Tanzania: Ulimwengu wa Blogu Wachambua Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010

Ifikapo tarehe 31 Oktoba 2010, Watanzania zaidi ya milioni 19.6 watafanya uamuzi muhimu kuhusu hatma ya nchi yao. Watafanya hivyo kupitia uchaguzi mkuu wa nne chini ya mfumo wa vyama vingi. Wakati zimebaki siku chache kabla ya uchaguzi huo, ulimwengu wa blogu wa Tanzania nao unafuatilia kwa karibu yale yanayotokea katika kampeni za vyama mbalimbali.

Miongoni mwa mamba ya kusisimua katika kampeni za mwaka huu ni pamoja na wanafunzi walio wengi wa vyuo vikuu kuonekana kwamba huenda hawataweza kupiga kura. Mwandishi wa habari mwandamizi Ndimara Tegambwage anayeendesha blogu inayojulikana kama Uhuru Hauna Kikomo anaeleza kuhusu jambo hili:

…Maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya serikali walijiandikisha kupiga kura pale vyuoni kwao. Wizara ilijua hilo. Tume ya Uchaguzi ilijua na kupanga hivyo. Wanafunzi walijua watakuwa vyuoni (kwa kawaida vyuo hufunguliwa mwishoni mwa mwezi wa Septemba au mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba,lakini mwaka huu serikali imeamua kwamba vyuo vifunguliwe mwezi Novemba). Serikali kwa ujumla ilijua hilo …

Anaeleza uzoefu ulivyo katika mataifa mengine:

.. Katika baadhi ya nchi duniani, kuna mifumo ya kuhakikisha raia wake waishio ughaibuni, wanashiriki zoezi la uchaguzi huko watokako. Serikali huhakikisha kila kura inakusanywa.

Kisha anawaasa wanafunzi

…Kuna kazi moja ambayo wanafunzi wanaweza kuifanya iwapo serikali haitabadili msimamo. Wabaki walipo. Wahimize wananchi kuamka mapema na kupiga kura. Wafanye uwakala wa vyama vyao…

Jambo lingine lililosisimua katika kampeni hizi ni uendeshaji wa tafiti za kura ya maoni. Taasisi tatu zilifanya tafiti zao. Ipo Research and Education for Democracy in Tanzania (REDET), ipo Synovate na vilevile kuna Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB) (maelezo zaidi yanapatikana kwenye blogu ya Wavuti). Matokeo ya tafiti za REDET na Synovate yamepokelewa kwa hisia tofauti. Christian Bwaya anayeendesha blogu inayoitwa Jielewe alibandika makala ya Evarist Chahali anayeendesha blogu inayoitwa Kulikoni Ughaibuni. Makala hiyo inaeleza wasiwasi wa kufanyika uchakachuaji wa matokeo ya mwisho na kwamba kazi ya utafiti ya REDET ilikuwa ni kufanya maandalizi hayo:

…Wapiga kura wasianze kukata tamaa kuwa CCM wataiba kura … kwa mfano Dkt Slaa akipata asilimia 51 na Kikwete asilimia 49. Hapo watarejea uchakachuaji kama ule wa Zanzibar … Ni muhimu kutovunjwa moyo na hujuma hizi. Yatupasa kufahamu kuwa Kikwete na CCM yake ni kama mgonjwa mahututi ambaye yuko tayari hata kuning'inia kwenye uzi ili asalimike. Tutashuhudia vituko zaidi ya huo uchakachuaji wa REDET …

Wapo waliopoteza imani na REDET kama mtoa maoni aliyejitambulisha kwa jina la Markus Mpangala kupitia kwa Bwaya, anasema:

… ilipoanzishwa REDET sijawahi kusoma wala sitarajii kusoma tafiti zao … samahani mimi huwa siamini maoni hususani tafiti za namna hii … REDET wanatumia pesa kibao kutafiti eti fulani anaongoza … REDET ni mchezo wa rede au kombolela tu.

Kwa upande wake Ansbert Ngurumo anayeendesha blogu ya Utakapojua Hujui Ndipo Utakapojua aliandika kuhusu matokeo ya utafiti uliofanywa na Synovate:

… Baada ya hapo alionyesha vielelezo vya utafiti uliofanywa na Synovate, ambao katika kipengele GPO 6 liliulizwa swali: “Kama uchaguzi ungefanyika leo, nani ungempigia kura ya urais?” – Synovate walikanusha kwamba swali hilo halikuwemo katika utafiti wao … ukweli ni uwa walifanya utafiti lakini CCM iliingiza ‘mkono’ wake baada ya kubaini kuwa matokeo hayo yalikuwa yanaonyesha Kikwete yuko nyuma ya Dkt Slaa …

Wakati hayo yakiendelea, mwanablogu anayejitambulisha kwa jina la Haki na anayeendesha blogu ya Food for Thought alituletea picha inayomwonyesha mfanyabiashara maarufu na mkereketwa wa CCM, Mustapha Jaffar Sabodo ikiwa na maelezo haya:

Mfanyabiashara na mkereketwa wa CCM nchini, Mustapha Jaffar Sabodo, ametoa hundi ya shilingi milioni 100 na kumkabidhi Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe. Fedha hizo zimelenga kusaidia chama hicho ili kukamilisha kampeni.

Wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu, ulifanyika mdahalo uliorushwa na kituo cha televisheni cha ITV. Katika mdahalo huo Dkt Wilbrod Slaa mgombea urais wa CHADEMA alijibu maswali moja kwa moja kutoka kwa wananchi. Maggid Mjengwa, mwandishi wa habari na mwanablogu, alijiuliza akionekana kutatizwa na mdahalo huo:

… Kama ni mdahalo, basi ingekuwa ni vema na busara kwa wagombea wengine wa urais kushiriki. Bila shaka, wagombea wengine nao wana haki za msingi za kupewa nafasi kuelezea sera zao na kujibu maswali ya wapiga kura.

Halafu anatufahamisha kwamba CCM waliamua wagombea wao katika nafasi zote kutoshiriki kwenye midahalo:

…Hata kama chama tawala, CCM, kimeweka wazi kuwa mgombea wao hatashiriki mdahalo …

Kwa upande wake mwandishi wa habari mpiga picha, Issa Michuzi, anayeendesha blogu yenye kusomwa sana nchini na nje ya nchi, IssaMichuzi yeye anafuatilia kampeni za Mh Jakaya Kikwete mgombea urais wa CCM pamoja na waungaji wake mkono wa karibu. Moja ya vichwa vya habari za makala zake ni: JK Afunika Bovu Mlimba, Mahenge na Ifakara.

UDADISI anayeblogu kupitia Rethinking in Action anasema nini kuhusu mgombea wa kiti cha urais anayetokea kambi ya upinzani na ambaye ameonekana kuipa CCM wakati mgumu:

…It is quite clear that Dr Wilbrod Slaa's decision to run as a presidential candidate has tilted the balance of power. Now the debate is no longer about whether the ruling party's candidate [Jakay Kikwete] will get a landslide victory – as in the previous election. rather, it is about how much that victory will be cut.

…Ni wazi kuwa uamuzi wa Dkt Wilbrod Slaa kuwa mgombea urais umeyumbisha mizani ya nguvu. Hivi sasa mjadala haujadili tena juu ya ushindi mkubwa atakaopata mgombea wa chama tawala [Jakaya Kikwete] – kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita. Badala yake, (unajadili) ni kiasi gani ushindi huo utapunguzwa.

Upande wa Zanzibar, dalili mwaka huu ni uchaguzi tulivu zaidi hasa baada ya makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa visiwani humo. Hata hivyo, bado kuna yanayoendelea kama anavyotuletea Mzalendo kupitia blogu ya Uchaguzi Zanzibar 2010 habari iliyoandikwa na Salma Said:

…SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekiri kwamba imeandikisha watu katika daftari la kudumu la wapiga kura wasiokuwa na sifa za kuandikishwa katika daftari hilo kutokana na sababu mbali mbali.

Mbali na kukiri hilo, pia serikali imekiri kuwaajiri waafisa wasaidizi wasimamizi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) waliokuwa hawana sifa za kuajiriwa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi katika semina ya wakuu wa mikoa, makamanda, maafisa wadhamini, kamati za ulinzi na masheikh iliyofanyika kwenye ukumbi wa Elimu Mbadala Vitongoji Mkoa wa Kusini Kisiwani Pemba….

Hata hivyo, anawaasa Wazanzibari (na Watanzania kwa ujumla) akisema:

…Waswahili wana msemo wanasema kwamba yashayopita sio ndwele tugange yanayokuja. Naam, nakubaliana na msemo huo lakini tukumbuke katika kuganga kunahitajika umahiri, ubunifu, ujuzi, uzoefu na busara za kutosha ili ndwele ile iliotokea nyuma isije ikajirejea tena…

Mpambano mkali katika nafasi ya urais (Muungano) uko kati ya Jakaya Kikwete wa CCM, Wilbrod Slaa wa CHADEMA na Ibrahim Lipumba wa CUF. Kule Tanzania Visiwani, makabiliano ni makali kati ya Dkt Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF.

Makundi mbalimbali ya waangalizi wa kimataifa tayari wapo nchini Tanzania. Mojawapo ni Jumuiya ya Madola, ambapo Katibu Mkuu wake, Kamalesh Sharma, alisema:

…The Commonwealth has a history of engagement with Tanzania, and we are pleased to observe these important elections,” adding, “We very much hope that they will further strengthen the democratic process and advance development in the country.”

…Jumuiya ya Madola imekuwa na historia ya kujishughulisha na Tanzania, na tunayo furaha kushiriki kuwa waangalizi katika uchaguzi huu muhimu,” akiongeza, “Tuna matumaini makubwa kwamba uchaguzi huu utaimarisha zaidi mchakato wa demokrasia na kukuza zaidi maendeleo ya nchi.”

Je, Watanzania kuamua nini? Kusuka ama kunyoa? Tutafahamu mara baada ya uchaguzi kupita.

3 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.