Hofu ya Yaliyotokea? Likizo ya Rais Mpya wa Zambia Yaibua Mjadala wa Afya Yake

President Edgar Lungu on a helicopter ride viewing the South Luangwa National Park during a holiday he took two weeks into office. Picture used with permission of Salim Henry/SHENPA.

Rais Edgar Lungu akiwa kwenye helikopta akiangalia Hifadhi ya Wanyama ya Luangwa Kusini wakati wa likizo yake aliyoichukua majuma mawili tu baada ya kushika madaraka. Picha imetumiwa kwa ruhusa ya Salim Henry/SHENPA.

Majuma mawili tu baada ya kushika madaraka, rais mpya wa Zambia Edgar Lungu amelishangaza taifa kwa kuchukua likizo, hali inayoibua maswali kuhusu afya yake — suala ambalo liliibuliwa awali wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi wa Januari 20 kumchagua mrithi wa Rais Michael Sata, aliyefariki akiwa madarakani mnamo Oktoba 28, 2014.

Kabla ya kushinda uchaguzi na kumrithi Sata, Lungu alifanya uchunguzi wa afya kwenye hospitali ya Lusaka Trust pamoja na Hospitali ya Kijeshi ya Maina Soko, zote zikiwa umbali mdogo tu kutoka yalipo makazi ya rais, ikulu, wilaya ya Woodlands jijini Lusaka. Akijaribu kuachana na utaratibu wa mtangulizi wake wa kuficha taarifa zake zinazohusiana na afya, msaidizi wake wa habari  Amos Chanda alisema kwenye taarifa yake:

Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu, Rais wa Jamhuri ya Zambia amechunguzwa afya yake mara mbili kwenye Hospitali ya Kijeshi ya Maina Soko na Hospitali ya Lusaka Trust.

Rais Lungu alifanyiwa uchunguzi wa kina kwenye Hospitali ya Maina Soko na kisha kuchunguzwa kinywa kwenye Hospitali ya Lusaka Trust. Madaktari wamemthibitishia kwamba afya yake iko imara.

Hata hivyo, likizo yake hiyo, iliyoanza baada ya  shughuli yake ya kwanza kimataifa ya kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) Addis Ababa, Ethiopia,  iliwastua watu. Lungu, mwanasiasa ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alikwenda kwenye hifadhi ya wanyama za Luangwa Kusini, moja wapo ya vivutio vikuu vya watalii nchini Zambia, akiwa hata hajamaliza kuteua Baraza lake la Mawaziri  wakati huo.

Rais Lungu, alinukuliwa na jarida la The Post, akitetea  uamuzi wake wa kwenda kwenye kile alichokiita mapumziko :

Nimekwambia kwamba sitakuwa na siku za fungate. Kuna tofauti kati ya likizo na mapumziko, nilikuwa nachungulia kamusi yangu asubuhi hii na ninajiuliza, ‘hawa watu wanajua tofauti hii?’

Ninaenda mapumzikono, sina likizo. Huendi likizo ukiwa umeambatana na watumishi wote wa ofisi yako. Katibu wa Baraza la Mawaziri naye anaambatana na mimi na hata baadhi ya Mawaziri na maafisa wa ikulu hawaendi kuniliwaza, ila kunisaidia kufikiri uteuzi ninaoufanya.

Aliongeza:

Ninavijua vipaumbele vyangu; baadhi ya watu wanasema, ‘Lungu hajui vipaumbele vyake’. Kipaumbele changu ni watu wa Zambia. Namna gani ninafanya kazi yangu si shughuli ya mtu mwingine yeyote kujua, ni yangu. 

Wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi wa Januari 20, Makamu wa Rais wa Chama cha Upinzani cha UPND, Canicius Banda, daktari wa tiba, alisema chama kinachotawala cha PF anakotoka  Rais Lungu kina kazi ya kulishawishi taifa kwamba hana matatizo ya kiafya kwa sababu cheti cha uchunguzi wa afya ambacho chama chake kimekiona kinaonesha kwamba mkuu huyo wa sasa wa nchi anaugua maradhi ya figo.

Banda baadaealikanusha madai yake kwamba aliona cheti cha uchunguzi wa afya ya Lungu.

Mwanablogu Elias Munshya Munshya, alijibu madai ya Banda kwamba aliona cheti cha uchunguzi wa afya ya Lungu aliandika:

Ninaweza kuona kwa nini baadhi ya Wazambia wana sababu ya kuwa na wasiwasi na afya ya wagombea urais. Lakini kudai tarifa za kiafya za wagonbea ni upuuzi kama ilivyo kutaka wagombea wawe na kiwango fulani cha elimu. Kama tunahitaji kweli kujali vyeti vya uchunguzi wa afya, basi maswali yanayofuata yanayohitaji majibu: tutaishia wapi? Hivi ushahidi kwamba mtu anaugua maradhi ya mapafu unaatiri uwezo wake kutawala? Hii ndio sababu katiba yetu inataka tu kwamba mtu hawezi kutawala kama ‘hali yake ni mbaya’. Haisemi kwamba mtu hatatawala kwa sababu tu ni mgonjwa, kwa sababu kusema hivyo kusingetekelezeka. .

Inaeleweka kwa nini Wazambia wana wasiwasi na afya ya marais wao au wale wanaotaka kuwa marais. Nchi hiyo imeshuhudia vifo vya wakuu wawili wa nchi –Levy Mwanawasa, aliyefariki mwaka 2008 nchini Ufaransa baada ya kupatwa na kiharusi akiwa kwenye majukumu yake ya Umoja wa Afrika nchini Misri, na sata, ambaye alikuwa akiiugua na kupelekwa Uingereza kwa uchunguzi wa afya, lakini baadae alifariki akiwa kule. Rais wa zamani Frederick Chiluba, rais wa pili kutawala nchi hiyo, alifariki nchini Zambia baada ya safari nyingi kwenda Afrika Kusini kwa matibabu na uchunguzi wa afya kwa matatizo yanayohusiana na moyo.

Lungu aliwashinda wagombea wengine 10, akishinda kwa asilimia 1.66 mbele ya mpinzani wake mkuu, Hakainde Hichilema wa chama cha Upinzani cha UPND, na kuwa Rais wa sita wa Zambia tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1964.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.