itakuwa ni ziara yake ya kwanza ya kihistoria kwenye nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na atatumia nyenzo kama Twita, Facebook na Ujumbe mfupi wa Simu za kiganjani (SMS) kuzungumza moja kwa moja kwa moja na Waafrika.

Erik Hersman anayeblogu kwenye blogu ya White African, anajadili majukwaa-nyenzo ya habari ambayo Obama anakusudia kuyatumia ili kuwafikia Waafrika zaidi ya wale wa Ghana. Erik alifanya kazi na ikulu ya Marekani katika kuandaa mikakati ya nyenzo mpya za habari kwa ajili ya Ghana na Afrika. Anaandika:

Redio bado ni nia ya kwanza ya mawasiliano barani Afrika, na Ghana ina sekta ya redio iliyo hai na yenye kushirikisha jamii zilizo vitongojini na jamii ya kitaifa.
Kama kila mmoja anavyojua, usambaaji wa simu za kiganjani umekua kwa kasi ya mlipuko barani Afrika, hii inamaanisha kwamba Ujumbe mfupi wa Simu (SMS) ni njia ya kidemokrasia ya kupata mrejesho kutoka kwa watu wa kila hali nchini. (jambo la kuchekesha ni kuwa huduma hii haipatikani kwa wakazi waaoishi Marekani – mengine juu ya suala hili yapo chini)
Mwisho, hakuna mtandao wa kijamii ulioazaliwa nchini Ghana, na kama ilivyo kwa nchi nyingine kote Afrika, Facebook imeweza kusambaa kwa kiwango kizuri. Nchini Ghana, watumiaji ni zaidi 100,000, kwa hiyo inaleta maana sana kwa timu inayoshughulikia nyenzo za habari kuwafikia watu bila kuzisambaza nguvu zao kwenye huduma nyingi nyingine. Kuwa na huduma ya Twita kama nyenzo ya akiba ni jambo linalotarajiwa, kwa sababu kutakuwa na matumizi huko vile vile.

Na anatundika habari za kina kutoka Ikulu ya Marekani:

SMS. Tunazindua jukwaa la SMS ili kuwaruhusu wananchi kutuma maswali, maoni na maneno ya ukaribisho (Kwa Kiingereza ama Kifaransa). Kwa kutumia vifupisho vya tarakimu vya mahali husika kwa huduma ya SMS nchini Ghana (1731) , Nigeria (32969) , Afrika Kusini (31958) na Kenya (5683), vile vile kutumia tarakimu ndefu kwa ajili ya wengine wote duniani *, Waafrika na raia ulimwenguni kote watahamasika kumwandikia Rais ujumbe mfupi wa maneno. Washiriki wa SMS wataweza pia kuomba kupatiwa dondoo za hotuba kwa Kiingereza na Kifaransa. Nambari zitakazotumika kwa ajili ya kuandikisha simu za mkononi kwa Afrika ni: 61418601934 na 45609910343.

Redio. Hotuba ya Rais itarushwa moja kwa moja kupitia vituo vya redio vya kitaifa na vile vya kanda wakati wa hotuba. Baada ya hotuba, jumbe zote zilizorekodiwa majibu ya Rais kwa jumbe zote fupi (SMS) zilizopokelewa zitapatikana katika vituo vya redio na wavuti. Rais anatarajia kujibu maswali anuai na maoni kwa mpangilio wa mada na eneo. Sauti zilizorekodiwa pia zitapatikana kwa ajili ya matumizi ya kila mtu atakayezihitaji kupitia wavuti ya Ikulu ya Marekani na teknolojia ya iTunes.
Video. Hotuba itarushwa moja kwa moja kwenye www.whitehouse.gov/live. Alama-funguo za video hiyo inapatikana ili uweze kuitumia katika wavuti yoyote.
Mazungumzo ya moja kwa moja kwenye mtandao. Tutawezesha gumzo la mtandaoni linalihusu hotuba kwenye Facebook (itakuwa hapa http://apps.facebook.com/whitehouselive). Ikulu ya Marekani itatengeneza “tukio” la Facebook kutokana na hotuba ambapo washiriki kutoka ulimwengu mzima wanaweza kujibishana. Anuani ya Twita ( #obamaghana) pia itatengenezwa na kutangazwa ili kuboresha maoni juu ya tukio hilo.

Watumiaji wa mtandao wanaweza kutuma maswali yao kwenye wavuti ya AllAfrica:

Nafasi yako ya kumuuliza Rais Obama kuhusu Afrika:
Unataka kumuuliza nini Rais Obama anapojiandaa kuitembelea Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mara ya kwanza akiwa kiongozi wa Marekani –akitua Ghana tarehe 10-11 Julai? Andika swali lako hapa, na tutakusanya maombi yenu. Tafadhali, kama ungependa, usiasahau kutaja umri na kazi unayofanya.

Kwa mujibu wa Michael Wilkerson anayeandika katika blogu ya Foreign Policy, matumizi ya Obama ya nyenzo mpya za mawasiliano kunaweza kuongeza umaarufu wake duniani:

Kama hapatakuwa na matatizo, udhihirishaji huu wa kupenda kupata mitazamo ya Waafrika huenda utapandisha umaarufu wa Obama duniani, ambao tayari ni kama mara mbili ya ule wa Marekani yenyewe. Katika soko la kitaalii la mjini Accra, fulana za Obama na michoro zinauzwa haraka kutoka kwenye safu na Waghana wanategema kupanda kwa biashara ya utalii baada ya ziara.

Mwanablogu Ghana Pundit anaripoti kuwa maelfu ya jumbe za simu za viganjani yametumwa kwa Obama:

Rais wa marekani amepokea maelfu ya jumbe za simu za viganjani zinazoihusu Afrika baada ya kuwataka watu kumtumia maswali kabla ya ziara yake nchini Ghana siku ya Ijumaa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.