Suluhisho la Kiradikali la Umaskini Duniani: Ufunguzi wa Mipaka

Tarehe 18 Disemba ilikuwa ni siku ya kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji [fr]. Wakati wa mgogoro uliopo wa hali mbaya ya fedha duniani, uhamiaji kutoka nchi zinazoendelea umelaumiwa na vyama kadhaa vya kisiasa kuwa ndiyo chanzo cha ukosefu wa ajira katika nchi hizo. Japokuwa hapajakuwa na utafiti wowote, mpaka sasa, ambao umethibitisha kuwa uhamiaji umekuwa na mchango wowote muhimu katika tatizo la ukosefu wa ajira, imani hii imeendelea kujikita katika fikra za watu wengi.

Jambo jingine ambalo limelojikita sana katika jamii zilizoendelea: ni ongezeko la kampeni za misaada ya kibinadamu wakati wa kipindi cha sikukuu (za mwisho wa mwaka).

Naam, kila mwisho wa mwaka katika nchi zilizoendelea zaidi, uanweza kuona kampeni ambazo zinahimiza raia wake kutoa michango ya kupigana na umaskini katika nchi za mbali ambazo hazina bahati.

Na zaidi ya taswira za umaskini uliokithiri zinazoonekana mara kwa kwa mara wakati wakipindi cha sikukuu (ambazo pia zinaitwa”picha za ngono ya umaskini” katika sekta ya maendeleo pale ambapo taswira za watu maskini zinapotumiwa sana na mahirika ya misaada), pia kuna takwimu za kuogopesha:watu bilioni 1.4 wanaishi kwa chini ya dola 1.25 kwa siku. Bila kujali maendeleo yasiyopingika katika nyingi ya nchi za kiAfrika, ukosefu wa usawa wa kijamii bado unaendelea kustua barani Afrika.

Wanauchumi wanakadiria kuwa 1/3 ya watu maskini duniani watakuwa wanaishi katika bara la Afrika ifikapo mwaka 2015. Ni ukweli, kuwa hali ngumu ya uchumi ni moja ya sababu zilizotajwa na milioni 700 duniani ambao wako tayari kuhama kutoka nchi zao za asili.

Nomads in Morocco on Flickr by Antonioperezrio (CC-NC-2.0)

watu wanaohamahama nchini Morocco kwenye Flickr na Antonioperezrio (CC-NC-2.0)

Mara nyingi inaonekana kana kwamba nchi ambazo hazijaendelea kabisa haziwe tu kuepuka laana ya umaskini, bil ya shaka hazina uwezo wa kukabili ukubwa wa majukumu waliyonayo. Na zaidi ya hivyo, nchi hizo mara nyingi hukumbushwa jinsi zisivyokuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya watu wao bila ya misaada ya kimataifa. Japokuwa misaada ya kimataifa ni matokeo ya matatizo ya dharura, hali hii mara nyingi huchukuliwa kama tusi kwa fahari ya utaifa.

Wataalamu kadhaa wanadai hata hivyo, kuwa umaskini uliokithiri hauepukiki. Kwa wataalamu wengi wa kiuchumi, suluhisho la kiradikali zaidi la kupunguza umaskini kwa haraka duniani ni, kufungua mipaka kati ya nchi na kuruhusu wafanyakazi kuhamia sehemu ambazo nguvukazi inahitajika zaidi.

Maprofesa Marko Bargaric na Lant Pritchett ni wanazuoni wawili wa kwanza kuwasilisha dhana ya “mipaka iliyo wazi” kama suluhisho la kupunguza umaskini duniani.

Ili kuhitimisha hivyo, Bagaric anaandika::

Kutuma rasilimali kwenda sehemu maskini kuna tija. Lakini ni njia ya taratibu na isiyotabirika ya kuboresha ustawi wa watu. Badala yake, tunafuatilia lengo hili kwa kuwezesha uhamiaji wa watu ili kwamba waweze kusafiri kwenda kule ambapo rasilimali zipo. […] Tatizo la njaa kwa kifupi ni tatizo la usambazaji, na si la upungufu. Njia bora zaidi ya kuongeza kasi ya kupunguza umaskini katika Dunia ya Tatu ni kuongeza uhamiaji kelekea (nchi za) Magharibi kwa kiwango kikubwa. Wakiachwa watumie mbinu zao wenyewe watu wengi wataishia kwenye njia endelevu za kujikimu, amabzo zitapelekea kwenye mizani butu kati ya rasilimali zilizoko duniani na watu wake.

Lant Pritchett anafafanua dhana hii kwa kina katika kitabu chake: Waache Watu Wake Waje; Kuvunjwa kwa Ukomo wa Sera ya Uhamiaji wa Kimataifa wa Nguvukazi. Ananukuu matokeo ya tafiti inayodai kuwa:

Kuondoa vikwazo vya uchumi vilivyobakia duniani kutaongeza Kipato (GDP) Cha dunia kwa takriban Dola za Kimarekani bilioni 100.
Kuondoa vikwazo vya uhamiaji, tukilinganisha, kutaweza kuongeza maradufu kipato cha dunia: yaani, ongezeko la kipato cha dunia kwa dola za Kimarekani trilioni 60.
Ongezeko hili la utajiri litagawanywa, lakini watakaonufaika kwa wingi watakuwa ni watu ambao sasa wanaishi katika nchi maskini.

Demonstrations held in favor of the immigrants’ right to work in Paris  by austinevan on Flickr (CC-NC-SA-2.0)

Maandamano ya kuunga mkono haki ya wahamiaji kufanya kazi jijini Paris na austinevan kwenye Flickr (CC-NC-SA-2.0)

Benki ya Dunia ilichapisha tafiti kuhusu mchango wa wahamiaji katika uchumi wa nchi zao za asili kwa njia ya utumaji pesa kutoka nje. Tafiti hiyo pia inaonyesha kuwa pesa zinazotumwa kutoka nje kuelekea nchi zinazoendelea zinatarajiwa kuongezeka na kufikia mpaka dola bilioni 351, na kufikia dola bilioni 481 duniani zikijumuishwa nchi zilizoendelea. Tafiti hiyo pia inaeleza kuwa:

Mtiririko wa pesa zinazotumwa kulekea nne ya sehemu sita zilizowekwa na Benki ya Dunia uliongezeka zaidi ya ulivyotarajiwa – kwa asilimia 11 kuelekea Ulaya ya Mashariki na Asia ya Kati, asilimia 10.1 kuelekea Asia ya Kusini, asilimia 7.7 kuelekea Asia Mashariki na Pasifiki na aslimia 7.4 kuelekea afrika Kusini ya jangwa la Sahara, bila kujali hali ngumu ya uchumi barani Ulaya na katika sehemu nyingine walizofikia wahamiaji wa Kiafrika.

Haihitaji kueleza kuwa, nadharia hizi zilizo tofauti na nadharia za kihafidhina zinahojiwa na wataalamu kadhaa pamoja na wanasiasa. Frank salter anafafanua kuwa hofu kubwa iko kwenye matatizo yaliyopo kwenye kila jamii yenye tamaduni mbalimbali:

Uhamiaji usio na kikomo utaharibu maslahi ya taifa (la Australia) kwa namna ambazo zimeandikwa na wanazuoni wa uchumi, soshiolojia na fani zinazohusiana nazo. Madhara makubwa yanatabiriwa kutokea kwenye kile kinachojulikana kuhusu matatizo yaliyopo kwenye (jamii zenye) utofauti. Yanayojumuisha ongezeko la ukosefu wa usawa hasa kwenye namna ya ubaguzi wa matabaka yanayotokana na asili za watu [..] Utofauti pia umehusishwa na kupungua kwa demokrasia, kuzorota kwa uchumi, kuporomoka kwa mshikamano wa kijamii na misaada kutoka nje, vile vile ongezeko la ufisadi pamoja hatari ya migogoro ya kiraia

Kutokea kwenye mtazamo wa kisiasa, bara la Ulaya lipo mbali na kufungua mipaka, na pengine ni tofauti ya hivyo. Nchini Ufaransa Sheria ya Guéant inazuia uwezekano wa wahitimu wa masomo kutoka nje kuajiriwa, jambo ambalo limezua miitiko mablimbali. Julie Owono, mshirika wa Global Voices, anaelezea maana ya sheria hii na miitiko ya wanablogu mbalimbali wa kiAfrika ambao wanaiona sharia hii kama sababu ya ziada ya kuchangia maendeleo kwenye nchi zao. Katika blogu ya Rue69, Owono anaongezakwamba Sheria ya Gueant pia inawabagua wanafunzi kutoka nje ambao wana uwezo mdogo wa kifedha. [fr].

Barani Afrika, ni wataalamu wachache tu ambao wameisoma dhana ya mipaka iliyo wazi, dhana ambayo, bila ya shaka, iko mbali sana na ukweli uliopo barani ili kuendelezwa. Profesa wa falsafa wa Chuo Kikuu cha McGill, Arash abizadeh, hataki kuhimiza kufunguliwa kwa mipaka, hata hivyo nasema kuwa mfumo uliopo wa mipaka hauwezi kuhalalishwa kwa mantiki ya uwazi ya kiliberali. Abidazeh anasema kuwa ikiwa tunataka kushikilia imani kuwa “binadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa”, mfumo wa mipaka, wenyewe, ni uvunjifu wa kanuni hiyo.

Mwanablogu wa kiMalagasi Sly anaandika kuhusu hatari za kufungua mipaka:

Mimi ni muAfrika na wakati inaonekana kana kwamba wazo hili litakuwa zuri kuna madhara kadhaa:
-biashara ya watoto
-biashara ya mihadarati
-Kusambaa kwa VVU na magonjwa mengine
-wakimbizi wataunda kambi kwenye nchi tajiri zaidi na kusababisha matatizo
Pamoja na kusema hivyo baadhi ya nchi barani Afrika zina mipaka iliyo wazi na baadhi ya majirani zao.

Sly anagusia ukweli kuwa kufungua mipaka kati ya Kenya, Uganda na Ethiopia, katika jaribio la kuongeza mshikamano wa kiuchumi, ulizua changamoto kubwa katika kanda hiyo wakati wa balaa la njaa la hivi karibuni.

Dhana hii ya kutumia kufungua mipaka ili kupunguza ukosefu wa usawa kijamii duniani inamaanisha kwamba kupunguza umaskini duniani kungekuwa ndiyo kipaumbele cha juu zaidi duniani. Kingekuja kabla ya masuala mengine muhimu kama vile usalama wa taifa na maslahi ya taifa ya nchi yoyote. Nadharia hii ya Pritchett na Magric bila ya shaka ina upande tata ambao una nia ya kuchokoza mdahalo.

Hata hivyo, mbali ya madai ya jumuiya ya kimataifa inayotaka kupunguza umaskini duniani, suluhisho la mipaka iliyo wazi linaweza tu kufikiriwa katika muktadha wa namna zake na hauwezi kupewa kipaumbele juu ya vipengele vingine kwenye ajenda ya kimataifa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.