Watoto Waliokosa Masomo kwa Miezi kadhaa, Wafundishwa kwa Njia ya Skype Nchini Libya

Children in Tripoli in August 2011. Photo by MITSUYOSHI IWASHIGE. Copyright Demotix

Watoto wakiwa huko Tripoli, Agusti, 2011. Picha na MITSUYOSHI IWASHIGE. Haki miliki Demotix

Makala na taarifa hii ya habari iliyoandaliwa na  Shirin Jaafari  kwa ajili ya kipindi cha redio kiitwacho  The World kwa mara ya kwanza ilionekana kwenye tovuti ya PRI.org  siku ya tarehe 26 Februari 2015, inachapishwa tena chini ya makubaliano ya ushirikiano wa maudhui.

Katika kipindi ambacho Libya ilikuwa ikiharibiwa vibaya kutokana na mapinduzi yaliyotokea mwaka 2011, ndicho kipindi hicho hicho Haifa El-Zahawi aliondoka kuelekea Marekani.

Kwa sasa anatafuta kazi akiwa kama daktari wa afya ya kinywa. Lakini pia, anautumia muda wake katika mradi mwingine tofauti: Anafundisha watoto nchini Libya.

Hali tete ya kiusalama nchini Libya imewafanya watoto washindwe kwenda shule tangu mwezi Oktoba. Kwa kuwa watoto hawawezi tena kuhudhuria masomo katika shule zao, El-Zahawi aliwaza ni kwa nini asisogeze madarasa karibu na huko walipo? Na hapa ndipo Shule ya Skype ya Benghazi ilipozaliwa rasmi.

“Tulianza na akaunti ya mtu binafsi pamoja na Skype”, anasema El-Zahawi akiwa mjini New York. Aliweka taarifa za mradi wake huu katika mitandao ya kijamii akiwaomba raia wa Libya kumsaidia. Katika muda wa wiki moja amepata “matokeo makubwa na ya kutia moyo kabisa.” Pia alipata habari kuwa kuna kampuni moja ya Teknolojia ya Mawasiliano ilitaka kumfadhili.

Hata hivyo, masomo kupitia mtandao wa intaneti yana changamoto zake. Upatikanaji wa mtandao wa intaneti usiotabirika ni kikwazo kikubwa kinachochangiwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara linalowakabili raia wa Libya. “Tunajaribu kwa kadiri tuwezavyo kuhakikisha wanafunzi wanapata masomo papo kwa hapo, lakini kutokana na changamoto zilizopo … tunajaribu kurekodi masomo na kisha kuyapakia mtandaoni,” El-Zahawi anasema.

Lakini, pamoja na changamoto hizi, Shule ya Skype ya Benghazi hadi sasa imekuwa na mafanikio makubwa. “Familia zimetutumia picha zinazoonesha wanafunzi wakifanya kazi wanazopewa na mwalimu wao,” El-Zahawi anasema. “Pia, wanavaa sare zao za shule.”

Wazo kuu la kuanzisha shule hii, El-Zahawi anasema ni kurudisha matumaini kwa familia na watoto “wanaohitaji elimu.” Anaogopeshwa na habari kama hii ya hivi karibuni ya kuchinjwa kwa watu kadhaa nchini Libya na kundi la ISIS, na anaamini kuwa kwa kuwaelimisha watoto wa Libya kutasaidia kukomesha kuenea kwa ukatili huu.

“Tunahitaji kuwapatia elimu watoto wetu,” anasema, “elimu tu ndiyo itakayotusaida kupambana na hali hii.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.