Uganda: Mke wa Rais ateuliwa kwenye Baraza la Mawaziri

(Makala hii ilitafsiriwa kwanza siku ya Jumatano, Aprili 15, 2009)

Janet Museveni

Janet Museveni


Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mwezi Februari yanawapa wanablogu wa Uganda fursa ya kubashiri matokeo ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2011.

Moja ya uteuzi aliofanya Rais Yoweri Museveni ni ule wa kumteua mke wake, Janet, kuwa Waziri wa Nchi wa Karamoja. Eneo hili liko kaskazini-mashariki mwa Uganda na kwa miongo mingi limegubikwa na migogoro na umaskini uliokithiri.

Wakati ambapo baadhi ya wanablogu wanajenga hoja kwamba uteuzi huo wa ngazi ya juu utasaidia sana kufanya eneo linalohusika kutazamwa kwa karibu, wengine wanaonyesha wasiwasi. Ariaka anaeleza:

Kwa mtazamo wa haraka, Mheshimiwa Rais Yoweri hatimaye amefanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri, jambo ambalo limekuwa kwenye minong'ono kwa zaidi ya miezi sita sasa. Ni ama kwa hakika ni mabadiliko ya aina yake. Tumeshuhudia Mke wa Rais, ambaye pia ni Mbunge wa eneo la Ruhama katika Jimbo la Ntungamo, akiteuliwa kuwa waziri wa Karamoja. Tumeshuhudia Syda Bumba akihamishwa kutoka Wizara ya Kazi kwenda kwenye Wizara nyeti ya Fedha. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Uganda kwamba Mke wa Rais anakuwa waziri, hata kama yeye ni waziri wa wizara ndogo tu. Pia ni mara ya kwanza kwamba mwanamke anateuliwa kuwa Waziri wa Fedha.

Uteuzi wa aina hii si jambo rahisi. Bila shaka ni sehemu ya mbinu za mchezo wa chesi katika siasa, ambapo mcheza kete anatupia jicho lake katika namna ya kupata ushindi.

Daniel Kalinaki, ambaye mara nyingi huandika makala kwenye blogu kuhusu siasa na ambaye aliandika tahariri juu ya uteuzi huo kwenye gazeti linalochapishwa nchini Uganda la Daily Monitor, anakubaliana kwa kusema:

Kwa kusema ukweli, hakuna tatizo kuhusu harakati za Janeti. Yeye ni raia wa Uganda na ana kila haki ya kuteuliwa kushika wadhifa wowote ambao anastahili kwa sifa. Hata hivyo, pale ambapo Rais aliyekaa madarakani kwa miaka 23 anaanza kujirundikia ndugu, marafiki, mashemeji karibu yake, basi si aghalabu kuwa anaweza kufananishwa na chifu wa ukoo fulani mwenye makusudi ya kuhakikisha utawala unabaki katika ukoo wake kuliko kuleta mageuzi ya kweli ya kidemokrasi.

Kwa upande wake, Antipop at Let There Be Me, yeye anaeleza katika namna yenye tashwishi akidurusu kuhusu ni kwa jinsi gani Museveni alifikia uamuzi huo. Anaeleza nadharia kadhaa, ambapo kwenye mojawapo anaeleza kwamba uteuzi huo ulikuwa ni zawadi iliyochelewa ya Siku ya Wapendanao, yaani Valentine:

kuhusu Siku ya Velentine:
…Siku iliyofuata wakati wa kustafstahi, na alipogundua kwamba tayari yupo kwenye msukosuko, huku akiwa hapendi kuwa katika hali ya kukabiliana na yeyote, alimweleza kwamba kutompa kwake zawaidi usiku uliotangulia ulikuwa na madhumuni ya kumpa zawadi nyingine ya kumshtukiza, na ambayo kwa hakika itafunika yote yaliyopita. Naye bibie alijipatia taarifa rasmi za zawadi hiyo kupitia gazeti alipendalo sana mnamo tarehe 17 mwezi Februari. Lakini pia aligundua kwamba ingempasa kusafiri umbali mrefu ili kujifungulia zawadi yake hiyo ya Siku ya Wapendanao, na kwa hiyo haikumshangaza. Kwake yeye zawadi ya nguo ya ndani ingemtosha kabisa.

Hata hivyo, si wanablogu wote wamepokea uteuzi huo kwa ukosoaji mkali. Phantom wa Even Steven anamalizia makala yake kwenye blogu ya Oscars kwa kuuliza:

Kwa habari nyingine, je, nini kibaya katika kumtuma Janet Museveni huko Karamoja?

Akiandika maoni kuhusu makala hayo, chanelno5 anamtetea Janet Museveni:

Hakuna ubaya na uteuzi huo. Ikiwa anataka kile ambacho wengine wanakikwepa, mwache achukue. Kusema ukweli huenda watu wa kule watanufaika na uteuzi wake huo.

Tumwijuke katika blogu ya Ugandan Insomiac anatafakari juu ya uteuzi huo, hata hivyo bado anautilia mashaka uteuzi:

Huenda kwa uteuzi huo, Rais Museveni anawatumia watu wa Karamoja salamu za mshikamano nao. Labda ana matumaini kwamba wale watu wanaounga mkono kila juhudi za Mke wa Rais basi watahamishia ‘usamaria’ wao katika miradi ya maendeleo ya Karamoja. Au labda picha inayomwonyesha Mama Janet akiwa amekumbatia mtoto mdogo wa jamii ya Karamojong itakuwa ni sehemu ya kujijengea sifa kwa upande wa Serikali ya Museveni.

Hata hivyo, bado siwezi kuondoa hisia zangu hizi mbaya…

Dennis Matanda, ambaye siku za karibuni alituma sehemu ya pili ya mfululizo wake wenye jina la “Rais afuatiaye wa Uganda”, anabashiri yafuatayo kuhusu yule atakayemrithi Museveni:

Ingawa Rais wa sasa hakufanya juhudi zozote za kumuandaa mrithi wa kiti chake kutoka katika chama chake cha National Resistance Movement, Vuguvugu, mkewe ambaye pia ni Mbunge, Janet Museveni, ambaye pia hivi karibuni ameteuliwa kuwa Waziri na mtoto wake, Luteni Kanali Muhoozi Kainerugaba, hawa wako mstari wa mbele.

Joe aliyeko Uganda anahitimisha mjadala huo kwa makala anayoiita “Utawala wa Kiukoo?” akieleza kwamba uteuzi wa Janet unaweza kuchukuliwa kama “ishara ya mambo yajayo.” Anaongeza kusema:

Kwa uzoefu wangu, baada ya kufanya kazi huko Karamoja kwa miezi miwili iliyopita, nimefurahi kusikia kuwa Waziri mwenye mizizi huko ngazi za juu atachukua nafasi kuongoza eneo hilo. Kwa kweli eneo hilo liko katika hitaji kubwa la kutazamwa kwa karibu.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.