China: Kujitoa Uhai kwa Msomi Mwingine tena – Kisa cha Yang Yuanyuan

YANG Yuanyuan, binti msomi mwenye miaka 30 aliyekuwa na shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai Maritime, alijinyonga kwenye bafu la nyumbani kwake mnamo Novemba 25 mwaka huu. Siku moja kabla hajachukua uamuzi huo alimwambia mama yake kwamba maarifa hayawezi kubadili majaaliwa.

Miaka ya hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la kujiua miongoni mwa wanafunzi Wachina katika vyuo vikuu, hasa wale wa shahada za uzamili na uzamizi. Katika jiji la Shanghai mwaka 2008, kulikuwa na majaribio 23 ya wanafunzi wa vyuo vikuu kujiua ambayo yalisababisha vifo 19. Katika mji wa Guangdong, mwaka 2008, kulikuwa na matukio 26 yaliyosababisha vifo 21. Hivi, nini hasa ni sababu za matukio haya ya kujiua? Kisa cha Yang huenda kikatoa mwanga kuhusu matatizo ya kijamii yanayowakabili wasomi wetu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka 163.com ni kwamba Yang alitokea katika familia ya mzazi mmoja. Yeye na kaka yake walilelewa na mama ambaye ilimpasa kufanya kazi sana ili kuwasaidia watoto wake kupanda daraja kupitia elimu – Yang alikuwa akisoma shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Shanghai wakati kaka yake anasoma shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Peking. Tangia mama yake Yang aachishwe kazi katika kiwanda fulani, alikuwa akiishi na binti yake katika bweni la Chuo Kikuu cha Wuhan ambako Yang alisoma shahada yake ya kwanza. Binti huyo alifanya kazi kwa miaka miwili ili aweze kulipa madeni yote kabla hajaamua kuendelea na masomo ya juu zaidi huko Shanghai. Huku akiwa na fedha kidogo tu, alijaribu kupata kitanda cha ziada kwa ajili ya mama yake kwenye bweni la chuo, lakini walisimangwa kwa sababu ya kuonekana wao ni watu wa kutoka shamba. Msimamizi wa bweni hata alimkatalia mama yake Yang kuingia kwenye bweni hilo.

Kifo cha Yang kimevuta hisia za watu wengi katika Intaneti hasa kwa kuwa inazidi kuwa vigumu kwa watu wengi wanaopata elimu ya juu kupata hadhi ya kijamii wanayoipigania. Ule mvuto wa kuwa mtu mwenye shahada unaanza kupotea. Mwanablogu Hailing, ambaye anamwonea huruma Yang, anaeleza kushangazwa kwake na kukosekana kwa uwiano kati ya elimu na mshahara katika jamii ya Wachina. Anajenga hoja zake kupitia makala yake aliyoipa jina la ‘Je, nani alaumiwe kwa kifo cha maskini Yang mwenye shahada ya uzamili?:

有时候人是很脆弱的,很可能会因为那么一二个想不通的问题,生命就从此终结。在外人看来一个贫困家庭可以出一个研究生一个 博士是多么了不起的事,而在当今学历与岗位工资严重不对等的社会,又有多少用人单位去关注你的学历?他们更关注你所给他们带来的价值,这是一个贫困家庭看 中学历大于能力的尴尬与悲哀?

Mara nyingine binadamu ni wadhaifu na wenye kuumia kirahisi, hivi, nani anayeweza kuyakatiza maisha yake kwa sababu ya swali moja au mawili ya kushangaza. Watu wa nje wanaweza kuchukulia kama jambo lisilo la kawaida kwa familia maskini kutoa mtu mmoja mwenye shahada ya uzamili na mwingine Daktari, lakini katika jamii hii ambamo shahada ya mtu haimwakikishii kupata nafasi ya kazi na mshahara unaolingana na kisomo chake, je, nani hasa atajali sana kuhusu historia yako ya kielimu? Mara nyingi, waajiri hujali zaidi thamani ile ambayo mwajiriwa atawaingizia. Ni ukweli huo ndio ulioleta msiba huu mkubwa kwa familia hii ambayo inaamini kwamba shahada ya juu zaidi ya elimu itaisaidia kukuza ubora wa maisha yao.

Wanablogu wengi wamelaani kukosekana kwa huruma katika jamii. Katika kutoa maoni kuhusu taarifa hiyo, raia mmoja wa mtandaoni (123.232.*.*) anaeleza kwamba:

不是贫穷杀死了她,而是周围人的冷漠和势利杀死了她,是那些永远缺乏同情心的人杀死了她….

Sio umaskini uliomuua lakini ni walimu na wenzake ambao wanaendekeza kutengana na kutojali wenzao, yaani wale ambao tayari wamekwishapoteza chembe zote za huruma katika nyoyo zao.

SHI Sansheng pia ana maoni kama hayo na anaushambulia kweli unafiki uliojificha kwenye utamaduni wa Confucian:

从大学到到政府,期间缺失的莫不是一个良知和人性。是什么造成了我们这个有着泱泱五千年文明,礼仪之邦的社会总是不断重复着几乎一样的悲剧?施教者、执政者满口仁义道德,一肚子男盗女娼。儒家的精神纵然有万好,如果只是用来遮丑和粉饰,即便是好也只能是同流合污了。

Kosa kubwa kabisa katika vyuo vyetu vikuu na taasisi za serikali ni kukosekana kwa dhamira na utu katika kushughulika na watu wengine. Inakuwaje kwamba misiba kama hii inaendelea kujirudiarudia katika jamii yetu? Wakati huo huo tunajivuna kwamba sisi ni taifa lenye historia ya aina yake ya ustaarabu unaorudi hadi miaka 5000 nyuma? Waalimu wa vyuo vikuu na watengeneza sera daima wanahubiri juu ya maadili lakini kwa kweli wao wenyewe ni kama genge la washenzi fulani hivi. Hata kama ile roho ya Ki-Confusian ni nzuri katika mambo mengi, lakini pale inapotumiwa ili kuficha upande mbaya wa jamii yetu, inageuzwa tu kuwa chombo cha kuwadanganyia watu.

Ni jambo la wazi kwamba watu walioelimika zaidi ni wenye nafuu zaidi kidogo ukilinganisha na wafanyakazi wahamiaji kutoka mashambani au wakulima wadogowadogo. Hapa kuna swali la kujiuliza kwamba kwa nini watu waliosoma ndio wenye udhaifu mkubwa wa kisaikolojia? REN Haiyong alijenga hoja kwamba msiba huo uliakisi kuharibika kwa mfumo wa elimu na familia. Katika makala yake ya kwenye blogu aliyoipa kichwa cha habari cha, “Mapenzi Matatu Yanayokosekana”:

我认为,理解杨元元的绝望心理,应当首先懂得人的幸福感的三大来源,也就是“三情”,即:亲情、友情和爱情……我们的学校 教育和家庭教育一直以来都有一个很大的缺陷,就是漠视人正常的感情需求,甚至把孩子们的读书求知和他们的情感需要对立起来,偏执地认为好孩子应 该一门心思读书,不能考虑情更不能考虑性。请教师们和家长们都能将心比心地、设身处地地为学生们、为孩子们想一想。尤其要 关怀女孩子,因为社会对女孩子更有一层情感压抑的要求,并把压抑的效果与道德品质的高低联系起来;好象一个女孩子只知道读书,对男孩子完全不感兴趣才是好 学生、好孩子。学习成绩越好的女生,在学校和家庭这样“纯洁”的要求下,就会更多地克制自己的情欲和性欲,也就会更多地压抑自己的正常情感需求。然而,人 的天性是无法改变的,人的忍耐也是有限度的,崩得太紧的弦,早晚是要断的。

Kwa maoni yangu, ili kuelewa vema kukata tamaa kwa binti huyu Yang, hatuna budi kwanza kuelewa vyanzo vitatu vya furaha ya binadamu: upendo wa familia, urafiki na uhusiano mzuri wa kimapenzi … mfumo wetu wa elimu shuleni na katika familia hupuuzia mahitaji hayo ya mapenzi. Walimu na wazazi huamini kwamba mapenzi husababisha mwanafunzi kufanya vibaya shuleni na hivyo huwahimiza kukazania masomo yao tu. Hawana budi kujaribu kufikiri kwa kujiweka kwenye nafasi za wanafunzi na watoto wao na kutoa uangalizi wa pekee kwa wasichana. Jamii yetu imejenga maadili yanayoelekeza kuzuia hisia za mapenzi kwa upande wa wasichana – hawatakiwi kuonyesha hisia zozote kwa wavulana, wanachotakiwa ni kuweka akili zao zote kwenye masomo yao ili wawe miongoni mwa wanafunzi vinara. Kwa hiyo kadiri mwanafunzi wa kike anavyofanya vizuri darasani ndivyo kadiri hiyohiyo atakavyozidi kukandamiza hisia zake za kimapenzi – kupenda na kupendwa. Hata hivyo, asili ya binadamu haiwezi kubadilishwa. Kujizuia huko daima kuna mipaka na huishia kuvunjika kama hali itazidi kuwa hivyo.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.