Palestina: Mawasiliano na Gaza

Katika mazingira ya kawaida bila kiwango kikubwa cha wanaojua kusoma, usambaaji wa intaneti husimama kati ya asilimia 13 mpka asilimia 15 (Gaza na Ukingo wa Magharibi kwa pamoja). Kutokana na mashambulizi yanayoendelea huko huko Gaza, uwezo wa kutumia intaneti umepungua sana. Japokuwa kuna idadi ndogo ya wanablogu wanaoandika moja kwa moja kutokea Gaza, wakazi wengine wengi wanatumia ujumbe wa maandishi wa simu za mkononi pamoja na simu nje ya nchi katika matumaini kwamba ushahidi wao utapata sehemu ya kuelezwa.

Mohammad wa KABOBfest, maybe anaishi Ukingo wa Magharibi, amekuwa akiripoti kuhusu Gaza kwa siku kadhaa sasa. Katika ujumbe wake wa kwanza wa tarehe 29 Desemba, anatuambia:

Nilitaka kuwapigia simu wajomba zangu ili kuwajulia hali wao na familia zao, sikuweza kwa siku nzima. Nilikuwa nahofu sana kujua hali waliyokuwamo. Lakini nilipopiga simu,nilipata mshangao mzuri.

Mjomba wangu Jasim aliniambia mambo yalikuwa mazuri zaidi leo, japo kulikuwa na hofu lakini watu wameanza kupata ahueni. Tumeweza kuhimili mshtuko wa shambulio la kwanza, alisema, na hiyo imetusaidia kustahimili hii leo. Alisema anga imekuwa kimya kwa muda wa saa moja na nusu hivi huko Khan Younis, lakini meli za kivita zilikuwa zinaendelea kushambulia sehemu za mwambao.Sauti yake likuwa imara, kama vile ilivyokuwa wakati wowote kabla ya mauaji kuanza, na aliniambia nisihofu sana. Hawakuwa na umeme kama kawaida, nikamueleza juu ya maandamano na ghasia zinazotokea Ukingo wa Magharibi na mvua za kuungwa mkono zinazomwagika duniani kote. Nilimwambia kuwa hakuna aliyewasahau, na aliniasa niendelee kuwaswalia. Wanawe wadogo walikuwa bado wamelala, lakini binti zake, Haneen na Yaqeen walikuwa bado wapo macho. Nilimuomba awaambie kwamba bado wako mioyoni mwetu.

Halafu nikampigia simu mjomba wangu Mahmood. Jana aliniambia kuwa anasubiri kifo. Waisraeli walimpigia simu na kumwambia kuwa wangeipiga mabomu nyumba yake katika dakika chache. Alituacha sote tukiogopa, lakini leo alituambia kuwa kumbe Waisraeli waliwapigia simu za namna hiyo kwenye makumi ya maelfu ya nyumba. Ni mbinu ya utesi na ukatili, iliyoundwa ili kuwagaidi makumi ya mjaelfu ya raia wakiwa majumbani mwao.

Lakini matumaini haya mara yalitoweka. Mnamo tarehe 3, Januari, Mohammed aliripoti tena:

Nimeweza kumfikia mjomba wangu Mahmood kwa mara nyingine tena mjini Gaza. Wakati wote tuliokuwa tukiongea kwenye simu, mlipukjo ulisikika kila baada sekunde kama 20 hivi. Katika baridi kali ya usiku, vitisho vinawafunika watu wa Gaza, na hasa ndani ya jiji la Gaza. Milio ya bunduki na milipuko inaiwamba mandhari ya anga jeusi yenye miungurumo ya ndege za kijeshi zisizoonekana na pia helikopta za kijeshi. Hakuna anayejua ni nini kinachopigwa. Mjomba wangu nananiambia kumekuwa na milipuko katika sehemu zote zinazowazunguka, Karibu na mbali, kutoka kila upande, hata idhaa ya redio yao, ambayo imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kuwaeleza ni nini kinachoendelea, haiwezi tena kueleza kwa hakika ni nini kinacholengwa na kupigwa. Hakuna anyejua kama mashumbulizi hayo ya anga yazilenga nyumba za watu, majengo, miskiti au sehemu ambazo zilishashambuliwa awali, kwa hiyo hakuna nayejua kama mbinu zimebadilika au la. Katika vita, kwa raia kama vile ilivyo kwa wanajeshi, hakuna linalotisha zaidi kama kutokujua.

Katika ujumbe wake wa tatu, anasimulia kwa undani mazungumzo ya simu na wanafamlia wake walioko Gaza, akilinganisha hali ilivyo kutokea jijini Gaza mpaka Khan Younis. Anaielezea simu moja mojawapo akiongea na mke wa mjomba wake:

Niliongea tena na Areej. Amepoa kwa kiasi Fulani, lakini alikuwa bado na hofu. Nilimuuliza kuhusu watoto. Akasema, mtoto, Yazeed, alikuwa amelala pembeni yake. Dina pia alikuwa amelala, na mama yao amewaambia Nada na Haya kwenda chumbani kwao ambako panaweza kuwa salama zaidi. Nilimuuliza ikiwa wapata joto ikiwa madirisha yao yako wazi wakati wote yakipitisha upepo, akaniambia wakati wakilala wanajifunika na na tabaka nyingi za mablanketi kadiri inavyowezekana, lakini wakati wa mchana na jioni baridi si kali sana. Nilmuuliza kuhusu Adham, mwanawe mwenye umri wa miaka 11. Aliniambia kuwa mwanawe amewasha mishumaa miwili na amesambaza wanasesere wake anajaribu kucheza, pamoja na baridi na hofu na makombora na vifo na athari. Alikuwa na vifaa vya kuchezea vya Lego, na magari pamoja na sanamu za wanajeshi. Sikutaka kumuuliza alikuwa anacheza mchezo gani na hao sanamu wanajeshi. Sikutaka kujua.

Mwandishi wa Global Voices Ayesha Saldanha wa blogu ya Bint Battuta wa Bahrain pia amekuwa akipandisha makala kutoka kwa marafiki zake walioko Gaza. Ujumbe wa leo wa SMS kutoka kwa rafiki yake Hasan una mstari wa mwisho unaoleza wazi:

12.30 asubuhi: Si simu ya ndani wala ya umeme vinavyofanya kazi. Ndio kwanza nimeamka na kuuona ujumbe wako wa simu ya mkononi. Nilisikia kelele kubwa za vifaru vikishambulia huko nje. Pamoja na helikoptas za kijeshi za Apache na drone. Wanaweza wakawa karibu hatujui.

2.20 asubuhi: “Bado havijafika karibu. Natumaini. Kama umeme ukiendelea hivi kama gaza hatutaweza. Najaribu kumpigia simu au kumuandikia ujumbe wa simu ya mkononi dada yangu bila mafanikio”

7.30 mchana: “mke wangu kaniuliza kwa nini nakunja sura. Nipe chochote kitakachoweza kunitia matumaini na nitatabasamu nilimjibu. Leo orodha ya mahitaji imezidi sana. Dawa, chakula na vifaa vya usafi. Niliamua kwenda mjini japokuwa walikwisha shambulia soko moja mjini Gaza. Waliua watu 5 na kujeruhi kundi la watu. Nilipoingia tu sokoni ndege ya F-16 ikazipiga nyumba 2 karibu kabisa na soko. Kila mtu alifikiri kama nilivyofikiri mimi. Kama sio soko basi itakuwa Msikiti. Nikapatwa na kihoro. Nikanunua nusu tu ya mahitaji yetu na kuharakia nyumbani. Wakati niko njiani wakapiga nyumba nyingine karibu na nyumba yangu. Vifaru vilipiga sana jana usiku mapaka tukawa tunaogopa.

12.30 jioni: ” kama mambo yataendelea kuwa mabaya nitaitia kadi yangu ya simu kwenye simu ya mke wangu. Ndege za F-16 zinapiga hivi sasa. Na mlio wa gari ya wagonjwa ni mkubwa. Kila siku ni mbaya zaidi kuliko siku iliyopita”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.