Afrika Kusini: Kuvuvuzela au Kutovuvuzela?

Mjadala kuhusu kifaa maarufu kinachoitwa vuvuzela kinachopigwa na mashabiki wa mpira wa miguu Afrika Kusini umetawala katika blogu mbalimbali duniani tangu kuanza kwa Kombe la Mabara la mwaka huu nchini Afrika Kusini, lililohitimika wiki iliyopita. Waandishi wa habari, watazamaji wa televisheni, makocha na baadhi ya wachezaji wa kigeni walitoa wito wa kusitisha matumizi ya kifaa hiki katika Kombe la Dunia la 2010 nchini Afrika Kusini. Mabishano haya yana sauti kubwa kama chombo chenyewe. Kuna hata kura ya mtandao ya kusitisha chombo hiki. FIFA imeruhusu vuvuzela litumike wakati wa kombe la dunia mwaka 2010 ikitoa hoja kwamba hiyo ni sehemu ya utamaduni wa mpira wa Afrika Kusini.

Haya ni maelezo ya Wikipedia kuhusu vuvuzela:

pembe ya kupuliza, yenye urefu wa kadiri ya mita moja , kwa kawaida hupulizwa na mashabiki katika mechi za mpira wa miguu huko Afrika Kusini. Asili ya jina hili ina utata. asili ya jina inaweza kuwa ni ya Kizulu yenye maana ya “kupiga kelele,” inayotokana na sauti kupulizwa kwake ya “vuvu” , au kutokana na lugha ya mtaani inayohusiana na neno “kuoga”

Mitazamo katika ulimwengu wa blogu imepishana sana. Wanablogu wengine wanakerwa na sauti inayotoka kwenye vuvuzela wakati wengine wanatoa wito wa watu kuwa na uvumilivu pamoja na uelewa wa mambo. Mwanablogu mmoja amefika mbali ha hata kudai kwamba kifaa hiki kinaeneza virusi vya UKIMWI!

Dave Taylor anaelezea vuvuzela kama “kifaa cha asili cha ghasia za mpira wa miguu”

Kwa Chris wa blogu ya Kombe la Dunia, vuvuzela ni “ile sauti kubwa ya jeshi la wadudu (kama vile nzige)”:

Ile sauti kubwa kama ya kundi kubwa la nzige ambayo umekuwa ukiisikia katika kila mchezo Kombe la Mabara si, kwa hakika, mojawapo ya yale ‘mapigo’ yanayoelezwa katika biblia. Hiyo ndiyo inaitwa vuvuzela…

Capitals Kremlin anaichukulia vuvuzela kama kipiga kelele kinachokera kuliko vyote:

Mabibi na Mabwana, Caps Kremlin anayofuraha kuwaletea: kipiga kelele kinachokera zaidi duniani, vuvuzela.

Kuna maelezo marefu ya vuvuzela kutoka 24.com:

…chukua mchezo kutoka Uingereza unaoitwa kandanda, chukua kamasi ya kinyago chenye macho yanayong'ara na pua yenye unga ya mfanyabiashara wa kutangaza bidhaa, pamoja na wabia wa makampuni ya pombe ambao wanataka kuongeza hisa kwenye soko la biashara, muongeze jamaa aitwaye Van Schalkwyk mwenye ile akili-ya-kuhepa uchanganye na kiwanda cha plastiki, unajua unapata nini? Vuvuzela.

Pitch Invasion anaiita vuvuzela “Chombo cha Shetani.

Karibu kwa plastic Africa:

halafu fuaatilia na mapigo makali ya taarifa rasmi za kutangaza habari juu ya jinsi pembe-ya-kudu ulivyokuwa ikitumika zama za kale kupiga mbiu za kuitawanakijiji mkutanoni, Vikundi vya wakristo vikidai kuwa hiyo ni sehemu ya ibada zao takatifu na tunaishia na mechi za soka ambazo zinaweza kuangaliwa kwenye televisheni pale tu sauti ikiwa imeminywa. Na kama huipendi (vuvuzela), ni lazima uwe mbaguzi au mbaya zaidi kati ya wale jamaa ambao wakisikia neno “utamaduni” tayari huanza kuzifikia bunduki.

Karibia kwenye blogu ya Afrika plastiki. Na usikitikie fursa iliyopotea.

Kutoka blogu ya Foreign Policy, “Jambo kubwa zaidi katika kombe la Dunia ni tarumbeta,”

Miaka mitano nyuma, wakati Afrika kusini iliposhinda haki ya kuandaa Kombe la Dunia la mwaka 2010, wengi walitaka zaidi kujua ikiwa nchi hiyo ilikuwa na miundo mbinu inayohitajika kuwa mwenyeji wa mashindano haya makubwa. Mwaka moja tu ukiwa umebakia, ingawa, waangalizi wengi wanakubaliana kwamba nchi imeshinda mtihani huo; badala yake, walalamikaji wakubwa wanatumia muda mwingi kulalamikia chombo kinachoitwa vuvuzela.

ReasonCheck anawaza, “…laiti haya mapagani zuzu yangejua furaha ya kutengeneza nota za muziki kwa kutumia mabomba haya ya jehanamu”:

Kama ulifanikiwa kuipata mechi yoyote kupitia luninga, bila shaka ulisikia sauti mbaya, kama ya kundi la wadudu wanaoleta kero. Lakini pengine inabidi kuwa pale kuielewa kero hasa ya kelele ile mbaya. Nilimchukua mwanangu kwenda kwenye mchezo usiku wa siku chache zilizopita na tumekuwa tukitaabika na kuumwa kwa vichwa tangu wakati huo, na ninashitukashituka wakati nikilala.

Ndipo nikawaza kwamba ikiwa haya mapagani zuzu yangeonyeshwa furaha ya kutengeneza nota za muziki kwa kutumia mabomba haya ya plastiki basi pangeweza kutokea mabadiliko ya kifikra kati yao na wangejaribu kuanza kupiga muziki.

Pitch Invasion anaangalia historia ya upigaji kelele kwenye mpira wa miguu duniani akianzia na kipiga kelele maarufu Uingereza, yale manyanga au machekeche ya mbao:

Kipiga kelele maarufu cha kwanza mpirani – na kilichokuwa kinapiga kelele hata kuifanya vuvuzela kunyong'onyea – kilikuwa ni lile chekeche la mbao huko Uingereza.
Akiandika katika jarida la Guardian, Simon Burnton alitegemea kwamba “huenda Afrika Kusini ingejifunza kutoka kwenye yale manyanga ya mbao yaliyotumbuiza kandanda la Uingereza katika kipindi cha baada ya vita –na yaliyopoteza umaarufu wakati kila mmoja alivyogundua jinsi yanavyokera. natumaini kuwa siku hivi karibuni hatima mthili ya hiyo itayafikia haya mavuvuzela.”
Hata hivyo, ni mageuzi ya kimsingi katika utamaduni mzima wa mashabiki na siyo utambuzi kwamba manyanga yale yalikuwa yanakera,ndiyo yaliyoyaondoa manyanga yale kwenye viambaza.”
Ingawa ni chombo kilichojitokeza hivi karibuni tu katika mapambano ya kandanda, kuna baadhi ya watu wanaohusianisha asili yake na utamaduni wa Kiafrika. “Asili ya vuvuzela inasemekana kuwa ni pembe la mnyama kudu liitwalo ixilongo kwa kiXhosa, mhalamhala kwa kiTshivenda –linapulizwa ili kuwaita wanakijiji kwenye mikutano.
Inaonekana vuvuzela lilianza kutumika mwaka 1992 katika mapambano ya mpira wa miguu huko Afrika Kusini, na wapenzi wa Timu ya AmaZulu. Mashabiki walitengeneza pembe kutokana na makopo yaliyotupwa, kwa furaha ya wengi na kero kwa wengine: Mwandishi wa Afrika Kusini Jon Qwelane aliandika mwaka 2007 kwamba “Siku hizi, kuna kifaa kilichotokea kuzimu, kinachoitwa vuvuzela, ambacho kimepelekea uamuzi wangu wa kuacha kuhudhuria mechi na badala yake kuzianngalia kwenye televisheni, huku sauti ikiwa imeminywa kabisa.”
Katika miaka ya 2000, huku Afrika ya kusini ikiwa imewasilisha maombi ya kuandaa Kombe la Dunia, vuvuzela ilizalishwa kwa wingi kibiashara kutokana na msaada uliotolewa na SAB Miller (Kiwanda cha kutengeneza Pombe Afrika Kusini) kwa kampuni ya Neil van Schalkwyk ya Masincedane Sport mwaka 2001, iliyoanza kuzalisha kwa wingi toleo nafuu la plastiki.

SA Sucks anaipinga “historia” ya vuvuzela kama “uongo wa kijinga unaosambazwa kupitia Wikipedia”:

Kuna uongo wa ajabu unasambazwa kupitia Wikipedia (asante Karooboy kwa kuuonyesha) kwamba asili ya vuvuzela imetokana na “pembe ya Kudu” ambalo lilikuwa likipulizwa na weusi. Ilikuwa karibu nife kwa kucheka kutokana na hadithi hizi za kutunga, pengine ni jambo ambalo tungelitarajia – ukweli kuwa haya madudu maharibifu yaling'oa (tarumbeta za honi) kutoka kwenye magari moshi wakati yakifanya uharibifu wao kwa pamoja ni wazi kuwa kisiasa hautaweza kumezwa kirahisi rahisi (au kukubalika). Chini kidogo katika makala hii kuna picha ya vuvuzela la manjano lenye umbo la pembe – niliipata picha hii kwenye mamia ya barua pepe zinazoingia kutoka kwa watu nisiowajua, zikiniomba eti nikiweke “oda” 10 000 ya majitu haya, yakiwa yamebandikwa nembo yangu ya kibiashara. Umbo la pembe yenyewe liko kiajabu lakini kama ile makala ya Wikipedia, ni dhahiri kuwa makampuni ya PR wanafanya kila linalowezekana kuzika historia ya kweli nyuma ya madude haya.

Kwa mujibu wa SA Sucks hakuna jambo lolote la dhati la Uafrika kwenye vuvuzela:

Moja ya mambo ninayopenda juu ya wanasiasa wanaoendesha himaya hii ni jinsi, kwa namna watakavyoamua, wanaweza kutunga historia wakati wowote.Vuvuzela ni mfano moja wapo.
Wale wanaotetea vuvuzela wanasema kwamba vuvuzela ni sehemu ya utamaduni wa mpira wa miguu Afrika Kusini na kwamba kutokuliruhusu kuatakuwa ni uvunjaji wa haki. takataka. Yamekuwepo kwa miaka chini ya kumi. Ilikuwa mpaka mwanaharamu anayeitwa “Neil van Schalkwyk, mmiliki mwenza wa Masincedane Sport, inayozalisha mavuvuzela ya plastiki, aliposhinda Tuzo ya SAB KickSrart ya mwaka 2001, ambayo ni mradi wa kuwasaidia wajasiriamali kwa kutoa misaada na mwongozo katika kuanzisha biashara.” Ndipo vuvuzela lilipoanza kujulikana.

Dave Taylor anadhani kuwa sauti ya vuvuzela inakera na kusumbua:

Mashabiki nusu-dazeni wakiwa na moja ya madude haya, au hata mashabiki wengi wanapoyapuliza kushangilia goli ama mchezo mzuri wa kulinda goli hilo ni jambo moja, lakini wale tulioangalia Kombe la Mabara la FIFA tumejifunza kuwa, namna ya ushangiliaji nchini Afrika Kusini inaonekana kuwa ni kuendeleza kelele hii moja kwa moja wakati wote wa pambano.
Na hatuzungumzii watu ishirini ama thelathini kwenye uwanja, tunazungumzia mamia, kama sio maelfu ya wenyeji wanaoendeleza hii kelele inapasua masikio wakati wote wa mchezo.

Makelele haya ya moja kwa moja niliyaona kuwa yanakera na kusumbua, na yaliingilia kati uwezo wa kuwasikia watu wakishangilia kabumbu safi ama kuzomea maamuzi mabaya ya refa.

Language Log anasema kwamba “thamani ya vuvuzela ni sawa na pointi 23 za mchezo wa bao la maandishi hata kabla ya kupewa faida – au pengine ni sawa na hivyo, kama lingeongezwa kwenye orodha rasmi ya maneno.”

Mark Gleeson wa blogu ya Reuters blog anafikiri kwamba mwishowe pesa itazungumza zaidi ya vuvuzela lolote. Anasema mabishano kuhusu vuvuzela yamegeuka “sawa tu na mgogoro wa ukoloni mambo-leo”:

Kwa vyovyote mjadala kuhusu vuvuzela ingeanzisha kelele kubwa lakini kwa baadhi ya wachambuzi wa mambo wa Afrika Kusini mabishano hayo yamegeuka kuwa sawa na mgogoro wa ukoloni mambo-leo.
Matarumbeta yenye kelele, yanayotawala viwanja vyote wakati wa Kombe la Mabara, yaliwasababishia watu wengi kufunga masikio yao.
Malalamiko kutoka kwa watazamaji wa televisheni Ulaya nzima yamekuwa makali sana kiasi cha kumfanya mdudu huyu wa plastiki kuwa moja ya ajenda kuu katika mikutano ya waandishi wa habari na rais wa FIFA Sepp Blatter ambayo aliifanya wakati wa michuano huko Afrika Kusini.

Mwishoni mwa siku, ni fedha za televisheni ndizo zitakazoongea. Kama watangazaji wakubwa wa matangazo hayo wataihisi kero inayosababishwa na mavuvuzela kiasi cha kuwaondolea raha ya kutazama kwa watazamaji wao, FIFA italazimika kujirudi na kuyasitisha mavuvuzela kwenye viwanja vitakavyotumika kwenye mechi za Kombe la Dunia mwaka 2010. Uamuzi huo hautajali itikadi yoyote bali pesa.

Bob wa blogu isiyo rasmi ya DC United hawaelewi wale wanaoichukia vuvuzela:

Binafsi siwaelewi wanaoichukia vuvuzela. Ninahisi watu wengine hawana uwezo wa kuchuja hizi kelele zinazotoka kwa wapiga kelele walio kwenye majukwaa ya uwanjani wakati wa mechi za Kombe la Mabara. Yanaitwa mavuvuzela. Ninahitaji moja.

Kuanzia sekunde za mwanzo za pambano la kwanza kabisa la Kombe la Mabara ambalo nililiangalia mwaka huu, New Zealand dhidi ya Hispania, Nilifikiri, “ni kelele gani ile?” na haraka nikaichuja. Na kwa njia sawa na hiyo, wakati nilipoishi Rosslyn, chini ya njia za ndege zilizokuwa zikiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Taifa, kelele za ndege nilinibugushi kwa kiasi cha wiki tu. Baada ya hapo sikuzisikia tena.
Yeyote ambaye amewahi kuhudhuria mechi anajua kwamba hilo huwa tukio la kujua mambo mengi tofauti. Kuna mchezo wenyewe, lakini kuna nyimbo, Mishumaa ya Kirumi, mabomu ya moshi, ngoma, honi. Enhhee, na hata mashabiki walevi vile vile.

Baadhi ya wasomaji wake wanapinga. Mmoja wao anachukia “dubwana lile” kwa sababu linaharibu mandhari ya mchezo:

Mimi ni mmoja wa wanaolichukia, siwezi kumuelewa yeyote ambaye anafurahia kuangalia soka kwenye televisheni ambaye anayapenda (mavuvuzela). Nayachukia madubwana haya. Lakini si kwa sababu yana kelele na yanakera. Ni mambo mengi – naam, watu wengi – wana kelele na wanaudhi, na hata (hasa) kwenye mapambano ya soka. Si kwa sababu wana kele na wanaudhi. Ni kwa sababu wanaharibu kabisa mandhari inayoendeana na pambano. Wanaiharibu.

Msomaji mwingine anasema, “huu ni wehu”:

*U*naweza kuwa na uwezo wa kuisukuma nyuma ya akili yako, lakini kwa wengi wetu, huu ni wehu. Sauti yake *si* ya “kimandhari”, *siyo* sehemu ndogo ya utazamaji, na haezi kukubalika.

Setumo anaandika kuhusu vuvuzela na kutokuvumiliana:

Kuweka kumbukumbu sawa, hatupulizi vuvuzela kwa sababu sisi ni Waafrika . Tunapuliza mavuvuzela kwa sababu tunapata mtawanyiko sawia wa homoni za adrenalini kutokana kelele zenye ubunifu zinazotoa. Vilevile, tunapata msisimuko wa adrenalini kwa sababu sisi ni binadamu. Siyo kwa sababu sisi ni Waafrika!
Na kwa vile hivi sasa tumeachana na imani potofu zinazotokana na ubaguzi wa rangi, inaweza kuwa rahisi kuisafisha kelele hii. Hatimaye, tunaweza kukubaliana kwamba hili ni suala la kupenda, kutokupenda na kutokuvumiliana.

Mmoja wa wasomaji wa Setumo anatoa hoja kwamba hili (vuvuzela) si jambo la Kiafrika:

Kwa hiyo Vuvu ni jambo la Kiafrika?? Kushindwa kwa FIFA 2010 si jambo la Kiafrika…ni suala la kimataifa. Ukweli ni kwamba Afrika Kusini inaandaa tu mashindano haya, na inajitahidi sana kupata wageni wa kimataifa kuja Afrika Kusini mwaka ujao. Kwa hiyo, kuweni na uelewa mdogo kwamba wale wasio Waafrika wanaioona kelele ya vuvuzela kuwa inakera kupita kiasi. Sidhani kuwa nchi nyingi zisizo za Kiafrika zingependa kuwa na ‘Uafrika’ukizingatia mambo kama vurugu, mauaji & utawala mbaya uliopo katika bara hili taabani.

Msomaji mwingine anaipenda sauti ya vuvuzela kiasi kwamba angeweza kununua sauti-mwito wa simu yake!:

@mcOlly – Kama mwenyeji wa Texas, ningependa kununua sauti-mwito hiyo ya simu.
Makelele haya dhidi ya vuvuzela ni ya kipuuzi. Kama haivutii kwenye televisheni, basi warusha matangazo washushe sauti za vipaza sauti vilivyoko uwanjani. Nimeijua vuvuzela kwa kuangalia Kombe la Mabara, na hiyo inanifanya nitamani kwenda kutazama Kombe la Dunia zaidi kuliko ilivyokuwa.

Shine2010 anadhani mavuvuzela yataifundisha dunia heshima na uvumulivu:

…Labda kukutana na maelfu machache ya mavuvuzela yatailazimisha dunia, na soka, kutekeleza kwa hakika baadhi ya fikra za kimaadili –uvumilivu, heshima n.k –ambazo inazihubiri kila wakati.

Robyn amekuwa ‘mlevi’ wa vuvuzela:

Kwa mara ya kwanza nilijaribu kulipuliza vuvuzela wiki mbili zilozopita, mwanzoni mwa Kombe la Mabara ambalo lilifanyika Afrika Kusini kabla ya Kombe la Dunia la mwaka ujao. Nilishindwa vibaya. Nilipuliza na kupuliza, hakuna kilichotokea, vijisauti fulani vidogo tu vilivyotoka. Lakini kwenye mechi kati ya Brazili na Italia, Niliupata ujanja wa vuvuzela na nikaungana haraka na umati katika mlio wa nota moja. Baaaah! Baaaah! Baaaah!
Ni sauti inayoudhi na kukera kiasi kwamba inabidi kutumia ule usemi “kama huwezi kuwashinda, ungana nao.” Kutokulipuliza vuvuzela katika mechi za za soka Afrika Kusini si tu kwamba inakufanya ujisikie kutengwa bali pia inakufanya uichukie kelele ambayo kila mmoja anaipiga.

Mwanablogu I Luv SA anacho kipande cha ushauri kwa wale wanaoichukia vuvuzela, “vumilieni”:
Mie, ninawaambia FIFA, mlinunua maneno matamu ya kuandaa mashindano nchini Afrika kusini, inawabidi mle chakula chote ambacho kinajumuisha kiungo kikuu, vuvuzela. Ni sawa na kuwaambia mashabiki wa uingereza kuizima kelele wanayoiita uimbaji. Vumilieni.

“Wakosoaji wanasema yana kelele sana. Sasa iweje,?” anaandika Ash kwenye blogu ya Wapenzi wa soka Afrika Kusini:

Hilo ndilo lengo la mavuvuzela. Lipo pale ili kutengeneza mandhari yenye kelele. Hii ni Afrika na tunajulikana kwa kucheza na kuimba na kwa kawaida kwa kutengeneza mandhari nzuri katika mechi zetu za mpira wa miguu.
Ni sehemu ya mazoea ya aina yake Afrika Kusini na nina hakika kama wageni wetu watahudhuria michezo hii na kushuhudia hali hii ya hewa (iliyojaa kelele ya mavuvuzela) basi watayapenda.

Kwangu, kuwaambia mashabiki wa nyumbani kuyaacha mavuvuzela yao nyumbani itakuwa kama kuwaomba wapenzi wa Liverpool kuacha kuimba “Katu Hutotembea Peke yako”, au kuwaambia mashabiki wa Brazili kuacha kusakata Samba kwenye mechi zao.

“Nini kilichovikumba kucheza na kuimba na mavazi ya sare?.” Msomaji mmoja anauliza na kuongeza, “usiruhusu mchango wako kwa dunia uwe ni ule ambao unaudhi!”:

Kama huo ndio utamaduni pekee ambao Afrika Kusini inao, basi hali n mbaya sana. Ni nini kilichovifika kucheza na kuimba na uvaaji wa sare? Mambo hayo yanafanya kazi vyema kwenye nchi nyingine Usiruhusu mchango wako kwa dunia uwe ni ule ambao unaudhi! Ni suala la ukarimu pia. Kutupigia kelele masikioni ni ushenzi. Mimi ninazima sauti. Namsikitikia yeyote anayekwenda Afrika Kusini kuangalia michezo. Hawatakuwa na chaguo lolote kuhusu suala hili.

Msomaji mwingine analinganisha vuvuzela na kelele inayoudhi ya jeshi la nyuki linalozinghuka juu ya kichwa chako…”:

Mtazamo anaotoa mwanablogu wa kufananisha nyimbo za Liverpool na mandhari ya samba huko Brazil uko karibu na utaahira. Bila ya shaka ningewataka mashabiki wa Liverpool waache ikiwa wangekuwa wanapiga kelele kwa nota moja tu ya YWNWA kwenye masikio yangu kwa muda wa saa moja na nusu. Kuna tofauti kubwa kati ya kelele inayoudhi ya nyuki wanaozunguka juu ya kichwa chako na ile ya dansi ya samba.

Hautakuwa unatazama timu za nyumbani au wachezaji,” msomaji mwingine anajibu:

Ni kwa jinsi gani Afrika Kusini inaweza kuimbia dunia kuwa yupi ni mgeni wa mpira wa miguu? Mgeni wa nchi, ndiyo. Mgeni wa mpira wa miguu? Usinifanye nicheke. Hautakuwa mpira wa Afrika kusini mwaka ujao. Utakuwa mpira wa miguu wa dunia nchini Afrika kusini. Hutakuwa unaangalia timu za nyumbani au wachezaji.

Anders anatuambia kuwa wanaochukia vuvuzela ni wale watu ambao wanaangalia michezo kwenye televisheni:

Malalamiko juu ya vuvuzela yatoka kwa wale, kama huyu rafiki yangu, wanaoangalia mashindano kutokea ng’ambo. Kwenye viwanja, mashabiki wanayapenda. Ni moja ya yale mambo ambayo unayachukia mpaka pale utakapokuwa na uwezo wa kuyajaribu; fikiria tochi ya miale. Kwenye televisheni matarumbeta yanaingiliana na utangazaji, pamoja na mambo mengine, lakini uwanjani hali ya kelele ni sehemu ya mandhari. Bila ya shaka hayakwaruzi ukiwa nayo ana kwa ana kama vile ukiyasikia kwa kupitia setilaiti.

Vita halisi ya vuvuzela, tunaambiwa haiko kwenye Mtandao bali nchini Uholanzi:

Kuna tishio la vita ya mavuvuzela huko Uholanzi. Kampuni ya SoccerID iliarifu siku ya Jumatatu kuwa itaingiza Ulaya mapembe haya yaliyosababishwa utata huko Afrika Kusini. Ndani ya majuma matatu ama manne mavuvuzela ya awali yatauzwa Uswisi. Kampuni ya NoLimitation, inadai kuwa ina haki pekee ya kusambaza mavuvuzela hayo.

Kampuni ya NoLimitation BV ilipata haki pekee ya mavuvuzela na ya kutumia jina hilo kupitia kampuni ya Kijerumani ya Kehrberg GmbH, inayodai kuwa na haki katika nchi zote za Umoja wa Ulaya. Kwa mujibu wa NoLimitation, hii ina maana kwamba wao ndio kampuni pekee nchini Uholanzi yenye haki ya kuuza tarumbeta hizi zenye vijipembe vitatu kwa jina la vuvuzela.

Chris wa blogu ya World Cup anaafiki kwamba vuvuzela “ina asili ya Afrika kusini” bali…

Tatizo ni kuwa, ina asili ya maudhi. Kama uliangalia japo sekunde 30 za Kombe la Mabara, uliweza kusikia ile kelele iwayo yote – na inawezekana kuwa matarumbeta yale yalikuwa ndiyo sababu iliyokufanya utazame kwa sekunde 30 tu.
Ni kelele moja endelevu kwa dakika 90. mpaka inafikia unaanza kujiuliza ni muda gani ambapo filamu hii ya kutisha ya dalaja la B itakapovunjika mbele ya macho yako. Binafsi nimeanza kuangalia mapambano hayo huku nimezima sauti –mchanganyiko wa timu ya utangazaji wa ESPN na vuvuzela vina uwezo wa kutumika kama sindano m’badala ya sumu au kitu kama hicho.

Phobian anashauri kwamba mavuvuzela yaruhusiwe tu Afrika Kusini inapocheza:

Kombe la Dunia ni la kila mmoja, si kwa wapuliza mavuvuzela peke yao. Labda yaruhusiwe tu pale Afrika Kusini inapocheza. Timu nyingine zinapocheza ziwe na sauti ya kuamua ikiwa wako tayari mavuvuzela yatumiwe ama yasitumiwe kwenye mechi zao.

SA Sucks anayapeleka mbali zaidi mabishano ya vuvuzela kwenye uwanja mwingine kabisa akitoa hoja kwamba mbali na uwezekano wa kuharibu masikio ya mtu, chombo hiki kinaweza kusambaza VVU/UKIMWI!

SA Sucks anaandika, “Ni wazi, Sipho hulisafisha vuvuzela kwa kulipekecha kila upande, huku akisambaza mate yenye virusi vya UKIMWI/TB (& na Mungu anajua ni magonjwa gani mengine) kwa watu wengine walio nyuma, mbele na pembeni yake.”:

Madaktari wataalamu wanaonya kwamba kelele za vuvuzela zinaweza kuharibu kabisa uwezo wa mtu kusikia, lakini hiyo haijazingatia hatari ya kuambukiza UKIMWI ya hili dude.
Tangu mechi za Kombe la Mabara, watazamaji walilipuliwa kutokea pande zote za uwanja na kelele zenye-kutikisa dunia za vuvuzela.Zaidi ya madhara ya kiafya ya masikio na maumivu ya kichwa, bidhaa nyingine itokanayo na upulizaji wa kifaa hiki ni mkusanyiko mkubwa wa mate. Ni wazi, Sipho hulisafisha vuvuzela kwa kulipekecha kila upande, huku akisambaza mate yenye virusi vya UKIMWI/TB (& na Mungu anajua ni magonjwa gani mengine) kwa watu wengine walio nyuma, mbele na pembeni yake.

Vuvuzela ni alama ya kila jambo lililoharibika katika “Afrika chini ya jangwa la Sahara the “Sahara Sub Saharan Africoon”:

Binafsi, ninalipenda (vuvuzela)! Kama kuna chochote kinaweza kuliangusha Kombe la Dunia la 2010, na kuwa ushahidi wa kila kisichofaa katika Afrika Nyeusi (Kusini mwa Jangwa la Sahara), yatakuwa haya mavuvuzela. Hebu fikiri namna uchafu unaokinaisha, ufukara uliokithiri, tabia za fujo za kinyani nyani na kele zilizokithiri zinazoletwa na hili dude; yote yatasafirishwa mpaka kwenye nyumba milioni 500 za Wazungu wa magharibi, huku dunia nzima ikishuhudia.

SA Sucks anawaonya wahudhuriaji wa Kombe la Dunia kujiandaa kwa “ubatizo wa moto” wa historia ya mwanadamu.” Mwanablogu huyu alishuhudia mwenyewe “masaa matatu ya kuzimu hapa hapa duniani”:

Jumapili nilijikuta kwenye masaa matatu ya kuzimu hapa hapa duniani. Nikaapa, pale pale, baada ya jioni ile ya kwanza (na ya pekee) ya kujionea mwenyewe soka la Afrika Kusini linavyokuwa kwamba, sitajiruhusu kujikuta mahala pale tena. Yapo mengi yaliyonikwaza na kuniudhi jioni ile, lakini hakuna kililonikera kama Vuvuzela.

“Kama FIFA wangeyapiga marufuku mavuvuzela basi na waifute sera ya mzunguko wa Kombe la Dunia kuyaandaa mshindano hayo Ulaya kila mwaka katika muda ambao unawafaa watu wa Ulaya na hali ya hewa ya Kiulaya katika viwanja,” anaandika Visual Guidance:

Ni lazima kiwepo kitu cha kulalamikia. Hakuna malalamiko kutoka kwa watu waliopo kwenye viwanja. Wanaipenda vuvuzela. Tatizo ni wazembe wanaoketi kwenye sofa maelfu ya maili mbali na viwanja, wanaojilaza kivivu vivu mbele ya televisheni zao na kulalamika kuwa kelele (za mavuvuzela) zinawapa maumivu ya kichwa. Boo hoo. Nijibuni –hivi matarumbeta yanakera zaidi ya Wana-Ultra na vipaza-sauti vyao katika viwanja vyao vya nyumbani kwenye ghuba yote Ultra au bendi ya Uingereza ikipiga wimbo wa ‘Great Escape’ pale Wembley?
Mashindano haya yanafanyikia Afrika. Hivi ndivyo wanavyofanya kwenye mechi za mpira nchini kwao, ndio utamaduni wao wa mpira.
Kama FIFA watayapiga marufuku mavuvuzela basi na waifute sera ya mzunguko wa Kombe la Dunia kuyaandaa mshindano hayo Ulaya kila mwaka katika muda ambao unawafaa watu wa Ulaya na hali ya hewa ya Kiulaya katika viwanja.

Garreth anaziona kelele za vuvuzela zinakera na mbaya lakini anafikiri kwamba jamii ya mpira duniani inahitaji kufahamu tamaduni mpya za mpira:

Hata kama sauti ni mbaya napelekea kukubaliana na SAFA (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika Kusini) katika hili. Pamoja na kwamba Kombe la Dunia linahusu mpira, vile vile kombe hilo linahusu jamii ya mpira wa dunia na kuzijua tamaduni mpya za mpira. Kama ninaanza kuonekana kama mtu wa siasa-za-ruksa, samahani sana, lakini hivyo ndivyo ninavyooona.

Sauti ya vuvuzela inaudhi na ndiyo maana kuta za Yeriko zilianguka!:

Sauti hii inaudhi! Ndio maana kuta za Yericho zilianguka! Watu wa Yeriko walijiangushia kuta wenyewe ili kuzikimbia zile kelele! Kifo kikawa chaguo lao sawia. Sasa, vivyo hivyo kwa mashabiki wa Afrika Kusini, WOTE NI MAPAFU! Je. hawajagundua kelele wanazosababisha? Hakuna atakayenunua tiketi ili eti jamaa ampigie kelele za vuvuzela mechi nzima!

Mwanablogu wa Cape Town Daily Photo hafikiri kama sauti hiyo ilikuwa ni mbaya kiasi hicho:

Sijawahi kuwa shabiki wa mavuvuzela (Tarumbeta la plastiki ambalo mashabiki wa Afrika Kusini hupuliza wakati wa mechi za mpira wa miguu) , lakini nikiwa mkweli, haikuwa mbaya sana. Haikuwa na sauti kubwa sana na ni lazima niseme mavuvuzela yaliongeza utamu wa mechi kwa kiasi kikubwa. Ni sehemu ya utamaduni wa soka la Afrika Kusini na haitakuwa kawaida yasipokuwepo.


Unajiandaa kwa Kombe la Dunia 2010?
:

Nunua viziba masikio kutoka kwenye duka la muziki –utaweza kufurahia mandhari, hata kama patakuwa na vuvuzela linalopigwa pembeni ya sikio lako.

Kama wewe ni shabiki wa mavuvuzela, unaweza kutembelea tovuti ya Blow Me na uipulize vuvuzela.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.