Dondoo za Video: Maandamano, Chaguzi, Utamaduni na GV

Sehemu hii inakusudia kuonyesha makala nzuri za hivi karibuni katika mtandao wa Global Voices ambazo zilionyesha njia anuai ambazo video zimewasaidia watu kusimulia habari zao duniani kote. Unaweza kufuatilia matukio ki-maeneo katika chaneli yetu kwenye mtandao YouTube au kwa kubofya kwenye kiungo cha eneo husika.

Maandamano ya Upinzani

2011 ulikuwa mwaka wa maandamano yaliyopata umaarufu sana. Mwisho wa mwaka hauna tofauti yoyote na miezi iliyopita ambapo watu waliokata tamaa waliamua kuingia mitaani kwa matumaini ya kufanya sauti zao zisikike na pengine kuleta tofauti.

Mashariki ya Mbali-Afrika Kaskazini

Kuwait: Waandamanaji wasio na Uraia Washambuliwa kwa Kudai Haki
Polisi waliwashambulia waandamanaji wasio na Uraia nchini Kuwait, ambao walikuwa wakidai haki za kupata nyaraka, elimu, huduma za afya, ajira na kupewa uraia.

Misri: Wanawake Dhidi ya SCAF, Nani Atashinda?

Wamisri wameghadhibishwa na Baraza Kuu la Kijeshi kuendeleza ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake; wakati huu waliwapiga na kama vile haitoshi, walimvua hijab yake mwanamke aliyekuwa akiandamana, kitendo kilichonaswa na video hii.

Misri: Wanawake Waandamana kudai Utu wao

Siku kadhaa baada ya matukio katika video iliyopita, wanawake waliandamana mjini Cairo walipinga udhalilishaji wa wanawake na vile vile wakitoa wito wa kuangushwa kwa utawala wa kijeshi kama ilivyosimuliwa katika Bahrain: Siku ya Damu ya Kitaifa, Maziko na Ukandamizaji Zaidi.

Iran: Yu Wapi Mwanafunzi Mwenzangu?

Kampeni ya wanafunzi ilizinduliwa mnamo Desemba 7 ili kuwakumbuka wanafunzi wote ambao hawakuweza kurudi katika Vyuo Vikuu vya Iran kwa sababu za kidini na kisiasa: baadhi walizuiwa, wengine walifukuzwa, wengine wako magerezani na wengine waliuawa mitaani. Uungwaji mkono kutoka sehemu nyingine duniani ulidhihirishwa kupitia video za kuwakumbuka wanafunzi waliofariki na wale waliokandamizwa. Video hii ilitumwa kutoka Barcelona, Hispania.

http://youtu.be/4535gGdL-qQ

Saudi Arabia: Watumiaji wa Mtandao watumia Uanaharakati wa Mtandaoni Kuyatangaza Maandamano ya Qatif

Mwezi wa Novemba uliorodhesha kurejea kwa maandamano katika Jimbo la Mashariki ya Saudi Arabia mwaka 2011, ambapo watu wa Qatif waliingia mitaani kudai mabadiliko, usawa, kuachiwa kwa watu waliokuwa kizuizini, uhuru wa kisiasa kama ambavyo nyingi ya kauli mbiu na sauti zao zinavyoonyesha. Mpaka sasa, waandamanaji wanne wamepigwa risasi na vyombo vya usalama kutokana na maandamano hayo.

Maandamano ya Kukaa yaliyosambaa duniani kote

Tazama ukurasa maalumu wa habari hizo.

Marekani: Mustakabali Usioeleweka kwa Vuguvugu la Maandamano ya Kukaa ya Wanafunzi huko California

Baada ya tukio lililonaswa kwenye video la kumwagiwa pilipili, ushiriki wa Chuo Kikuu cha California katika vuguvugu la dunia nzima la Maandamano ya kukaa ulivutia macho ya vyombo mbalimbali vya habari. Walipinga ongozeko la asilimia 40 ya ada ya kuandikishwa, kiwango kikubwa cha riba kwa mikopo ya wanafunzi na kupungua kwa upatikanaji wa msaada wa kifedha kutoka katika serikali ya jimbo hilo.

Bahrain: #Maandamano ya Kukaa kwenye Mtaa wa Budaiya Yaendelea

Waandamanaji wa amani huko Bahrain wanaoishinikiza serikali kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na kuwaomboleza watu zaidi ya 40 waliouawa na vikosi vya usalama tangu mwezi Fevruari walikabiliwa na mapambano makali na polisi, mateso ya kikatili, mabomu ya machozi na risasi za mpira. Hili linatokea baada ya polisi kunaswa katika video mbambali wakiwatesa waandamanaji 25 darini kwa kutumia fimbo na visu.
Ufilipino: Maandamano “Kukaa” Yauzidi Ukatili wa Polisi

Wakiionyesha dhima ya “sawang-sawa na tayo” (tumechoka),” maandamano hayo ya kukaa yalidai mambo mengi kuanzia na kitendo cha Utawala wa Aquino kupunguza bajeti ya elimu na huduma za jamii, mfumuko mkubwa wa bei ya mafuta na bidhaa muhimu, marekebisho ya sheria ya ardhi, masuala ya uhamiaji, ubomoaji holela wa makazi ya watu maskini mijini, na uvunjifu usiokoma wa haki za binadamu.

Chaguzi

Vurugu zilizotokana na uchaguzi ziliwafanya maelfu kuingia mtaani. Huko Urusi matokeo yaliyoonyesha zaidi ya asilimia 140 ya idadi ya wapiga kura tayari yamekuwa kichekesho kilichoenezwa sana mtandaoni. Na ingawa wa-Kongo wanaoishi nje ya nchi yao hawakuwezeshwa kupiga kura, walihakikisha wanapaza sauti zao zisikike duniani kote.

Ulaya ya Mashariki na Kati

Huku kukiwa na uchaguzi nchini Urusi, video za mtandaoni zilithibitisha kuwa ni nyenzo muhimu sana katika kuweka kumbukumbu za ukiukwaji taratibu za uchaguzi kama kufutika kwa wino unaomzuia mpiga kura kurudia zoezi hilo isivyo halali, rushwa kwa wapiga kura na ushiriki mkubwa wa wapiga kura na maandamano ya baada ya uchaguzi. Posti kama Urusi: Hakuna ukiukwaji wa Ukiukwaji wa Uchaguzi na Urusi: Siku ya Pili ya Maandamano ya baada ya Kuchaguzi zinaeleza sababu hasa zilizo nyuma ya maandamano kama vile matokeo ya uchaguzi, kuwekwa kizuizini kwa wanablogu na vile vile mapigano dhidi ya makundi ya watu wanaopingana na wanaharakati yaliyondikishwa na kupelekwa Moscow kutokea sehemu nyingine ili kumwunga mkono Vladimir Putin. Mfano wa ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi ni matumizi ya kalamu zenye wino unofutika ambazo zilikutwa katika vituo vya kupigia kura:

Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara

Kongo (DRC): Wakongo Waishio Nje ya Nchi Walipuka Kumpinga Kabila

Raia wa Kongo wanaoishi nje ya nchi yao waliandamana mbele ya balozi za nchi hiyo katika nchi mbalimbali. Ingawa hawakupewa haki ya kupiga kura katika uchaguzi uliopita wa rais na wabunge, waliandamana kwa lengo la kuifanya dunia kutambua hali inavyoendelea nchini mwao na kwa matukio mengine kupinga matokeo ya uchaguzi na kudai kuondoka kwa Rais Kabila. Serikali za Kimataifa zimeingia kwenye mazungumzo na serikali ya Kongo kutafuta suluhu na kumaliza ghasia zinazoendelea katika miji yao mikuu.

Utamaduni

Je, utamaduni unapatikana kwenye desturi zinazorithishwa kupitia vizazi au unapatikana kwenye kwenye tabia na shughuli zinazozoeleka na kufuatwa na watu? Nchini Mexico, watoto wanakua wakiamini kuwa wao ni watu duni kwa sababu ya rangi ya ngozi yao. Nchini Cuba, muziki maarufu wenye vionjo vya ngono huchujwa na kuzuiwa, na nchini Trinadad, maadhimisho ya dini ya Kiislam ya Shia yamegeuka kuwa sherehe.

Amerika ya Kusini

Mexico: Matokeo ya Jaribio la Ubaguzi wa Rangi kwa Watoto

Watoto hawa wanadhihirisha namna ubaguzi wa rangi unavyokuwa tatizo nchini Mexico. Kilichohitajika ni wanasesere wawili, mmoja mweupe na mwingine mweusi ili watoto waonyeshe wanavyomchukulia mwanaserere mweupe kuwa bora, hata kama walijitambulisha zaidi kupitia mwanaserere mweusi.

Visiwa vya Karibiani


Maadhimisho ya Ashura Duniani Kote

Maadhimisho ya Waislamu wa Shia ya Ashura hufanyika sehemu nyingi duniani. Huko Trinidad na Tobago maadhimisho hayo yamegeuka kuwa sherehe ya Hosay na mila hiyo imewashirikisha wa-Sunni, wa-Hindu na wa-Trinidad wenye asili ya Afrika.

Cuba: Kibao cha Regggaeton kiitwacho “Chupi Chupi” kimepigwa marufuku na Serikali

Wimbo maarufu wenye miondoko ya reggaeton unaoimba wazi wazi kuhusu ngono ya kinywani umepigwa marufuku ukitajwa kuwa ni wa matusi na vyombo vya utawala vya Cuba. Mjadala kuhusu kufuatiliwa (kwa nyimbo hizo na vyombo vya serikali) umehamia mtandaoni ambapo watu wanajadiliana juu ya faida ya wimbo huo kama sehemu ya utamaduni halisi wa visiwa hivyo, watu wapende wasipende, na matokeo ya kauli hiyo ya serikali katika kukuza umaarufu wa nyimbo za namna hiyo.

Global Voices Mtandaoni

Ningependa kuwashukuru nyote kwa kusoma na kuunga mkono kazi yetu, shukrani kwa nyote tunaoweza kuwaletea habari hizi na nyinginezo. Tafadhali chukua sekunde chache kusoma juu ya kampeni yetu mpya ya kutunisha mfuko inayokujia kwa video murua:

Global Voices ni jumuiya ya watu wanaojitolea inayoundwa na waandishi, wafasiri, na wanaharakati wa mtandaoni zaidi ya 500 wanaokuletea habari pamoja na mazungumzo yasiyopewa kipaumbele katika vyombo vikuu vya habari kutoka duniani kote. Tazama video yetu mpya ikionyesha picha na nukuu kutoka kwa baadhi ya wanaotuunga mkono:

Video hii pia inapatikana katika lugha kadhaa..

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.