- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Misri: Wanawake Wanaoandamana Waenziwa Kwenye Mtandao

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Misri, Maandamano, Mawazo, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Wanawake na Jinsia

Nafasi ya wanawake katika upinzani dhidi ya serikali unaoendelea nchini Misri imenasa macho ya wanablogu na raia wanaoeneza habari kwenye tovuti za mitandao ya kijamii. Idadi kubwa ya waandamanaji wanaojitokeza mitaani na kudai mageuzi serikalini yamesababisha ushiriki wa wanawake kupanda na kufikia ncha ya mizani katika nchi ambamo ni hatari kupinga mamlaka waziwazi.

[1]

Mwanamke anaongoza waandamanaji huku amebeba bendera ya Misri kwenye Mtaa wa Batal Ahmed. Picha na Nour El Refai, © Demotix (27/1/2011)

Katika “Wanawake Ni Sehemu Muhimu Ya Maandamano Ya Upinzani Misri [2]“, mwanablogu Jenna Krajeski anaandika kwamba mahudhurio katika siku ya kwanza ya maandamano (Januari 25, 2011) yalijumuisha mahudhurio ya wanawake ambayo hayajawahi kutokea kabla. Inaelekea kuwa uhalisia wa nguvu za umma katika kujipanga uliwatia moyo kuwa kuna hali ya usalama.

Je ni kwa nini wanawake wamezama sana katika maandamano haya ya upinzani, ambayo yameitwa “Siku ya Hasira”, kuliko ilivyokuwa katika maandamano mengine yaliyopita dhidi ya serikali ya Misri? Makundi yaliyoanzishwa kwenye facebook hayana uhusiano na vikundi vikuu vya upinzani. Maandamano haya pia yalionekana kuwa na usalama zaidi. Waandalizi waliwataka wahudhuriaji wayafanye (maandamano) yawe ya amani, na huo ndio uliokuwa wito mkuu katika baadhi ya maeneo ya jiji siku ya Jumanne. Zaidi ya hivyo, vijana walioelimika wa Misri, wanaume na wanawake, walikuwa wamekinaiwa na serikali ambayo haijabadilika hata kidogo katika sehemu kubwa ya maisha yao, ambayo inawanyima fursa hata watu walioelimika. Na pia kulikuwepo na (mageuzi ya) Tunisia. Mara tu, kuhudhuria maandamano kulionekana kuwa siyo tu kwamba kuna gharama sare na hatari iliyopo, lakini pia kunaweza kuchochea mabadiliko ya kweli.

Video ifuatayo ya YouTube Msichana Jasiri Zaidi ya Wote Nchini Misri iliyotumwa na iyadelbaghdadi [3] inaonyesha msichana anayetoa kauli ya kupinga utawala wa Mubarak. Maneno yake yamewekewa tasfiri ya Kiingereza.

Mike Gilgio [4] mwandishi wa Daily Beast [5] anaandika kuwa wakati si jambo lisilo la kawaida kwa wanawake kubugudhiwa kijinsia wakati wa maandamano ya umma nchini Misri, katika maandamano haya wanaume walionyesha mwenendo wenye heshima zaidi kwa wanawake katika kile kilichoitwa Maandamano Yenye Udhu [6] – ambayo kwayo dhana ya maandamano ya umoja dhidi ya dola yana umuhimu zaidi ya mikwaruzano ya kijinsia.

Kadhalika Nour El Refai [7] anatoa mwangwi wa dhana hiyo ya wanawake na wanaume kuwa maswahiba katika makala yake ya blogu “Wanawake na Wanaume Wako Sawa katika Maandamano ya Amani Dhidi ya Mubarak [8]“. Mapambano hayo ya umoja pia yanajumuisha watu kutoka kada tofauti za maisha.

Kwa mara ya kwanza, Wamisri kutoka kada zote za maisha wenye hali tofauti za kijamii na kiuchumi wamejiunga na maandamano.

Hata hivyo ujasiri wa wanawake waliojitokeza kutokas kwenye vivuli haujapewa nafasi ya kutosha kwenye vyombo vya habari, kwa mujibu wa Megan Kearns [9] anayeandika kwenye “Mapambano Mitaani: Wanawake wa Misri Wanaipinga Serikali bega kwa Bega na Wanaume Lakini Kuna picha Chache Tu za Wananawake [10]“:

Usiku baada ya usiku, wanawake na wanaume wameidharau amri ya kutotembea jijini Cairo, na kukusanyika katika viwanja vya Tahrir, au Viwanja vya Ukombozi. “Maandamano ya Watu Milioni Moja” kuelekea kasri ya rais (Ikulu) yamepangwa kufanyika kesho na mgomo wa kitaifa umepangwa kufanyika Jumatano. Raia wa Misri wanasema hawataacha kufanya vitendo vya upinzani mpaka hapo Rais Mubarak atakapojitoa madarakani. Na wanawake nchini Misri watadai haki pia. Lakini pale vyombo vya habari visipoonyesha picha za wanawake walioshiriki, inaonekana kana kwamba hawajajikita kwenye mapinduzi; wanatolewa nje ya historia.

Ushiriki wa wanawake unaorodheshwa kupitia tovuti za kijamii, kama vile Ukurasa wa Facebook wa Wanawake wa Misri [11] uliotengenezwa na Leil-Zahra Mortada [12] anayeishi mjini Barcelona. Kuanzia Januari 31, 2011 majira ya saa 12 jioni kwa saa za mashariki(EST), maudhui katika ukurasa huo yalijumuisha zaidi ya picha 130 zinazizoonyesha wanawake wa rika mbalimbali, pamoja na baadhi waliovalia mabuibui (Burqa), wengine waliovalia vilemba na wengine waliovalia nguo za kimagharibi. Wazo kuu linalowaunganisha ni kuonyesha hasira na mapambano dhidi ya polisi.

Baadhi ya picha hizo zinazagaa katika tovuti za kushirikiana picha. Watumiaji waTwitpic [13] Kardala [14], Farrah3m [15] na sGardinier [16] walizituma tena kwa Twita picha hizo za wanawake wanaondamana, wakati programu-tumizi za kushirikiana picha Plixi [17] and Picasa [18] pia zilitumika kwa malengo hayo hayo. Blogu za Subterfusex [19] na Seilo@GeekyOgre [20] pia zinasambaza picha hizo.

Mpiga picha anayejitegemea Monasosh [21] alituma picha za wanawake wanaoandamana kwenye Flickr

[22]

Mwanamke Akilalamika – ‘Fedheha gani Hii! Aibu Gani!! Kaka anampiga risasi kaka yake mwenyewe’ na mtumiaji wa Flickr monasosh (CC BY 2.0)