Kongo: Utata Watawala Goma

Miezi miwili iliyopita mapigano yamezuka tena katika jimbo la mashariki la Kivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya kundi la upinzani linaloongozwa na Jenerali laurtent Nkunda na majeshi ya serikali, kinyume na makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwezi januari. Watu wapatao 250 000 wameteguliwa kutoka kwenye makazi yao tangu machafuko yalipolipuka tena mnamo mwezi wa Agosti, na kupelekea idadi ya watu waliopoteza makazi yao kufikia zaidi ya milioni 2 katika ukanda huo. Vikundi vya raia wenye hasira vimekuwa vikishambulia ofisi za Umoja wa Mataifa huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini, vikundi hivyo vimekasirikia Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuwalinda.

Fred R. akiandika katika Extra-Extra anaelezea mazingira ya nyuma ili kuweza kufahamu kwa nini umma umeghafirika:

… jukumu [la kuleta amani na usalama kwa kumaliza janga la majeshi ya kigeni na wanamgambo wa ndani] liliwaangukia majeshi yaliyojaa tahadhari, na yaliyoelemewa kikazi kupindukia ya Umoja wa mataifa pamoja na jeshi la Taifa lililojaa rushwa na uzembe ambalo liliundwa na mjeshi pinzani yaliyokuwa yakipigana huko nyuma. Ndani ya nchi hii kubwa iliyogawanyika katika vitongoji visivyo rahisi kuvifikia, haingekuwa jambo rahisi kutatua matatizo yote ya rushwa, uzembe, ushindani wa kikabila pamoja na ushindani wa kutaka ukubwa. Lakini kipindi kilichofuata baada ya uchaguzi mkuu kilitoa mwanya wa fursa kwa serikali mpya kuunganisha nchi kwa visheni au malengo makuu yaliyo wazi (kwa msaada wa Umoja wa Mataifa) vikiungwa mkono na mkondo wa sheria. Walipoteza mwanya huo.

Mark Leon kwenye Toleo la Umoja wa Mataifa anatoa maoni kuhusu masononeko ya umma yanayoelekezwa kwa umoja wa Mataifa:

Wenyeji wanaweza kueleweka jinsi walivyokerwa kwani majeshi ya kulinda amani hawajafanya ipasavyo ili kusitisha mavamizi ya waasi. Maandamano nje ya boma la Umoja wa Mataifa yaligeuka kuwa ghasia mwanzoni mwa juma wakati wenyeji wa mji wa Goma waliporusha mawe kwenye boma hilo kutokana na kukata tamaa. Kwa bahati mbaya, majeshi ya kulinda amani hayawezi kuzuia mashabulizi hayo bila ya kuongezewa vikosi.

Wanahitaji msaada. Haraka.

Ujumbe wa Fred unatoa maelezo ya nyuma ya kina kuhusu hali ilivyo huko Kivu ya kaskazini. Michelle F. kwenye blogu ya Stop The Genocide anakokotoa picha ya majeshi yenye silaha aliyoiita “supu ya majeshi yenye silaha kwa herufi” katika Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Kongo kwa wale ambao hawajui ni nani wahusika wakuu kwenye mzozo huu:

- Jenerali Laurent Nkunda na chama chake cha Taifa kwa Ajili ya Kulinda Watu au Congres National pour la Defense du Peuple (CNDP) anadai kupigana kwa ajili ya kuwalinda Wananchi wa Kongo wa kabila la Watusi dhidi ya wageni wasioalikwa na wala kutakiwa nchini humo,

- Jeshi la Wanademokrasia kwa Ajili ya Ukombozi wa Rwanda, Forces Democratiques de Liberation du Rwanda (FDLR), au Interahamwe, waliondesha mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, amabo wameweka kambi huko mashariki ta Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada utawala wao wa vitisho nchini mwao. Majeshi ya FDLR hivi sasa yanajumuisha makuruta wengi kutoka Kongo, pamoja na watoto.

- Jeshi la Wananchi wa Kongo Forces Armées de la République Démocratique du Congo (FARDC), ambao huko nyuma walijulikana kama mamahiri wa kila jambo ambalo jeshi la wananchi halitakiwi kufanya, na

- Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUC, jeshi ambalo kama Michael alivyoliezea, hivi sasa linashambuliwa na wananchi waliokasirishwa na kutokuwa na uwezo kwa jeshi hilo kuwalinda raia. Ofisi ya Kimataifa ya Wakimbizi, Refugees international inaeleza kuwa MONUC wamo kati-ya-jiwe-na-pahala-pagumu nchini humo.

Siku nne zilizopita waasi wa CNDP waliteka kambi kubwa ya jeshi huko Rumangabo kadhalika makao makuu ya Mbuga za Taifa za Virunga zenye ukubwa wa Maili Mraba 3000 (Kilometa za mraba 7,800) ambazo ni makazi ya sokwe wa milimani wapatao 200 kati ya jumla ya sokwe 700 wa aina hiyo duniani. Waasi hao wamewahi kuitumia mbuga hiyo huko nyuma lakini walikuwa hawajawahi kuitumia kama makao yao makuu. Mkurugenzi wa mbuga hiyo, Emmanuel de Merode, anaandika kuhusu matukio ya Jumapili katika blogu rasmi ya ya Mbuga za Virunga:

Mapambano [..] yamezingira kabisa kituo cha mbuga na walinzi wa doria mbugani wamelazimika kukimbilia misituni ili kuokoa maisha yao. Waasi ndio wakazi pekee wa kituo cha mbuga cha Ramangabo hivi sasa. Hili halijawahi kutokea wakati wowote kabla.

Huu ni wakati mgumu. Tunahitajika kuwafikisha walinzi wetu wa doria mbugani wapatao 50 na zaidi mjinin Goma kwenye usalama, Kilometa zipatazo 45 kusini mwa Rumangabo. Barabara kuu imefungwa kutokana na mapambano hivyo wanatembea kwa miguu kukatiza misitu kusini mwa mbuga, kuelekea Kibumba, takriban kilometa 20 hivi zaidi,ambako tunatarajia kwenda kuwachukua kwa kutumia malori. Tunajaribu kuendelea kuwasiliana nao kwa simu lakini hawana nguvu za betri (mawe) ya kutosha kwenye simu zao.

Siku mbili baadaye, 12 katika wale askari wa doria waliokuwa wakikimbia katika misitu waliokolewa na kupelekwa Goma. . Innocent Mburanumwe alielezea jinsi alivyokuwa mchovu, mwenye kiu na njaa wakati timu iliyotokea Goma ilipowakuta na kuwaokoa:

Askari doria wa mbuga walianza safari Jumapili mnamo saa 3 asubuhi wakiwa kundi la watu 14 – kadhalika walikuwa na wanajeshi 4 ambao pia walikuwa wanwakimbia waasi. Walikatiza mbugani, wakitarajia kutokeshezea barabarani, lakini walisikia milio ya mabomu na na mizinga na hivyo iliwabidi kurudi tena msituni. Bila ya maji walianza kufyonza mawe ili kutuliza kiu, pia walijaribu kunyonya umande kutoka kwenye matope kwa kuweka kitambaa kati ya midomo yao na tope lenye nyevunyevu.

Jumatano, msemaji wa CNDP alitangaza kusitishwa kwa mapigano, japokuwa hali huko Goma iliendelea kuwa kutoeleweka. Kama ambavyo Kate Cronin-Furman kutoka blogu ya Wronging Rights anavyodokeza, “kila mmoja inaonekana kuwa anajiandaa na vita, pengine kwa vile Nkunda huko nyuma amewahi kuonyesha kutoelewa maana ya neno usitishwaji wa mapigano.”

Samantha Newport anaandika kuhusu utata uliopo kwenye blogu ya Mbuga za Taifa za Virunga:

Goma ni vurugu tupu. Nimeelezwa, kupitia simu mbalimbali na jumbe fupi za simu za viganjani, kwamba jeshi limeweka silaha chini huko Kibumba, malili 12 kaskazini ya Goma, na wanawakimbia waasi. Kwa maneno mengine wamekata tamaa kabisa.
[..]
Gavana wa Kivu ya Kaskazini pia ameukimbia mji.

Hivi sasa ni majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa pekee yaliyopo kuzuia majeshi ya Nkunda kuuteka mji wa Goma.

Kuna makisio mengi na ubashiri hivi sasa – na hofu.

Katika ujumbe mwingine kwenye blogu ya Mbuga za Taifa za Virunga, Emmanuel de Merode pia anaandika kuhusu utata unaotawala Goma:

Pengine utata ndiyo njia pekee ya kuielezea hali ilivyo. Kuna kutupiana risasi kwingi mjini, kukiwa na silaha kubwa mbali zaidi. Kila mtu anajificha nyumbani. Pia kumekuwepo na uporaji, haswa na baadhi ya watu wenye silaha wanaopora magari na pikipiki. Laurent nkunda ametoa tamko kwenye televisheni na redio akitangaza kusitishwa kwa mapigano, jambo la kutia moyo, kwa bahati mbaya hilo halijasababisha jioni yenye utulivu.

Tumefikwa na wimbi la uzushi pamoja na ule wa uvamizi wa jeshi la Rwanda, mamluki wa Kiangola wakija kutokea magharibi, karibu kila kitu, na hakuna moja lenye msaada.

Asubuhi hii Samantha anatoa habari mpya kuhusu hali ilivyo, pamoja na picha chache kwenye boma anamoishi:

Waasi wa CNDP – waasi wa Nkunda – wanaushikilia Kiwanja na Rutshuru na wamesimika utawala wao kwenye eneo hilo. Jeshi la taifa, polisi na wafanyakazi wa serikali wote wameondoka – kwa hiyo sehemu kubwa ya jimbo imo chini ya utawala wa CNDP hivi sasa.

Innocent alikuwa na usiku uliokosa heri. Nyumba ya jirani yake iliporwa na askari waliokuwa wakiukimbia mji. Kwa bahati nzuri Innocent, mkewe na watoto 5 wako salama na hawakuporwa.

Dawn Hurley, mfanyakazi wa kimataifa aishiye Goma anaandika katika blogu yake From Congo kuhusu ukosefu wa uhakika na hofu usiku unapoingia:

Usiku hapa unaweza kuwa ni jambo la kutisha. Mchana, maisha yanaonekana kuwezekana mjini Goma. Lakini usiku huingia majira ya 12.30 hapa na kuanzia hapo mpaka asubuhi kila mmoja na lwake. Watu wengi hawana magari, kwa hiyo hawawezi kwenda popote baada ya kuingia giza. Na siku hizi, haipendekezwi hata kuendesha gari wakati wa usiku. Watu wengi hawana umeme, kwa hiyo mara nyingi huketi na familia kwenye vibanda vyao, wakijiombea salama, wakisikiliza miwangwi ya risasi ikirindima mjini, huku wakisubiri nuru ya asubuhi. Hakuna simu ya dharura ya 911 ya kupiga kama una tatizo. Watu huwaita marafiki ambao wana kidogo cha kutoa, ghairi ya sauti iliyo upande wa pili wa simu.

Colette Braeckman, mwandishi wa habari wa Kibelgiji na mwandishi wa vitabu kadhaa vinavyohusu Afrika ya Kati, anaweka katika blogu yake [fr] maelezo ya Dunia Ruyenzi, mwanaharakati wa haki za binaadamu huko Goma:

Tulipitisha usiku mzima tukiwa tumejifungia, huku milio ya risasi ikizingira kote. Jeshi la Kongo lililaumiwa lakini nina hakika kwamba, kulikuwako pia wanajeshi wa Nkunda waliojipenyeza ili kuamsha hofu. Wengine wao pia walikuwa wakitafuta pesa na waliua watu watatu. Waliwatisha MONUC na kuwatupia risasi. Mbali na hilo uwanja wa ndege haujachukulia na ndege zinaweza kutua. Magereza yamefurika watu waliokamatwa na polisi na jeshi. Tunajaribu kutengeneza orodha ya wafungwa, na kuwapata wakiwa ndani ya mapango yao. Wanajeshi wa serikali hawajakimbia wote, baadhi bado wanapigana huko Rutshuru…

Katika habari mpya kutoka blogu ya Mbuga za Virunga, saa 4 usiku, Emmanuel anaandika:

Kuna kutupiana risasi kusikotabirika katika mitaa lakini kiasi pungufu ikilinganishwa na jana. Hali ile ya kutisha imeanza kupungua. Kesho, naibu katibu wa Masuala ya Afrika katika serikali ya Marekani anatarajiwa kuwasili Goma kusaidia majadiliano. Luis Michel, Kamishna wa Maendeleo ya Kimataifa wa Jumuiya ya Ulaya yupo jijini Kinshasa na waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Carol de Gujt, anatarajiwa kuwasili mjini Kigali. Na tuendelee kutumaini…

Wiki mbili zilizopita mwandishi wa habari Jina Moore, ambaye alikuwa Rwanda huko nyuma ambaye pia aliandika juu ya Kongo, ameandika katika blogu yake News From Central Africa:

Hatimaye nimefahamu lile jambo ambalo nimelisoma kwenye vitabu, ambapo waandishi wakongwe huliongelea kuhusu hisia ya kukata tamaa inayowapata wanapotaka kurejea kwenye maeneo yaliyoharibiwa kabisa ambayo waliwahi kuyaandika wakati mambo yalipochukua mkondo mbaya zaidi. Inamaanisha jambo jingine wakati unafahamu fika sehemu hiyo ikoje, na kuna jambo linalotafuna ndani yako, likikuita kurejea tena huko.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.