Je, Waganda Wameridhika na Utendaji wa Serikali Yao Kama Matokeo ya Utafiti Yanavyoonesha?

Voters line up at a polling station in Nyendo Masaka, Uganda, on February 18, 2011. Photo by Peter Beier. Copyright Demotix

Wapiga kura wakiwa wamejipanga kwenye kituo cha kupigia kura huko Nyendo Masaka, Uganda, mnamo Februari 18, 2011. Picha na Peter Beier. Haki miliki Demotix

Shirika la Kimarekani liitwalo International Republican Institute (IRI) lilitoa matokeo ya utafiti wake mwisho wa mwezi Machi, yaliyoonesha kwamba Waganda wengi wameridhishwa na utendaji wa serikali yao. Zaidi ya theluthi mbili ya waliohojiwa (asilimia 69) walisema kwamba kwamba serikali iko kwenye njia sahihi katika kutekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, wale waliotoa maoni yao wanadhani serikali ilikuwa inafanya vizuri au vizuri sana kwenye kusimamia uchumi, kupunguza uhalifu na kutoa huduma za msingi za jamii kama vile afya, maji safi, barabara na elimu. Hata hivyo, serikali ilionekana kufanya vibaya kwenye eneo la kupambana na ufisadi, huku asilimia 69 ya waliohojiwa wakifikiri kwamba mamlaka zinazohusika hazikuwa zikishughulikia tatizo la ufisadi inavyotakiwa.

Matokeo haya yaliibua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vikuu vya habari, na wachambuzi wengi walihoji iweje Waganda wengi wafikiri nchi yao, iliyotawaliwa na Rais Yoweri Museveni kwa karibu miongo mitatu, ilikuwa kwenye mwelekeo sahihi wa kimaendeleo.  

Kwa mujibu wa  Taarifa ya Malengo ya Maendeleo ya Mileniamu ya 2013 nchini Uganda , nchi hiyo chini ya Museveni imefanikiwa “kupunguza nusu ya idadi ya watu wanaoishi kwenye ufukara uliokithiri na kupunguza madeni yake” – na ilikuwa inafanya vizuri katika kutimiza malengo mengine nane. Nchi hiyo ina ukuaji wa wastani wa pato la ndani (GDP) wa asilimia 5.2 kwa 2013 kwa sababu ya kuuza zaidi bidhaa nje ya nchi na kukua kwa uwekezaji, na ilitarajiwa  kuendelea kukua hata kwa mwaka 2014 na 2015, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Maendeleo ya Afrika (ingawa ukame mkubwa unaweza kuwa umebadili utabiri huu).

Hata hivyo, mashirika ya kimataifa yamekuwa yakilaani matendo ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kubanwa kwa uhuru wa kujieleza nchini Uganda, ambapo utawala wa nchi hiyo umetumia sheria mpya kuwalenga wanaharakati na viongozi wa upinzani. Mwezi oktoba 2014, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International lilionesha kwamba wananchi wa Uganda “hawakuwa na uwezo wa kuwapinga watawala wao wa kisiasa, kuongea kwa uhuru na kulaani sheria kadhaa zinazopingana na haki za binadamu. ” Shirika la Human Right Watch linaorodhesha masuala yayo hayo, ikiwa ni pamoja na “vifo vya watu wasiopungua 49 wakati wa maandamano ya mwaka 2009 na 2011.”

‘Watu hawakui ili waupende na kuuenzi udikteta’

Wasomaji waitoa maoni mengi wakichambua matokeo hayo ya kura ya maoni yaliyochapishwa kwenye tovuti ya gazeti binafsi linaloheshimika nchini Uganda na linalochapishwa kila siku liitwalo Monitor. SagInc, akitolea mfano wa madikteta wanaofahamika, aliandika:

Swali ni nani aliomba na kufadhili utafiti huu ufanyike? Utashangazwa na kiasi cha pesa kilichotumika na nani hasa walizitoa fedha hizo. Madikteta wa zamani kama Ben Ali wa Tunisia, Suharto wa Indonesia, Yakubu Gowan na Nigeria, Nicolae Ceaușescu wa Romania wote walishiriki kuchakachua mitazamo ya jamii ili kupalilia udikteta wao na kujaribu kuficha hali halisi ya mambo na hata hivyo hawakuweza. Historia inatuambia kwamba watu hawakui kuupenda na kuuenzi udikteta isipokuwa kinyume chake.

IRI inasema kura hiyo ya maoni ilifanyika kati ya Desemba 2014 na ilifadhiliwa na shirika la misaada la Marekani, wakala wa Marekani kwa Maendeleo ya Kimataifa.

Waganda wana kila sababu ya kuwa na wasiwasi. Siku chache baada ya matokeo hayo kutandazwa, vyombo vya habari nchini humo viligundua kwamba serikali inasemekana ililipa shirika moja la mahusiano ya umma lenye makazi yake nchini Marekani shilingi milioni 614 za Uganda (sawa na $206,000, au euros 174,000) “kuitengeneza vizuri taswira ya Uganda” baada ya mtafaruku ulioenea duniani kote kufuatia sheria inayofanya mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja kuwa kosa la jinai linaloadhibiwa kwa kifungo jela kwa baadhi ya mazingira. Sheria hiyo ya kupambana na ushoga  ilibatilishwa na mahakama ya katiba ya nchi hiyo mwezi augusti 2014.

Habari picha haki miliki ya International Republican Institute.

Nchini Uganda, asilimia 65 wa watu walioshiriki utafiti huu wanaunga mkono ukomo wa madaraka, suala ambalo linaendelea kubeba umuhimu kila uchao. Tayari Museveni amechaguliwa na chama cheke cha National Resistance Movement kugombea kwa mara nyingine kwenye uchaguzi wa mwaka 2016, ingawa kuna mkanganyiko kuhusu uwezekano wa kuchaguliwa kwake  kwa sababu ya ukomo wa umri uliowekwa na katiba (Museveni ana miaka 70, na atazidi ukomo huo — miaka 75 — wakati wa kipindi cha miaka mitano atakachokuwa madarakani). Mwezi Januari 2015, Museveni alisema hayuko tayari kukabidhi madaraka kwa viongozi wa upinzani, akiwaaita “mbwa mwitu wanaotaka kuisambaratisha Uganda.” 

James alikuwa na maoni haya:

Uchaguzi na ukomo wa awamu ya uongozi ndio mtazamo wa wengi. Takwimu zilizobaki ni uchakatuzi tu.

‘Udikteta, mauaji, uongo’

Kwenye tovuti hiyo hiyo, mchambuzi Jomo alijiuliza kama washiriki wa utafiti huo walikuwa na taarifa za kutosha:

Sijui kama watafiti walizingatia ukweli kwamba wananchi wengi wa Uganda (hii ni busara ya mtaani isiyohitaji usomi), mjini na vijijini, hawana uelewa wa mambo, na wanategemea tetesi, au taarifa zinazotolewa na taasisi za serikali, ili wawe na mtazamo fulani.

Augustus Karube alifikiri utafiti huo unatoa taarifa muhimu kwa vyama vya siasa na alifikiri namna viongozi wa vyama vya siasa wanaweza kutumia utafiti huu:

Kilicho muhimu zaidi, kwa upinzani ni, namna ipi nzuri ya kutumia taarifa hizi, kujiandaa, kujenga mikakati, kwa lengo la kushughulikia masuala muhimu, yaliyoguswa kwenye utafiti huu mdogo. Vyama vya siasa vichunguze masuala ambayo washiriki wnegi hawakuyakubali au waliyapinga au walishangazwa nayo, hata hivyo wasiyazingatie sana. Lakini pia wasiyapuuze na kuyaona ni takataka.

Angalau, utafiti huu ni waraka tu, unaotoa mwelekeo wa hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, chini ya utawala huu, kama yanavyotazamwa kupitia maisha na uzoefu wa wapiga kura wenyewe, ukiacha ukweli ambao hauwezi kusemwa. Tumieni utafiti huu kwa busara. Chochote kisipuuzwe na kuchukuliwa kijuu juu, na pia tusichukulie kila kilichosemwa kuwa ni uongo au ukweli. Una maoni gani? Kama ungeulizwa na hukuulizwa?

Vyma vya upinzani nchini Uganda vimetishia kugomea uchaguzi wa rais na wabunge utakaofanyika mwezi Februari 2016, kwa hoja kwamba Tume ya Uchaguzi una upendeleo  kwa Museveni na chama chake kinachotawala na wanadai ibadilishwe. 

Uchambuzi uliofanywa na Moses Khisa, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu ya sayansi ya siasa ya Chuo Kikuu cha Northwest huko Illinois, Marekani kwenye gazeti la Observer la nchini Uganda akikosoa matokeo hayo ya utafiti na kuyaita kuwa “uwongo mtupu” ulipokelewa kwa hisia tofauti na raia. Msomaji ajiitae mungu aliandika:

MK lazima na wewe ukubali kwamba dhana yako ya ‘mwelekeo sahihi’ inatofautiana sana na ile ya wananchi wa Uganda.
Kwa Waganda mapungufu yote ya utawala wa M7 [Yoweri Museveni] kwa kweli ni kama muziki mtamu na welekeo sahihi wa mambo. Kijijini kwangu watakwambia [Museveni] alisaidia kupunguza vumbi kwenye barabara zao kwa sababu tangu aingie madarakani hakuna mtoto wao aliwahi kufaulu kimasomo, na kupata kazi inayolipa kumwezesha kununua hata gari. Kwa hiyo hata barabara ya lami inayojengwa kijijini kwao hawana kazi nayo. Ni kukataa ustaarabu wa kimagharibi labda? Fikiria zaidi

Francis, msomaji mwingine, aliandika:

Unaweza kuandika nini kuhusu M7/NRM/NRMO [Museveni] na National Resistance Movement/National Resistance Movement Organisation] kuliko Udikteta, Mauaji, Uongo, Undugu, Urafiki, Unyang'anyi wa ardhi, Ghasia, Matumizi ya Jeshi, Ujambazi, Wizi, Ufisadi, Utawala wa kiimla, Vitisho, Umasikini, mfumo mbovu wa elimu, Ukabila, udini, udanganyifu.

Miongoni mwa wasomaji wa gazeti hilo la kila siku, Peter ni mtu pekee aliyeotoa maoni chanya:

Kama nchi inaelekea kwenye mwelekeo sahihi na Museveni anafanikiwa kwa alama za juu, mantiki ni kwamba hakuna tatizo. Matatizo mengine yanayotengenezwa hayapo, na hayana msingi. Wale wanaotaka kuingia madarakani wasubiri mwaka 2016, ili kuiona Uganda ikisonga mbele kwenye uelekeo sahihi.

Bambalazaabwe Ssemakula aliwakilisha maoni ya wengi:

Kuwe na utafiti au usiwe na utafiti, hakuna kitakachobadilika maadam wale walio madarakani hawaoni kwamba taarifa hizi kuwa za kutiliwa maanani kwa sababu haziipendezi NRM [Chama tawala tawala kinachoongozwa na Museveni]

Waganda kwenye mtandao wa Twita, nao kadhalika, walikuwa na maoni kuhusiana na matokeo hayo, kwa utumia alama habari ya #IRIUgandaPolls. Watumiaji wa twita  T.Ddumba pamoja na mwanafunzi wa uandishi wa habari Kemigisa Jacky waligusia ahadi hewa za wanasiasa:

Ahadi nyingi lakini hakuna maono mengi, hakuna kinachofanyika katika hali halisi, lakini asilimia 69 ya Waganda wanaamini nchi yao iko kwenye uelekeo sahihi wa kimaendeleo

Mtaalam wa maji na usafi  Fredrick Tumusiime, anayeishi Kampala, alijibu twiti hizi, akisema:

Kama mwelekeo sahihi maana yake kuweza kulala na kuamka siku ya pili, basi nchi iko pahala pake. Wananchi hawana matarajio makubwa

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.