Afrika: TEKNOHAMA Kwa Ajili ya Wakimbizi na Watu Wasio na Makazi

Katika wiki za hivi karibuni Global Voices imeendelea kuwakilisha kwa wasomaji wake mifano zaidi ya jinsi uanahabari wa kiraia unavyotumika kuwawezesha wakimbizi na watu wasio na makazi. Hata hivyo, wakati ambapo blogu na mitandao ya kijamii ikiwa bado inaendelea kukuza sauti, hivyo pia ndivyo tasnia ya TEKNOHAMA inavyofanya kwa ujumla.

Kwa mfano, MobileActive, inahamasishwa na uwezo wa simu za mkononi zinavyowawezesha wakimbizi siyo tu kuwasiliana na wapendwa wao, bali pia kuweza kujua mahali walipo. Tovuti hiyo inawaonyesha wasomaji wake makala maalum ya Jarida la Uhamiaji wa Kulazimishwa ambalo linaangalia kwa kina suala la Teknohama katika muktadha huu.

Refugees in Uganda are using SMS and cellphones to reconnect with family members and close friends. Photo via MobileActive

Wakimbizi nchini Uganda wakitumia simu za mkononi kuwasiliana na jamaa pamoja na marafiki wa karibu. Picha kupitia Mobile Active.

Wakimbizi mara nyingi hufikwa na athari lukuki: Hali ambayo kwanza ilisababisha wakimbie, vile vile ukweli kwamba familia nyingi husambaratika wakati wa kuhama. Ili kuwa na afya njema na ustawi na uwezo wa kutulia tena, ni muhimu kufahamu walipo ndugu na jamaa, usalama wao, na uwezo wao wa kuendelea kuwasiliana. Leo hii, simu za mkononi ni teknolojia ya muhimu zaidi kwa wakimbizi ili kuweza kuwapata ndugu na kuendelea kuwasiliana nao.

Jarida la Uhamiaji wa Kulazimishwa Toleo la 38, Nakala ya Teknolojia inapitia teknolojia hususan kwa ajili ya wakimbizi. Sura mbili (za jarida hilo) zinaangaza nuru juu ya matumizi ya simu za mkononi baina ya wakimbizi, aidha juu ya baadhi ya matatizo ya teknolojia hii katika kutafuta na kuwasiliana na ndugu kama vile suala la usalama na upatikanaji.

Naibu Kamishna wa Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Wakimbizi T Alexander Aleinikoff ametoa utangulizi katika toleo hilo maalum:

Japokuwa kwa juu juu, kambi za wakimbizi za leo hazionekani tofauti sana na vile zilivyokuwa miaka 30 au 40 iliyopita. Inaonekana kana kwamba maendeleo yamewapitia mbali. Lakini ukiangalia kwa karibu, ni wazi kuwa mambo yanabadilika.

Hivi sasa, wakimbizi na watu walipoteza makazi katika nchi maskini zaidi mara nyingi huwa na uwezo wa kupata simu za mkononi na wana uwezo wa kuangalia televisheni za setilaiti. Migahawa ya intaneti imechipuka katika sehemu walizofikia, na vifaa vimenunuliwa na wajasiriamali wakimbizi au vilivyotolewa na mashirika ya misaada ya kibinadamu kama vile UNHCR. Na mashirika ya misaada yanaongeza matumizi ya teknolojia za kileo zaidi: kama vile mifumo ya taarifa za jiografia, Skype, takwimu za biometrika pamoja na Google earth, vikiwa kama ni mifano michache.

Katika makala moja, mfano wa mradi wa kutafuta watu ulitekelezwa na ushirika wa Wakimbizi nchini Kenya (RCK) kwa kushirikiana na Umoja wa Wakimbizi (RU) umeonyeshwa:

Mwaka 1991 Ahmed Hasan Osman* alikimbia mtafaruku huku Somalia, na kuiacha familia yake mjini Kismayu, na kufanya safari ya kuelekea Kenya ili kutafuta hifadhi. Ahmed aliishi kwa muda kwenye kambi ya wakimbizi ya Ifo kabla ya kupewa makazi huko Colorado nchini Marekani ambako alipewa uraia kamili wa Marekani.

Mwaka 1992, binamu yake Abdulahi Sheikh aliwasili nchini Kenya akitafuta msaada, alipopewa hadhi ya ukimbizi, Abdulahi aliishia kwenye kambi ya Dagahaley huko Dadaab. Aliamini kuwa Ahmed alikuwa ama mjini Dadaab au aliwahi kuwepo pale lakini jitihada zake za kumtafuta hazikuzaa matunda na pindi alikata tama ya kumpata. Bila ya shaka, Abdulahi aliamini kuwa Ahmed alikuwa kesharejea Somalia.

Mapema mwaka 2011 RCK ilimuajiri Abdulahi ili kusaidiamradi wa RU kwenye kambi ya wakimbizi ya Dagahaley. Abdilahi alijiunga na mradi wa kutafuta watu na kuanza kuwatafutwa wapendwa waliopotea. Alipoliona jina analolifahamu, aliwasiliana na mtu huyo kwa kupitia mfumo wa ujumbe mfupi wa simu wa RU. Pale alipopata majibu aligundua kwamba, baada ya miaka 20 ya kutengana na kutafutana, alimpata binamu yake mpendwa. Leo hii, watu hawa wawili wanawasiliana kila mara na wote Abdulahi na Ahmed wanaendelea kusaka marafiki na wanafamilia zaidi.

Bila ya shaka, kama vile MobileActive inavyosisitiza, matatizo kadhaa ya miundombinu yanaendelea kuwa kizuizi kwa matumizi makubwa ya mfumo huo:

Kwenye baadhi ya maeneo ya Afrika, hakuna mtandao wa mawasiliano. Washiriki wa warsha walitoa maoni kuwa pale ambapo (mtandao) upo, simu hukatwa mara kwa mara, na baadhi hukutwa na maingiliano ya mawasiliano kama vile kuingiliana kwa simu. Nguvu ya mtandao wa mawasiliano kwenda nje ya nchi ni dhaifu, na ukosefu wa chanzo cha uhakika na madhubuti cha umeme kwenye nchi za wapokeaji unaweza kuwa tatizo, japokuwa hili linatofautiana kanda kwa kanda. Ongezeko la idadi ya watu katika baadhi ya maeneo hudhoofisha nguvu ya mtandao, kutokana na matumizi makubwa ya umeme. Watu wanaweza pia kuwa na ugumu wa kupata umeme wa kuchaji simu zao za mkononi.

[…]

Kupata teknolojia bora zaidi ya kutumia kwa wanafamilia tofauti kunaweza kuwa vigumu, hasa iwapo wao wenyewe wamepoteza makazi, kutokana na sababu kama wingi wa huduma zilizopo, kama wanafamilia wanaweza kuzimudu na kama wana ujuzi wa kuzitumia. Mshiriki mmoja alibainisha kuwa wengi wa wanafamilia walio ng’ambo inawabidi kupata teknolojia za mawasiliano kwa kupitia watu wengine. Mshiriki mmoja alielezea matatizo aliyoyapata kuwasiliana na mumewe aliyekuwa kambini. Alimtumia pesa za kununulia simu lakini watu wengine kambini pia hutumia simu hiyo hiyo na aghalabu kumfanya asubiri kwa masaa ili apate kuwasiliana na mumewe.

Njia mbadala za bei nafuu kama vile barua pepe, au simu za kwenye intaneti au ujumbe mfupi wa maneno zinaweza kuwa hazipatikani au aghali, na upatikanaji wa intaneti barani Afrika ni ghali mno. Zaidi ya hivyo, wanafamilia waliopoteza makazi walioko ng’ambo wanaweza kuwa hawajui kutumia vifaa hivi.

Kutoka kuwapa wakimbizi upatikanaji wa habari juu ya afya na fursa za elimu mpaka utumiaji wa Facebook, maongezi kwa ktumia Gmail na Skype ili kudumisha mawasiliano na wanafamilia na marafiki kuvuka mipaka ya kijiografia, toleo hili limetoa picha kamili ya jinsi gani Tknohama inavyotumika.

Ushahidi pia imetajwa ikihusishwa na tetemeko la ardhi nchini Haiti mwaka 2010 na vile vile kwa ujumla wakekama inavyohusiana na migogoro, majanga na wakimbizi. Kadhalika, Maabara ya Fikra ya PBS inaangalia ushirikiano wa Al Jazeera na Ushahidi katika kuwaunganisha na kuwawezesha waSomali waliotenganishwa na vita pamoja na ukame:

Somalia Speaks (Somalia Inaongea) ni ushirika kati ya Souktel, shirika lililoko Palestina linalotoa huduma za ujumbe wa simu za mkononi, Ushahidi, Al Jazeera, Crowdflower, pamoja na Taasisi ya Waafrika Walio Ughaibuni. “Tulitaka tupate mitizamo ya raia wa kawaida wa Somalia ili kwamba ituambie jinsi ambavyo mgogoro ulivyowaathiri wao pamoja na waSomali walio ighaibuni,” Soud Hyder wa Al Jazeera alisema katika mahojiano.

[…]

Lengo la Somalia Speaks ni kukusanya sauti ambazo hazisikiki kutokea ndani ya eneo vile vile kutokea kwa waSomali walio ughaibuni kwa kuuliza kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkononi: Kwa jinsi gani mgogoro wa Somalia umekuathiri? Majibu hutafsiriwa kwa Kiingereza na kupachikwa kwenye ramani. Tangu kuzinduliwa, takriban jumbe 3,000 za simu za mkononi zimepokelewa.

[…]

Kwa Al Jazeera, Somalia Speaks pia ni fursa ya kujaribu mbinu bunifu za simu za mkononi katika uanahabari wa kiraia na ukusanyaji habari.

Mnamo mwezi Oktoba 2010, MobileActive ilionyesha pia mradi wa simu za mkononi uliotekelezwa na Asasi ya Refugees United nchini Uganda kwa msaada wa Ericsson, UNHCR na Mtandao wa Omidyar, na kueleza kuwa kuna blogu moja ilyouita (mradi huo) “mtandao wa kijamii ambao ni muhimu zaidi ya Facebook.”

Nakala ya teknolojia ya Jarida la Uhamiaji wa Kulazimishwa inaweza kusomwa kwenye mtandao hapa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.