Afrika ya Kusini: ANC Yafanya Mjadala wa Uchaguzi Kwa Kutumia huduma ya Twita

Vyama vya siasa nchini Afrika ya kusini vimo katika hatua za mwisho za kampeni ya uchaguzi ujao. Chama tawala cha ANC (African National Congress) kilifanya mjadala kwa kutumia huduma ya twita.

Vyama vya siasa vimeanza kutumia mitandao ya kijamii kwenye intaneti ili kufikisha ujumbe. Chama kikubwa ambacho kimekuwa kikitumia huduma hizo ni chama cha DA (Democtratic Alliance) ambacho kampeni yake imetiwa moyo na kampeni ya mwaka jana ya Obama.

Chama cha DA kinaendesha kampeni ya kujitangaza kwenye mitandao ya kijamii pamoja na akaunti kadhaa za twita kama ile ya meya wa mji wa Cape Town na mkuu wa chama cha DA, Helen Zille.

Tarehe 17-04-2009 chama cha ANC kilitangaza akaunti yake mpya ya twita “ANC_DEBATE ” ambayo itakuwa ikiendesha mijadala ya moja kwa moja huku Jessie Duarte, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi na msemaji wa sasa wa chama cha ANC akijibu maswali.

Baada ya kutangazwa kulizuka majadiliano kuhusu umuhimu (wa akaunti hiyo). Mtumiaji wa huduma ya twita wa Kiafrika ya Kusini @ woganmay alitengeneza kurasa maalum kwenye tovuti ya twittersa ili kukusanya maoni. Maoni kadhaa katika mjadala huo yalikuwa hasi na chama cha ANC kililaumiwa.

Kwa mfano, Jason alihisi kuwa jitihada hizi zimechelewa na muda umekwisha.

Wakati Naeem alihisi kwamba idadi ya Waafrika kusini wanaotumia huduma ya twita ni ndogo sana.

Tovuti ya ANC_Debate ilifikiwa na mafuriko ya maswali na ufuatao ni muhtasari wa baadhi ya majibu.

@Saulkza: tuongelee uchumi: Mtafanya nini kuzuia kudhoofika kwa uchumi? Vipi kuhusu ukosefu wa ajira?

@ANC_debate: Uwekezaji kabambe kwenye miundombinu utachangamsha shughuli za kiuchumi, huduma za jamii ni uti wa mgongo wa sekta muhimu.

@nikzaz: mtafanya nini kuhusu uhalifu nchini Afrika ya Kusini?

@ANC_debate: tutakarabati mfumo wa sheria za uhalifu – uratibu bora, tutatengeneza miundo ya kisasa na tutaongeza rasilimali. Tutaiandaa jamii na kukabili vyanzo (vya uhalifu).

@shaynekrige:Kwa maoni yako ni kosa gani kubwa ambalo ANC imelifanya katika miaka 15 iliyopita?

@ANC_debate: Siyo kosa kubwa, bali kutotilia mkazo iapasavyo kwenye kushirikisha wananchi serikalini na katika maamuzi yanayowahusu.

Oni hili, linazua swali: Je tutauona ukarabati katika ANC ya leo, njia mpya za kuushirikisha umma kwenye maamuzi ya serikali? Labda serikali ya kidijitali 2.0?

Pia walijibu maswali yanayohusu hofu za uchujwaji wa habari

@jasdonwar: je unalo lolote la kusema dhidi ya madai kwamba vyombo vya habari vya Afrika ya Kusini vitapunguzwa baada ya uchaguzi?

@ANC_debate: hiyo ni mbinu ya kujazana hofu. Chama cha ANC kilipigania uhuru wa vyombo vya habari na hakuna lolote linaloashiria kuwa tutapuuza (msimamo huo)

Kuhusu swala la kuchuja michoro ya kuchekesha (vikatuni) vyenye mandhari ya kebehi

@JeremyTNel: Je unaamini kuwa michoro ya kuchekesha ina utovu wa heshima? Je chama cha ANC kingependa kudhibiti michoro hiyo?

@ANC_debate: Wachoraji wa vikatuni wanapaswa kuwa si waoga. Sanaa ya michoro ya kuchekesha (vikatuni) yenye mandhari ya kusanifu ni sanaa muhimu. Lakini wanapaswa kufuata maadili kama wana habari wengine.

Kuhusu masuala ya (nishati) endelevu

@flintza: Je mnakidhi vipi mahitaji ya nishati ya Afrika ya kusini huku mkiwa mnadhibiti nyayo za gesi ya ukaa. Inavyoonekana mnamakinikia makaa ya mawe (hamna uwezo wa kuona mbali)

@ANC_debate: Afrika ya kusini inapaswa kusogea mbali na nishati ya makaa ya mawe lakini bado ni moja ya vyanzo vikuu vya nishati katika upeo ulipo mbele yetu. Nishati hiyo inaongeza uwezo wa kuwekeza kwenye nishati nyuklia, jua na upepo.

Kuhusu suala la mgombea kiti cha urais Jacob Zuma kuwa kizimbani kwa tuhuma za rushwa

@ANC_debate: kila mtu ana haki sawa mbele ya sheria na ana haki ya kudhaniwa kuwa hajakosa. Chama cha ANC kinasema sheria lazima ichukue mkondo wake & mkondo huo ni kwa ajili ya Zuma na mtu mwingine yeyote.

Kuhusu mikakati ya kuzuia UKIMWI

@ANC_Debate: Tunatilia maanani kuzuia maambukizi, kuhamasisha matumizi ya kondomu na tabia njema. Usambazaji wa dawa za ART ili ziwafikie wote wanaozihitaji. Tutaimarisha ushirikiano na jamii yote

@irenebarnard: je ni kwa jinsi gani mtawapasha habari wananchi kuhusu maendeleo ya “kampeni yenu ngangari ya kuzuia Virusi Vya Ukimwi”

@ANC_debate: Watu wanatakiwa kushirikishwa katika utekelezaji kwa kupitia zahanati, mashirika yasiyo ya kiserikali, taarifa za serikali na vyombo vya habari.

Ili kusoma zaidi juu ya mjadala huu, tembelea tovuti ya Capetownalive ambayo ina muhtasari wa baadhi ya maswali.

Baadhi ya watumiaji wameripoti kuwa walizuiwa kushiriki au pengine walidharauliwa na Jessie aliwajibu kuwa hakuna mtumiaji ambaye alizuiwa, hata hivyo walikiri kuwa si maswali yote ambayo yalijibiwa. Kuna mipango ya kufanya wasaa huu wa maswali na majibu kuwa wa mara kwa mara kwa sababu imetangazwa kwamba ijumaa ijayo patakuwa na wasaa mwingine.

Niliandika katika blogu yangu kuwa japokuwa mjadala huu umekuja katika ngwe za mwisho na unashirikisha watumiaji wa huduma ya twita pekee, hii ni hatua kubwa yenye mwelekeo mzuri kwa chama cha ANC kwani kinawapa wananchi fursa ya kujadiliana nao moja kwa moja. Kama mpango huu utasambazwa nchini kote na kuruhusu watu wenye simu za mkononi kutuma maswali yao na kupokea majibu kutoka kwa wagombea, hatua hiyo itakuwa yenye manufaa sana katika kuwashirikisha Waafrika ya Kusini wote.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.