Ethiopia: Mwanablogu Ahukumiwa Miaka 18 Jela kwa “Kuvunja Katiba”

Makala hii ilionekana mwanzo katika tovuti ya Electronic Frontier Foundation. Imehaririwa kidogo kwa ajili ya hadhira ya Mradi wa Utetezi wa Global Voices

Mnamo Mei 1, Mahakama Kuu ya Ethiopia ilitoa hukumu kali kwa mwandishi aliyeshinda tuzo Eskinder Nega, ambaye sasa atatumikia kifungo cha miaka 18 jela. Nega aliwekwa ndani Septemba 2011 na kufunguliwa mashitaka ya “ugaidi” chini ya sheria isiyoelewekaw nchini Ethiopia ambayo imekuwa ikitumiwa kuwalenga waandishi wa mtandaoni na wapinzani wa kisiasa. Mashitaka yake na rufani yake vilicheleweshwa mara kwa mara, wakati makundi ya kimataifa ya watetezi wa haki za kibinadamu na uhuru wa kujieleza yaliendelea kuikosoa hukumu na adhabu yake hiyo. EFF, PEN America, ambayo ni Kamati ya Kuwalinda Waandishi, na mashirika mengine yalifanya kampeni ya kumweka huru, na hata jopo la Umoja wa Mataifa liliiona hukumu hiyo kama uvunjifu wa sheria ya kimataifa.

Mohamed Keita wa Kamati hiyo ya Kuwalinda Waandishi katika kuujibu uamuzi huo wa mahakama, “Kushitakiwa kwa Eskinder na waandishi wengine ni dalili za utawala unaoogopa maoni ya raia wake.”

Free Eskinder campaign image.

Picha ya kampeni ya Kumwachia huru Eskinder.

Eskinder Nega alikwenda Marekani kwa elimu ya juu, akisoma katika Chuo Kikuu cha Marekani kabla hajarudi Ethiopia kufanya kazi ya uandishi. Alianzisha magazeti manne -yote yakikumbana na mkono wa serikali na kufungiwa- na amewahi kufungwa mara kadhaa kwa sababu ya makala zake zilizoonekana kuiudhi serikali. Alinyang'anywa leseni yake ya uandishi wa habari, na hapo ndipo Nega alipoamua kuhamia mtandaoni, akawa mwanablogu anayetumia majukwaa ya mtandaoni kujadili hali ya kisiasa nchini Ethiopia. Wakati waaandishi wengi nchini Ethiopia wamenyamazishwa na wengine kuamua kuikimbia nchi katika juhudi za kuyalinda maisha yao na ya familia zao, Eskinder Nega aligoma kata kata kuihama nchi wala kuacha kuandika. Ujasiri wake na kujitolea kwake kama mwanndishi kumemfanya awe alama muhimu yenye hadhi ya kimataifa ya uhuru wa habari na nguvu ya mtandao wa intaneti katika kuhakikisha kuwa haki ya kusema kwa uhuru inaendelea kuwepo katika mazingira kandamizi.

Eskinder Nega aliandika kwa moyo kuhusiana na fursa ya Ethiopia kulinda haki za binadamu na uhuru wa kujieleza. Katika makala moja kwenye blogu yake, aliandika hivi:

Utawala wa kidhalimu umeanza kupoteza nguvu yake. Tayari umepoteza swahiba mkuu, katika nchi za Kiarabu. Kasi sasa iko kwenye uhuru. Uhuru hauna rangi. Uhuru hauna dini. Uhuru haupendelei kabila. Uhuru haubagui nchi tajiri na masikini. Kwa hakika, Uhuru haukwepeki nchini Ethiopia, utatamalaki tu.

Maandishi ya Eskinder Nega yametengeneza upenyo wa kuona hali halisi ilivyo katika nchi ya Ethiopia na yamefanyika dira kwa watu wa ethiopia na hata duniani kote. Kufungwa kwake mara kwa mara kunaonyima dunia sauti ya kiuandishi ya aina yake na yenye nguvu kutoka katika eneo hilo la dunia lenye njaa taarifa sahihi, za haki na zenye kuonyesha upande wa pili.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.