Waziri wa Uganda: Wanawake Wasiovaa Mavazi ya Heshima Wanaomba Kubakwa

A screenshot from the petition calling for the minister's resignation.

Picha ya tamko linalomtaka waziri huyo ajiuzulu.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Vijana wa Uganda Ronald Kibuule, wanawake wanaovaa mawazi yasiyositiri miili yao wanaomba kubakwa, na watuhumiwa wanaodaiwa kuwabaka wanawake waliovaa namna hiyo waachiliwe huru. Alisema vile vile kuwa katika kesi za ubakaji, polisi wawe wa kwanza kusimamia namna wanawake hao waathirika walivyovaa, na kama wamevaa hovyo, nao washitakiwe kwa kosa la kukaribisha uhalifu.

Kibuule alitoa matamshi hayo akiwa kwenye halmashauri [kaunti] ya Kajara, wilayani Ntungamo siku ya Jumamosi Septemba 21, 2013 wakati akihudhuria ufunguzi wa Chama cha Ushirika na Akiba cha Vijana wa Kajara. Kauli hiyo ilionekana kwenye gazeti la Uganda Daily Monitor la Septemba 24, 2013. Makala hiyo, hata hivyo, haikueleza mukhtadha ambao Kibuule alitoa matamshi hayo.

Bunge limemtaka waziri huyo ajieleze bungeni ilikuwaje akatoa matamshi hayo juma lililopita.

Raia wa Uganda mtandaoni walijadili matamshi hayo kwa hasira wakitumia alama habari #Kibuule kwenye mtandao wa twitter. Wale waliomtaka ajiuzulu wanatumia alama habari #KibuuleMustGo [Kiluule Lazima Ang'oke] na #KibuuleOut [Kibuule Nje].

Tamko lililopo kwenye mtandao wa Change.org linamtaka ajiuzulu:

Kwa manano haya, Bw. Kibuule anautangaza ubakaji wa wanawake kwa kigezo la mavazi yao; anawahurumia wabakaji kwa makosa yao ya jinai waliyoyafanya kwa wanawake wanaodaiwa kuvaa vibaya na; anahakikisha waathirika wa ubakaji wanapata hofu ya kujitokeza hadharani kwa kuogopa kushitakiwa kwa kubakwa. Lazima aachane na msimamo huo haraka sana kwa kuwa ni wazi alichokisema hakiwakilishi ustawi wa wapiga kura wake.

Rosebell Kagumire (@RosebellK), mwandishi wa Uganda mtandaoni, aliandika:

Watoto 4000 kaskazini mwa Uganda wananajisiwa kila mwaka. Nina hakika Kibuule anadhani ni kwa sababu watoto hao walivaa vibaya! Wajinga walio madarakani!

Wandera Samuel (@wandyBlackstig) anatafakari mawazo haya ya Waziri yametokea wapi:

Kibuule anakaa kwenye kochi|anabadilisha badilisha chaneli za runinga | anajikuna sehemu nyeti| anafikiri —> kwamba wasichana waliovaa vimini wabakwe

Linda (@LindaNEK), mfanyabiashara wa ki-Ganda, alikejeli mamlaka ya kimaadili aliyonayo waziri:

Kibuule hana ubavu wa kimaadili kutoa matamshi hayo yanayohusiana na Maadili hasa sote tukijua jamaa ana wake wengi @DailyMonitor

Mark Namamanya (@mnamanya), mwandishi wa michezo, aliona alibaini:

Katika jamii nyingi, mtu anayefanya kituko kama Kibuule angekuwa anafanya mkutano na waandishi wa habari kutangaza kujiuzulu. Inasikitisha, si moja ya jamii hizo nyingi

Gordon G Ananura (@NgabiranoIV) alijiunga na wale waliokuwa wakimkejeli waziri:

Nilijua kuwa Kibuule ni kichekesho

Hata hivyo, baadhi ya wa-Ganda kama Ibrahim Batambuze (@TheBigPapaa) waliunga mkono matamshi ya waziri:

Ninaungana na wewe kwa asilimia 100. Kama unaacha milango yako wazi na anakuja jambazi anakuibia, unamlaumu nani kwa ujinga wako?

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.