Wa-Macedonia Wamcheka Rais wao ‘Kuchemka’ Kwenye Mahojiano

Ikiwa imebaki wiki moja tu kuelekea kwenye uchaguzi wa Rais nchini Macedonia, mgombea Urais ambaye ndiye Rais wa sasa Gjorge Ivanov alisababisha mjadala makali kwenye mitandao ya kijamii baada ya mgombea huyo ‘kuchemka’ kwenye mjadala wake wa kwanza wa kampeni za urais..

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walisambaza habari za ‘kuchemka’ kwa Ivanov kwa kutumia alama habari  #хорхе (tafsiri ya utani ya neno la Kihispania kwa Kimacedonia Gjorje – Jorje), wakiwafikia hadhira kubwa ndani na nje ya nchi hiyo.

Pamoja na makosa mengine aliyoyafanya kwenye mahojiano hayo, Ivanov alidai kuwa Rais wa zamani wa Ufaransa Jacques Chirac aliwahi kuwa rais wa Marekani:

Wakati Jacques Chirac akiwa ni Rais wa Marekani, alichukua nafasi yake kama meya wa jiji la Paris, na kwa sababu ya uzoefu huo alielewa vizuri masuala ya wahamiaji.

Tovuti ya habari ya Macedonia iitwayo A1on.mk ilichapisha nukuu ndogo ya mahojiano hayo ya televisheni yanayoonyesha madai haya:

Kwa kurejea hatua ya kujenga ubalozi mpya wa Macedonia nchini Kazakhstan, Ivanov  alidai kwamba Kazakhstan ni nchi kubwa kuliko zote za bara la ulaya kwa pamoja:

“Nilikuwa nchini kazakhtan na kufungua ubalozi wetu pale. Na ili kukuonyesha jinsi gani Kazakhatan ni kubwa -hebu fikiria ukubwa wa bara la Ulaya na nchi zote zinazounda bara hili. Huo ndio ukubwa wa ardhi ya Kazakhastan.”

Rais huyo anafahamika kwa kugomea midahalo ya hadharani tangu aanze kampeni, ukiacha mahojiano machache ya hapa na pale anayoyafanya na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali.

Bju4miECYAAGQib

Picha ya maigizo ya Rais Gjorge Ivanov akishiriki kwenye shindano maarufu la chemshabongo ya televisheni nchini Macedonia “Nani Anataka Kuwa Milionea”. Aliyetengeneza picha hii hafahamiki -inasambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwanzoni mwa kampeni za Urais, mmoja wapo ya vituo vya televisheni vya taifa, Telma kilidai kuwa kilikumbana na hali ya [mk] kutokuwa na fursa sawa ya kupata habari na ushindani usio wa haki katika soko la habari, hali ambayo kituo hicho kinasema imesababishwa na serikali. Kituo cha Telma kilimkaribisha Rais Ivanov kushiriki kwenye mahojiano ya televisheni ya moja kwa moja, lakini akikataa. Telma ilikuwa na maoni yafuatayo:

Mtu ambaye anataka kuwa rais wa wananchi wote, na hiyo ikimaanisha rais wetu pia [sisi wa Telma], aliamua kutumia vibaya madaraka yake na kuamua kutupuuza, bila kutoa majibu ikiwa amekubali au amekataa!. 

Kitendo cha Ivanov kugomea mwaliko wa kituo cha televisheni cha Telma kushiriki kwenye mahojiano kiliibua mjadala mwingine kwenye mitandao ya kijamii hususani watumiaji wa mtandao wa Twita nchini Macedonia. Mtumiaji wa Twita @parg0 kutoka Skopje alisema:

#Хорхе ameanza kukataa mialiko. Kiti chake kitakuwa wazi kwenye studio. http://t.co/AIzDm1P4ub Au basi tayari wanacho [kitu wazi].

Baada ya twiti hii, watumiaji wengine wa mtandao huo walitaarifu kuwa Ivanov alikuwa amekataa au kupuuza mialiko kwenye mahojiano au midahalo kutoka kwenye vyombo huru vya habari.

Chombo vya habari Libertas kilibainisha kuwa masaa kadhaa baada ya kuanza kwa mjadala huo wa mtandaoni kuhusu ‘kuchemka’ kwa Ivanov kwenye televisheni, baadhi ya video zenye maudhui ya mahojiano hayo yanayojadiliwa zilikuwa zimeondolewa kwenye mtandao wa YouTube [mk]. Baada ya kuondolewa kwa video hizo, baadhi ya watumiaji wa twita walimfananisha Ivanov na Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyib Erdoğan.  

Niligundua jana kuwa video iliyokuwa inamwonyesha Ivanov akisema Chirac alikuwa rais wa Marekani imeondolewa. Msisahau, #Хорхе ana moyo unaofanana na ule wa Erdoğan.

Baada ya kuondolewa kwa video hizo, watu walimfananisha IVanov na Waziri Mkuu wa Uturiki Recep Tayyib Erdogan, ambaye pia alikumbana na upinzani mkali kwa kuifungia mitandao ya kijamii mwishoni mwa mwezi Machi 2014.

Bado haieleweki kwa nini video hizo hazipatikani tena. Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanadhani huenda YouTube imeziondoa kufuatia malalamiko ya baadhi ya watazamaji, ila kwamba walioziweka ndio wameziondoa video hizo, au kwamba zimeondolewa kwa shinikisho kutoka serikalini bado haijulikani.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.