Ebola Haijafika Gambia, na Watu Wanashughulika Kuhakikisha Hali Inabaki Kuwa Hivyo

The logo of #EbolaFreeGambia campaign. Image source: #EbolaFreeGambia Facebook page.

Nembo la kampeni ya #EbolaFreeGambia inayolenga kuelimisha watu kukabiliana na maradhi ya Ebola. Picha imechukuliwa kwenye ukurasa wa Facebook wa #EbolaFreeGambia.

Jitihada za Gambia, nchi ndogo ya Afrika Magharibi ambayo bado haijakumbwa na mlipuko wa maradhi ya Ebola, zimeongezwa kuilinda nchi hiyo na virusi vinavyoeneza maradhi hayo.
Kufikia mwezi Agosti 31, takribani watu 1,900 katika nchi za Guinea, Liberia, Naijeria na Sierra Leone wamepoteza maisha yao, kwa mujibu wa  Shirika la Afya Duniani. Kufuatia kuthibitishwa kwa mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini Senegali , nchi jirani ya Gambia, ilikumbwa na tahayaruki kufuatia wasiwasi wa namna nchi hiyo ilivyojiandaa kukabiliana na maradhi hayo kadhalika kuhusu uelewa wa jamii kuhusiana na ugonjwa huo. Kuthibitishwa kwa mlipuko wa maradhi hayo kulisababisha kuenea kwa hofu miongoni mwa raia wa Gambia kwa sababu ya ukaribu uliopo kati ya nchi hiyo na Gambia ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa njia za panya katika mpaka wa nchi hizo. 

Muungano wa asasi za kiraia nchini Gambia umeanzisha kampeni ya   Gambia isiyo na Ebola kama jitihada za kujaribu na kuifanya nchi hiyo kujikinga na maradhi hayo. Its Ukurasa wa Facebook, ulioanzishwa tarehe 30 Agosti, tayari unafuatiliwa na watu 2,900.

Maelezo ya muungano huo kwenye tovuti yao yanasema:

Kwa kuelewa ukaribu uliopo kati ya Gambia na maeneo mengine yaliyokumbwa na mlipuko wa maradhi ya Ebola, kuna ulazima wa kuchukua hatua za dharura kudhibiti kuingia kwa maambukizi ya maradhi hayo nchini Gambia kwa kuwaelimisha watu kuhusiana na ugonjwa huo, namna unavyoambukizwa na kadhalika jinsi ya kujilinda na maambukizi. Serikali ya Gambia tangu wakati wa kulipuka kwa ugonjwa huo katika eneo la Afrika Magharibi imechukua hatua kadhaa za kuilinda nchi yetu na ugonjwa wa Ebola. Madhara ya kulipuka kwa ugonjwa huu katika eneo la Afrika Magharibi tayari yanaonekana kwa kudorora kwa uchumi wa Gambia ukiacha matatizo ya kiafya yanayoweza kujitokeza kama ugonjwa utaenea na kuingia Gambia.

Kampeni hiyo inaunga mkono jitihada za serikali kwa kukuza uelewa wa watu kuhusu kujiandaa, kujilinda na namna ya kuchukua hatua maambukizi yakitokea kwa kutumia tovuti yao, video za mtandao wa You Tube, Facebook na namna nyinginezo zinazoweza kutumika kuwafikia watu nchini humu.

Tazama moja ya video ya kampeni hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa You Tube hapa chini:

Wakati huo huo, mnamo Septemba 11 ubalozi wa Marekani mjini Banjul kwa kushirikiana na wasanii wa Gambia ulizindua wimbo maalumu kwa kupambana na Ebola. “Wimbo huo wa Ebola ” umewashirikisha wasanii Tra, Badibunka, Cess Ngum, Killa ACE, & Sandeng, na Amadou Sussocebook. Unaweza kuusikiliza wimbo huo hapa chini:

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jijini Banjul tayari imeanzisha laini ya simu inayopatikana masaa 24 kupitia mitandao yote nchini humo. Kampeni ya #EbolaFreeGambia inatofautiana na jitihada nyingine zinazochukuliwa na Wizara ya Afya zinazolenga kuwaelimisha wa-Gambia.

Habari za mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini Senegali zilimfanya mtumiaji wa mtandao wa Facebook nchini Gambia Arfang Jobe  kupendekeza kwamba  makampuni ya simu yashirikiane na Wizara ya Afya kutuma ujumbe mfupi wa maneno kuwaelimisha watu kuhusiana na ugonjwa huo.

Wakitoa maoni kwenye bandiko hilo, Hassan Njie alionya:

Jambo la mwisho kabisa tunaloweza kufikiri kulifanya ni kutuma ujumbe utakaowajaza watu hofu nchini humu. Ujumbe unapaswa kutengenezwa kwa namna nyepesi kuelewa. Watu hutafsiri na kufanyia kazi habari wanazozipokea kwa namna tofauti. Tuchukue tahadhari!

Kb Bojang alishauri:

Ninadhani itafaa pia, kama wanaweza kutuma ujumbe wa sauti kwa wateja wao katika lugha tofauti zilizopo nchini, kuhusiana na hatua za kukabiliana na Ebola, kwa sababu nina wasiwasi watu wengi hawatakuwa na muda wa kusoma ujumbe wanaotumiwa.

Makapuni ya simu yameanza kutuma ujumbe wa kuelimisha wateja wao kuhusu Ebola. Hata hivyo, haijawa wazi kama ni kweli mpango huo ni matokeo ya moja kwa moja ya kampeni ya kukabiliana na Ebola iliyoanzia kwenye mitandao ya kijamii.

Mwezi Agosti, watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford walitangaza kwamba wataanza majaribio ya kinga kwa wa-Ingereza waliojitolea kushiriki zoezi hilo wakishapata ruhusa ya kuzingatia maadili ya tafiti, na kisha zoezi hilo linatarajiwa kufanyika pia kwenye nchi za Gambia na Mali. Tangazo hili limepokelewa kwa hisia tofauti nchini Gambia huo wengine wakiwa na wasiwasi.

Akitoa maoni juu ya tanagazo hilo, Mass Bajinka aliandika kwenye mtandao wa Facebook:

Kwa nini isiwe Liberia, Naijeria na nchi nyingine ambazo tayari zina maambukizi hayo…kwa nini iwe Gambia???? Hatuna hata kirusi kimoja hapa kwa nini sasa iwe Gambia? Ninatumaini serikali haitakubaliana na mpango huo.

Eddie Baldeh alishauri:

Serikali lazima ikatae mradi huu…kwa nini iwe Gambia? Nchi ambayo haijawahi kuwa na maambukizi ya Ebola wala tetesi za maradhi hayo….Fanyeni majaribio yenu kwingine na iacheni Gambia kivyake…tena kwa amani!!!

Lakini baadhi ya watu wana mtazamo chanya na zoezi hili na wangependa majaribio yaendelee nchini Gambia:

Sababu moja kwa nini kila mmoja ana wasiwasi kuhusiana na kulipuka kwa maradhi haya ni kwa saabu wanajua hakuna tiba. Na sasa kwa sababu chanjo inaelekea kufanyiwa majaribio, sisi hawa hawa tunakuja na hisia zetu. Kila dawa iliyoko kwenye soko ina madhara yake na kabla ya kuifanya itimike kwenye tiba lazima kwanza uthibitike kuwa salama kwa wanyama kwanza na kisha inafanywa isifanye kazi kitaalam kabla ya kuanza kuitumia, ili isije ikasababisha ugonjw ahuo. Sasa kwa nini Gambia? Ni kwa sababu chanjo hujaribiwa kwa watu wasio na ugonjwa ili kuchunguza ubora wake na kitengo cha cha MRC hapa Gambia kina uzoefu wa miaka mingi katika kufanya tafiti hizi. Hebu tuwanyamazishe watu wanaopenda kukosoa kila kitu na tushukuru kwamba kuna utafiti makini unaendelea ili kuweza kupambana na maradhi hayo hatari.

Vyovyote iwavyo, ukweli ni kwamba watu wengi nchini wana wasiwasi kuhusiana na uwezekano wa virusi hivyo kuingia nchini humo.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.