Sheria Mpya Uganda: Mashoga Sasa Kukabiliwa na Kifungo cha Maisha Jela

Protest against Uganda anti-gay legislation

Wanaharakati John Bosco, (mwenye pingu mkononi) na Bisi Alimi (mwenye bango) wakiwa na mavazi ya kifungwa wakiandamana jijini London kupinga sheria mpya ya kupinga ushoga nchini Uganda tarehe 10, Decemba, 2012. Picha kwa hisani ya Reporter#20299. Haki miliki ya Demotix.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesaini muswada unaopiga marufuku ushoga na kuufanya kuwa sheria tangu Januari 24, 2014. Sheria hiyo mpya itaadhibu vitendo vya ushoga kwa kifungo cha maisha jela katika baadhi ya masuala.

Bunge la Uganda kwa kishindo kabisa lilipitisha muswada huo mnamo Desemba 20, 2013. Sheria hiyo inatoa adhabu ya kifungo jela kwa yeyote ambaye hatatoa taarifa za kuwapo kwa raia anayefanya vitendo vya kishoga kwa mamlaka za kiserikali na vile vile sheria hiyo inatoa hukumu kwa mtu yeyote kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook na Twita kwa minajili ya kupigania haki za mashoga kitendo kinachotafsiriwa na sheria hiyo kuwa ni cha jinai na hukumu yake ni kifungo kisichozidi miaka saba jela.

Rais wa Marekani Barack Obama na viongozi wengine duniani walimuonya Rais Museveni kuwa sheria hiyo ni uvunjifu wa haki za binadamu.

Wanaharakati wa asasi ya Uganda inayotetea haki za mashoga na wasagaji (LGBT) wanasema kuwa sheria hiyo inaifanya Uganda kuwa sehemu hatari zaidi kwa mashoga duniani. Watu wengi wamejadili suala hili kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakiunga mkono hatua hiyo na wengine wakiipinga vikali.

Kiongozi wa Kundi la Watu Wenye Ujinsia Usiozoeleka na ambaye ni mwanaharakati wa haki za mashoga  Frank Mugisha alitwiti:

Akaunti ya Twita na ya Facebook ni kinyume cha sheria, faini ya sarafu 5,000 au kifungo jela hadi miaka mitano na kisichozidi miaka saba au vyote viwili kwa pamoja

Love1Another akaandika:

Marekani, sasa mnaweza kuishukia Uganda na kufanya chochote mnachotaka, muswada sasa umekuwa sheria

Wadda Mutebi alitoa maneno makali kwa wanaopinga mswada huo:

Nyie manaopiga kelele za kuutukuza ushoga, mkafie kuzimu. Mtandelea kuzungumzia haki zenu za kijinga za binadamu wakati mkipumzika na ibilisi huko

Jenny Hedstrom akaandika:

Inakatisha tamaa. Rais Museveni leo amesaini Muswada wa kupiga marufuku Ushoga

John Paul Torach alibaini kuwa serikali na wapinzani walikuwa na lao moja kwenye suala hili:

Tena kinachopiga kelele kuliko kusainiwa kwa muswada huu ni kimya cha wanasiasa wa upinzani…wakikubaliana wote…unajua umeshapoteza

Eriche White Walker alifikiri kuwa viongozi wa dini wameshindwa kuhimiza maadili kwa watu:

Serikali inapoanza kuingilia mambo ya maadili kwa kutumia sheria maana yake viongozi wa taasisiza kidini wameshindwa kazi

“Mimi ni Mwafrika” alihoji kuwa mambo ya hisia za kijinsia ni ya kibinafsi na hayapaswi kuingiliwa:

Siwezi kuelewa wanaounga mkono mswada huu! Huwezi kuwalazimisha watu wengine wakubaliane na mtazamo wako wa mambo ya ujinsia. Hakuna anayesema lazima uwe shoga!

Stuart Grobbelaar kwa mzaha anasema Uganda ipitishe sheria itakayopiga marufuku talaka na kuhakikisha ndoa ifungwe kwa vijana bikra pekee:

Mmefanya vizuri kupitisha sheria hiyo. Hebu sasa, mniambie lini tutashuhudia miswada ya kupinga talaka, kupinga ndoa za wasio bikra?

Wananchi wa Uganda sasa hawana hakika nini kitatokea kuhusiana na diplomasia ya mahusiano ya nchi hiyo na nyingine, hususani Magharibi, zinazoamini sheria hiyo inavunja haki za msingi za binadamu.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.