Papa Nchini Kameruni (1): Utata wa Safisha-safisha Jijini Yaounde

Papa Benedikti wa XVI anazuru Kameruni kuanzia tarehe 17 mpaka tarehe 20 Machi 2009. Ziara hii imepelekea serikali kuchukua hatua kali za usafi kama anavyoelezwa katika blogu ya Griet,Thorsten, Jara and Lisa:

1. Maduka yote madogo, nyumba, vibanda vya wachuuzi ambavyo havina sura nzuri vianbomolewa na makatapila makubwa. Malori hayo ya katapila yanafika, na kutazama kibanda/nyumba/au chochote ambacho dereva haridhishwi nacho, halafu anabomoa pamoja na vyote vilivyomo. Hii ilianza kama wiki moja iliyopita katikati ya mji. Ghafla jiji halikuwa na wachuuzi wa mitaani tena, maduka yote yaliyoko posta yalitoweka n.k. Hivi sasa (operesheni hiyo) imeenea mpaka uwanja wa ndege.
2. Barabara inayoelekea uwanja wa ndege ina taa mpya za barabarani. Lakini ni katika njia hiyo TU kutokea uwanja wa ndege mpaka katikati ya jiji.
3. Jumanne (kwa hakika, na siku nyingine zitathibitishwa) baranbara kati ya uwanja wa ndege na katikati ya jiji zitafungwa. Angalia: Papa atawasili wakati wa jioni, lakini barabara zitafungwa kuanzia ALFAJIRI. Hivyo hakuna atakayeweza kwenda au kurudi kutoka kazini, shule n.k.

Makala hii kadhalika inaunganisha blogu nyingine ya familia ya mfanyakazi kutoka nje Sander Elke en Milan ambayo ina picha ya uharibifu wa maduka yaliyoko kandokando ya barabara kwenye mitaa ya Yaounde.

Bomoabomoa hii imezua mjadala katika blogu za wafanyakazi wawili kutoka nje walioko Kameruni. Blogu ya Συγκακοπαθησον inayoandikwa na mmisionari aliyeko Kameruni ilichapisha mabadiliko yatakayotokana na ujio wa Papa jijini Yaounde.

Je nina mtazamo upi kuhusu suala hili? Ni jambo zuri kwamba jiji linapata sura mpya – (safisha-safisha) inalifanya jiji lionekane zuri zaidi, na mataa ya barabarani yamerahisisha kuendesha magari usiku kadhalika kupata usafiri wa teksi kuwa rahisi na salama – lakini ni masikitiko kwamba safisha-safisha hii inamaanisha uharibifu wa namna ya watu wanavyoishi. Kwa bahati mbaya, hawa watu hawazifahamu “taratibu”, wengine kwa kupenda, na hivi sasa wanakumbana na matokeo. Jambo la kusikitisha ni kuwa serikali ilikuwa imeridhika na kuachia mambo yaendelee kuwa yalivyo (pengine kwa miaka 10 au zaidi) mpaka jambo kubwa lilipotokea, kama vile ujio wa Papa. Kama wangebomoa majengo yale pale tu yalipotojitokeza, pasingekuwa na uharibifu wa njia za kuishi za watu. Lakini hata hivyo, nadhani sheria ni sheria hata kama haitekelezwi.

Mtazamo huu haujapokelewa vizuri na mfanyakazi wa kujitolea wa VSO aliyezaliwa Uingereza ambaye anablogu katika blogu ya Our Man in Cameroon. Majibu yake katika makala iliyoitwa Impossible Missionary yalikuwa ni mepesi:

Vibanda vya biashara vya mitaani ni njia ya maisha hapa. Vipo kila sehemu. Ni rahisi kusema kuwa vipo kinyume ya sheria lakini vinaweza kuwa ni majengo madhubuti. La zaidi, kama vipo kinyume cha sheria nadhani vimeruhusiwa kuwepo kwa sababu kuna mtu, mahali fulani ambaye kila mara anachukua faranga elfu kadhaa kama rushwa.
Watu wanahangaika hapa. Unaweza kusema kuwa majengo haya hayazalishi sana katika nchi kama hii ambapo juhudi na ujasiriamali viko chini mno… naam, ni njia iliyoje ya kuwatuza. Ninakuomba, kama unakubaliana na niliyoyaandika na kama uafikiri kuwa mtazamo wa mmisionari ni wa kijinga, tafadhali acha maoni. Siyo hapa chini, bali katika blogu ya mmisionari.

Hata hivyo, wasomaji waliendelea kuandika maoni kuhusu habari hii kwenye blogu ya Our Man in Cameroon. Maoni yalifikia kiwango ambapo Karis, mke wa mmisionari aliingilia kati ili kumtetea mume wake:

Wow! Sikujua kwamba mume wangu anaweza kusababisha mtafaruku wa namna hii. Nadhani kuwa wakati mwingine huwa tunafikiri kuwa ni watu wanaotufahamu pekee ambao husoma blogu zetu na watu hao hufahamu jinsi ya kuchukulia yale tunayoyaandika badala ya kuyachambua mstari kwa mstari pasina kutufahamu hata chembe. Trav, nakushukuru kwa maoni yako mazuri. Dad A, nashukuru kwa utani wako. Kila mara huwa unanijaza tabasamu usoni kwangu. Ninatamani kuwa nyie wote mliotoa maoni hapa na kwenye blogu ya mume wangu mngekuwa mnamfahamu mume wangu – msingekuwa wakali namna hii wakati mkichambua sentensi zake.
Mimi na yeye tumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu ni jinsi gani njia za maisha za watu zimepokonywa na yote hayo kwa sababu tu ya ziara ya Papa kwa siku chache. Tulipokuwa mjini jumatatu na kuona vitu vinavyotupwa kwenye magari ya mizigo, nilichefuka mpaka tumboni. Zaidi ya mara moja tulijisemea, “je watu hawa watakula wapi usiku wa leo? Na siku inayofuata na inayofuata?” Tuliendelea zaidi ya hapo kwenye…
Na hivi leo, nilimuona akiwasaidia watu kuhamisha cherehani, meza na mapakacha ya makabrasha yao kuyapeleka mbali zaidi hapa barabarani kwetu wakati serikali ilipokuwa inakuja na magari ya kubomoa. Hapana, hilo halikusisitizwa katika makala hii ili kuonyesha mazungumzo na vitendo vyetu, lakini wow… hilo halimaanishi kuwa mume wangu hana hisia na watu wa hapa! Pengine ninaweza kumshawishi aandike makala nyingine, lakini sina hakika kwa sababu inaweza ikawa ni bora tu kuacha mambo kama yalivyo badala ya kufanya yachambuliwe tena. Naona bora nikome. Mke kumuunga mkono mume wake hakutabadilisha akili za watu.

Majibizano hayo hayakuishia hapo. Ziara hii ya Papa ina makeke mengi kwenye ulimwengu wa blogu!

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.