Afrika: Wanablogu wamwombolezea Michael Jackson

Msanii wa Kinaijeria akimuiga Michael Jackson katika tamasha mjini Abuja. Picha kwa hisani ya N.R kwenye huduma ya Flickr

Msanii wa Kinaijeria akimuiga Michael Jackson katika tamasha mjini Abuja. Picha kwa hisani ya N.R kwenye huduma ya Flickr

Kifo cha mwanamuziki maarufu wa miondoko ya Pop, Michael Jackson kimeamsha hisia kutoka karibu kila ncha ya dunia. Mashabiki wamekuwa wakishirikishana kumbukumbu za Jackson katika wavuti yake rasmi katika lugha zaidi ya kumi, na habari hiyo ya kifo imetawala kurasa za kwanza za magazeti dunia kote.

Barani Afrika, wanablogu wanatoa heshima za mwisho kwa Mfalme wa Pop kwa kutundika picha na video za muziki. Akiandika kutokea Nigeria, Oluniyi David Ajao anatoa orodha ya nyimbo 26 anazozipenda za Michael Jackson , wakati mwanablogu wa Uganda Serekelz anaienzi kumbukumbu ya Jackson kwa maagizo ya jinsi ya kucheza dansi ya mtindo wa kutembea mwezini, ambao ni muondoko wa dansi uliobuniwa na Jackson.

Nchini Ghana, Kent Mensah wa Africa News anakusanya miitikio wa watu kuhusu kifo cha Jackson kwenye Twitter na Facebook:

“Afrika inampenda Michael Jackson… tangu kuzaliwa unajifunza namna ya kujikusuru na kwamba Michael Jackson ni muziki…mwanamuziki maarufu kuliko wote,” Rasco Patterson alisema kwenye twitter @chickenwang4.

“Ufanye ulimwengu huu uwe sehemu nzuri zaidi kwako na kwangu haya ni maneno ya kutoka kwa gwiji wa kweli kama Michael Jackson. Nitakukumbuka daima Waco Jaco, ,” alisema Elton Afari, Accra, Ghana kwenye Facebook.

Akiyapa mwangwi mawazo ya mashabiki wengi wa Kiafrika Sudanese Thinker anamkumbuka mwanamuzki huyu maarufu:

Kwa namna nyingi Michael Jackson alikuwa ndiyo utoto wangu. Muziki wake uliujaza utoto wangu na furaha na kumbukumbu nzuri. Uliniamsha nilipokuwa chini. Ulinifanya niwe na furaha nilipokuwa mwenye huzuni.

Na hata kama alikuwa mtu wa ajabu na mwenye mapungufu, nitamkosa sana yeye pamoja na vipaji vyake.

Na mwanablogu wa Uganda Dickson Wasake anamkumbuka Jackson kwa shairi:

Kwenye kifo cha Michael Jackson:
Machozi yameijaza dunia,
Weusi kwa Weupe;
Msichana wa Kiliberia analia,
Na vivyo ndivyo afanyavyo Diana mchafu,
hata watu baki huko Moscow,
Wote tunapayuka;
“Ah ni mbaya sana; ah yatia huzuni sana;
Mfalme ametutoka mapema sana,
Na siwezi kuacha kumpenda!”

Ingawa wanablogu wengi wanaombolezea kifo cha Michael Jackson, wengine wanahoji vituko vyake, pamoja na kubadilisha kwake rangi ya ngozi. Nchini Ghana, mwanablogu Emmanuel Bensa anaomboleza kwa malalamiko:

….utamaduni wa Kiafrika unatuambia kwamba hatupaswi kuwasema vibaya marehemu– na sitarajii kufanya hivyo wakati wowote hivi karibuni, lakini nitakachokifanya ni kusema katika maana halisi jinsi uamuzi ulivyokuwa mbaya wa kujigeuza kuwa mweupe.

Weusi ni mzuri–na utakuwa hivyo daima. Kama mtu mweusi, Michael Jackson alikuwa na wajihi, sauti; kipaji. Ah aibu gani.

Kwa Mwanablogu wa Uganda Rosebell, kifo cha kimeamsha tafakari ya kwa nini habari zinatoa uzito mkubwa kwa kifo cha mwanamziki huyu badala ya majanga mengine:

Nilipokuwa nikitazama maoni ya watu duniani kote baada ya kifo cha Michael Jackson, nilijiuliza kama ni kweli binadamu wote wanaweza kuwa sawa. Si kwamba sitambui mchango wa MJ katika muziki na kipaji chake kikubwa, nitakuwa mwenye welewa mdogo kwa kufanya hivyo, lakini ninashangazwa iweje hatuumizwi tunapoona vifo dunia nzima. Kila mmoja anaonekana kusema ah alikufa akiwa bado kijana wa miaka 50, na nilifikiri pia kwamba katika Uganda wastani wa umri wa kuishi ni miaka 50. je unajua kuwa katika Afrika kufa kwa uzee ni historia? Hivi unajua kwamba taharuki hii tuliyonayo kwa kumpoteza na MJ, Wairaki wengi wanakutana nayo kila siku? Hofu ya kuyapoteza maisha yao na vitendawili vya namna watoto wao watakavyokua, vinawabana watu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Omar Basawad wa Safari Notes anapingana na ukosoaji huu, akitilia mkazo kipaji cha ajabu cha Jackson:

Chochote kinaweza kusemwa kuhusu Michael Jackson, vyovyote vile mtu anavyomfikiria – jambo moja liko wazi: aliandika kielelezo cha wakati.

“Pumzika Kwa Amani” anaandika Mwanablogu wa Kenya WildeYearnings. “Sasa unalo anga zima kucheza kwa madaha kwa staili ya kutembea mwezini…”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.