Karibeani Ya Kifaransa: Tamasha la Kanivali 2009 Lazinduliwa

Kanivali ni utamaduni, sehemu ya uhai wa kila Muhindi wa Magharibi na bila kuwaacha wale wa Karibeani ya Kifaransa.

Ufuatao ni muhtasari wa blogu kutoka Martiniki, Gayana ya Kifaransa, Haiti na Guadalupe, ambao unaelezea mambo yanavyokuwa kwenye Kanivali.

Katika blogu ya brevesdeguyane, tunajifunza jinsi Kanivali inavyozinduliwa huko Gayana ya Kifaransa na tunazivumbua picha za vielelezo vya utamaduni wa Kiguyana ya Kifaransa wa “Touloulous”. Neno hilo kwa asili yake lina maana ya kaa wadogo wenye rangi ya kuvutia, ambao hukimbia upesi na kujificha chini ya ardhi pindi wanapohisi kutishwa. Je kuna uhusiano upi baina yao na wanawake wa kuvutia waliojibadilisha? Lilie Belle katika blogu ya MaGuyane anaielezea Kanivali inavyokuwa katika Gayana ya Kifaransa na anatoa jibu la swali hilo [Fr]:

“Touloulous” hupiga gwaride mbele ya wanaume, ambao wamefika kwenye sherehe peke yao au katika makundi ya marafiki. Ina maana kwamba wanaume huwa hawajui ni jinsi gani wake zao walivyojibadilisha. Hivyo, wanawake hao wa Toulousehuweza kuwachabanga waume zao au hata wakubwa wa kikazi !! Toulouse huwaalika wanaume kucheza na si kinyume.
[…] Kwa miaka michache sasa kumekuwa na mtindo mpya: Tolos. Wanaume, waliojibadilisha, huwaomba wanawake kucheza.

Maneno ya Darlie ni mwangwi wa maneno yaliyo kwenye blogu ya kigayana ya Kifaransa ya Lillie Belle's na Eric Leon 97320, wakati anapoeleza kuwa uzinduzi wa sherehe za kanivali ni tukio linalosubiriwa kwa hamu [Fr]:

Mabibi na Mabwana, Kanivali ya Haiti imezinduliwa rasmi. Utakuwa ni mwezi mmoja na nusu wa kushereheka.

Kwa maneno machache, Darlie anafafanua kuhusu Kanivali (ya Haiti) [Fr]:

Rangi, mavazi, vinyago, viongozi wa halaiki, ngoma, vichekesho, Charles Oscar, magari ya maonyesho, maonyesho… mabibi na mabwana, tarajieni orodha ya vyakula mbalimbali katika mji mkuu wa Haiti na mjini Jacmel, kuanzia jumapili hii mpaka mapambazuko ya siku ya Jumatano ya Majivu (ambayo ni siku muhimu kwenye kalenda ya Kikatoliki).

Wakati anapozungumzia mchanganyiko, Darlie anababatiza kiini cha Kanivali katika Karibeani ya Kifaransa: vielelezo vya vyanzo mbalimbali vya utamaduni huo. Siku hizi huko Guadalupe, Gayana ya Kifaransa na Martinique, Kanivali husherehekewa kila jumapili kwa magwaride maarufu yaliyopangwa vizuri ya bendi za watu waliojibadilisha na kuvaa vinyago. Bendi nyingine zinafuata utamaduni wa kanivali za Ulaya ambako watu hujipamba kwa mavazi yanayong’ara ya manyoya na shanga, na kama inavyokuwa katika Kanivali nyingi za Kilatini, kama ile maarufu zaidi inayofanyika mjini Rio De Janeiro. Bendi hizi huingia kwenye mashindano ya kuchagua bendi nzuri zaidi, muziki mzuri, uchezaji mzuri na hatimaye kuchagua Malkia na Mfalme wa Kanivali. Tovuti hii ya “la Mairie de Fort-de-France” huko Martinique inaonyesha picha za uchaguzi huo unaojumuisha vizazi tofauti: Malkia mtoto, Malkia nusu, Malkia na Mama wa Malkia.

Bendi za mtindo mwingine zilianza kwanza nchini Guadalupe: hizi huitwa Vyama vya Kitamaduni, vyenye nia ya kuwapeleka watu wa Karibeani ya Kifaransakaribu na mizizi au asili yao ya Kiafrika. Wanaitangaza kanivali kwa kutumia tamaduni za mizimu yao, uhalisi na muziki wa kitamaduni zaidi unaotumia ngoma zilizotengenezwa nchini, kwa kutumia ngozi za mbuzi (mas a po). Hutangazwa kwa mijeledi na udi na hawapigi muziki kwa kufuata taratibu za ala, kadhalika huwa hawachezi ngoma zilizopangwa kisanifu mitaani. Chapa yao ni kuandamana kama vile kidini, katika hali ya kustaajabisha. Hizi ni picha za “Klela” (funguo), na bendi ya “mas a po” kutoka Guadalupe.

Bendi za mitindo hii miwili huwa mitaani kuanzia Jumapili ya Kuwasili Mamajusi mpaka Jumatano ya Majivu, ambapo Vaval, (kinyago cha Mfalme wa Kanivali) kinapochomwa moto kuashiria mwisho wa kanivali na mwanzo wa mwezi wa kutubu na swaumu (kwaresima). Katika Guadalupe, hata hivyo, watu hurejea tena siku 15 baadaye kwa ajili ya gwaride jingine, wakati wa “Jeudi de la Mi-Carême” siku 15 baadaye aktikati ya kipindi cha mfungo. Rangi za gwaride hili ni nyekundu na nyeusi ili kuonyesha kwamba Vaval amefariki lakini ataishi tena mwaka ujao.

Picha zote katika makala hii ni sehemu ya kanivali ya 2008 na Dimanche Gras, kwa hisani ya mwandishi. Unaweza kuona seti nzima kwenye Facebook, hapa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.