Malawi: Maoni ya Mtandaoni Kuhusu Kifo cha Mutharika

Taarifa za vyombo vya habari nchini Malawi na duniani kote zinaeleza kwamba Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika amefariki dunia. Wakati hakuna maelezo rasmi ya serikali juu ya tukio hilo wakati makala hii inapoandikwa, uchelevu wa tangazo umetengeneza imani kuwa kuna jambo baya zaidi linaloendelea [*soma habari mpya chini].

Redio ya Taifa ya Malawi ilitangaza jioni ya Alhamisi kuwa Mutharika (mwenye umri wa miaka 78) alipelekwa Afrika Kusini kufuatia mshtuko wa moyo asubuhi ya siku hiyo ya Alhamisi.

Mutharika alikuwa chini ya shinikizo la ndani na la kimataifa la kuboresha hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini Malawi.

Huku shughuli za kila siku zikiendelea kama kawaida kwenye miji ya Malawi, wanablogu na raia wengine wa mtandaoni kwenye tovuti za habari za kijamii wameopokea habari hizo na mitazamo mchanganyiko.

Kwenye kundi la facebook la Malawi Fuel Watch (Tovuti inayofuatilia hali ya mafuta), raia mmoja wa mtandaoni aliandika:

Hebu nicheke, rais ameondioka na sasa mafuta ya ptroli yanapatikana!

Watu wa Malawi wamekuwa wakipanga foleni kwa masaa mengi ili kupata mafuta tangu tangu mwaka 2010.

Wakati mtu mwingine aliandika:

Peter Mutharika [kaka yake rais], muwache Joyce [Makamu wa Rais] achukue madaraka ikiwa hali itakuwa ilivyo, tunahitaji mafuta sasa…

Bingu wa Mutharika akiwa Makumbusho ya jiji la New York. Picha rasmi ya Ikulu ya Marekani na Lawrence Jackson iliyotolewa kwa Matumizi ya Umma.

Mwanahabari wa Malawi ambaye pia ni mwanablogu Rebekka Chimjeka aliripoti kuwa mwili wa Bingu unatarajiwa kurudishwa nchini Malawi haraka. Alisema kuwa Malawi inatarajia Makamu wa Rais Joyce Banda ataongea na wana habari. Mwanahabari huyu amekuwa akiweka habari mpya zinazohusiana na kifo cha Mutharika kwenye blogu yake.

Mwanahabari mwingine Kondwani Munthali alizipinga ripoti kuwa Mutharika alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Milpark huko Afrika Kusini:

Malawi ipo njia panda. Rais Bingu wa Mutharika asilani hajapelekwa hospitali ya Milpark kama ilivyodokezwa na serikali, imegundulika.
Ishara zote, kitabibu, kutoka kurugenzi ya uendeshaji mashtaka, kutoka kwenye familia na kutoka vyanzo vingine zinaashiria kuwa Rais kwa masikitiko alifariki dunia jana na yupo kwenye nyumba ya mazishi huko Afrika Kusini.
Nyaraka za matibabu kutoka Hospitali ya Milpark zinaonyesha kuwa watu 16 walikuwa katika Kitengo cha Wagonjwa Mahututi na hapakuwa na nyaraka zozote zinazomhusu rais.

Aliiombea dua Malawi huku akitarajia kwamba katiba itashinda:

Kuna taarifa kuwa baadhi ya watu kwenye chama tawala wanajaribu kulishinikiza bunge likutane na kubaibadili katiba ili kwamba isimruhusu makamu wa rais kutwaa madaraka.
Ni maombi ya blogu hii kwamba utaratibu wa katiba utafuatwa na kwamba Urithi, Heshima na Hadhi ya Rais itaheshimiwa kwa kuruhusu amani na utaratibu a katiba kufuatwa.

Utabiri wa TB Joshua wa Naijeria wa mwezi Februari kuhusu kifo cha Rais wa Afrika ulizua mashaka kwa watu wa Malawi na waumini wengine walionekana kuzidisha imani kuwa Mungu angeingilia kati katika suala hili.

*Habari Mpya: Makamu wa Rais wa Malawi amethibitisha kwamba Rais Bingu wa Mutharika amefariki dunia na ametangaza siku 10 za maombolezo. Kwa kufuata katiba, Makamu wa rais Joyce Banda atatwaa madaraka. Hata hivyo, msemaji wa serikali anasema kwamba hataweza kumrithi Mutharika kwa sababu (Banda) si mwanachama wa chama tawala. Alifukuzwa kutoka katika chama tawala mwaka 2010 baada ya kutofautiana na jaribio la Mutharika la kutaka kumtayarisha kaka yake kuwa mrithi wake.

Malawi Voices iliripoti kuwa viongozi wa jeshi wamekubali kufuata katiba kwa kumuunga mkono Joyce Banda:

Jeshi la Malawi lilifanya kazi ya muhimu sana, Jenerali Odillo aliongoza mkutano na viongozi wa jeshi na kwa kauli moja walikubali kufuata katiba. Jenerali huyo alimtaarifu Joyce Banda, Peter Mutharika na Goodall Gondwe kuwa jeshi litadumisha katiba na jambo lolote tofauti na hilo halitavumiliwa. Timu ya maaskari lilikuwa katika hali ya tahadhari kwenye kambi ya kijeshi ya Kamuzu na wengine wachache walikwenda kulinda nyumba ya makamu wa rais. Matukio haya pamoja na shinikizo la moja kwa moja la serikali ya Marekani kwa Peter Mutharika vilitia pancha “mipango ya Peter na Goodall”

Kundi la mawaziri lilijitokeza katika mkutano na waandishi wa habari usiku wa Ijumaa na kutangaza kuwa makamu wa rais Banda hataweza kumrithi Rais Bingu wa Mutharika.

Hii ni mara ya kwanza kwa Malawi kumzika rais aliyekuwa madarakani.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.