Sudani: Maombolezo ya Mwandishi Maarufu wa Riwaya na Mahakama ya Kimataifa

Baada ya kimya kirefu, wanablogu wa Kisudani, wamerejea kwenye ulimwengu wa blogu kuongea, na kushirikiana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni. Mawazo hayo yanajumuishwa katika muhtasari huu pamoja na yale ya wanablogu tuliowazoea.

Baada ya malalamiko kuhusu hali mbaya ya usalama wa afya kwenye Uwanja wa Ndege wa Khartoum, Msudani mwenye matumaini anaomboleza kifo cha mwandishi mashuhuri wa riwaya, Al- Tayeb Saleh.

Sudani imempoteza raia mpendwa, ambaye alichangia vikubwa kwenye fasihi ya Kisudani na ya Kiarabu. Kazi yake iliyopata sifa zaidi ni ile ya riwaya ya mwaka 1966 “Msimu wa Kuhamia Kaskazini.” Riwaya hiyo, kwa kipindi fulani, ilizuiliwa nchini Sudani kwa vile ilijumuisha lugha ya picha za ngono, hata hivyo imetambuliwa kama “Riwaya ya muhimu zaidi ya Kiarabu kwenye karne ya 20” na Chuo cha Fasihi cha Kiarabu kilichoko mjini Damascus, Siria.

Mapema mwaka huu, Muungano wa Waandishi wa Sudani, waliomba Al Tayeb Saleh atunukiwe Nishani ya Fasihi ya Nobeli kwa mwaka 2009.

Ras Babi Babiker, kadhalika anaomboleza kifo cha Saleh kwa kutukumbusha ile riwaya iliyolikuza jina lake katika ulimwengu wa kisasa wa fasihi ya Kiarabu.

Msimu wa Kuhamia Kaskazini (Kwa Kiarabu: Mawsim al-Higra ila ash-Shamal) ni rawaya ya hali ya juu sana kuandikwa katika kipindi cha baada-ya-ukoloni na mwandishi Al-Tayyib Salih. Ilichapishwa kwanza kwa Kiarabu mnamo mwaka 1966, na imetafsiriwa katika Kiingereza na Kifaransa.

Riwaya hiyo inamfuatilia msimulizi (ambaye hakutajwa jina) katika safari yake ya kurejea kijijini alikozaliwa nchini Sudan baada ya kuishi Uingereza kwa miaka saba akitafuta elimu zaidi.

Alipowasili nyumbani, alikutana na mwanakijiji mpya (“Mustafa Sa’eed”) ambaye hababaishwi na mafanikio aliyoyapata (mhusika), na anaonyesha maya kwa kutojihusisha naye. Mwanakijiji huyo alifichua maisha yake ya nyuma usiku mmoja baada ya kulewa kwa kuimba mashairi katika Kiingereza sanifu, na kumuacha msimulizi wetu akishangaa baada ya kuugundua ukweli kuhusu mwanakijiji yule. Iliondokea kuwa Mustafa pia alikuwa ni msomi aliyesoma katika nchi za Magharibi lakini alikuwa amejawa na chuki na uhusiano wa ajabu na marafiki zake wa kutoka nchi za Magharibi. Hadithi ya maisha magumu ya Mustafa akiwa Ulaya na hasa uhusiano wake wa kimapenzi na mwanamke wa Kiingereza, ndiyo unachukua nafasi ya kati katika riwaya hiyo.

Wakati huo huo, Mwanablogu Drima pia aliomboleza kifo cha mwandishi huyo mashuhuri na wanablogu wenzake, kwa kuandika uchambuzi wa kina wa matokeo ya agizo la kumkamata rais wa nchi yake iliyotokana na tuhuma za mauaji ya kimbari na makosa dhidi ya wanaadamu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

ICC peke yake haiwezi kufanya lolote kutekeleza agizo hilo la kukamatwa (kama italitoa) na Umoja wa Mataifa ni chui asiye na meno, lakini…

… vile hivi sasa tunaye Susan Rice kama balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Hillary Clinton kama Katibu wa Mambo ya Nje (anayo blogu yake pia) na serikali ya punda wa kibuluu, sera ya Marekani kwa Sudani itaanza kuwa tofauti na ile iliyokuwepo miezi michache iliyopita wakati Bush alipokuwa madarakani.

Agizo la kukamatwa linayotolewa na ICC katika mazingira mapya litakuwa na uzito, hivyo kutolewa kwake kutakuwa na manufaa kama zana ya kumshinikiza Omar Al-Bashir kutengeneza mazingira yatakayoleta amani katika Darfur na kutekeleza mkataba wa Amani Sudani ya Kusini, CPA.

Mimz, ambaye amerejea katika ulimwengu wa blogu baada ya muda mrefu, hivi karibuni pia alizungumzia agizo hilo la ICC na mikasa yake binafsi katika Facebook.

“Dang! Kabla sijaanza kueleza. Ni Karibu ya mwaka na nusu tangu nilipokuwa hapa kwa mara mwisho. Na mambo mengi yametukia katika wakati huo. Haya ni machache:

1. Nilijiunga na Facebook
2. Kuna matatizo ya kiuchumu ulimwenguni yanayoendelea, na yanazidi kukua.
3. Obama alichaguliwa kuwa rais wa Marekani
4. Majeshi ya Israeli yaliivamia Gaza na kuua na kujeruhi mamia ya watu.
5. Mahakama ya Jinai ya Kimataifa imetoa agizo la kumkamata Omer El-Bashir kwa tuhuma za makosa katika vita.
6. Nilifanya mahafali
7. Sami El-Haj aliachiwa huru kutoka Guantanamo Bay. (bila ya shaka nina kazi kubwa ya kuhariri)
8. Gillian Gibbons alikamatwa kawa “makosa ya kukufuru ya Teddy Bear” mjini Khartoum
9. Waasi walifika Khartoum na kuwashambulia watu wote.
10. Nilijitoa kwenye Facebook

Hivi nilishasema kwamba nilipata shahada?

Hipster, mwanablogu wa Kisudani anayeishi UAE, pia amerejea na anablogu tena. Anasimulia mkasa wake wa Ki-Che Guevara uliomkuta alipokuwa anaendesha kuelekea kazini.

Nilisita kutokana na maudhi ya ghafla, nikaliangalia lile gari baya, na kustaajabu kuona rangi na maneno yaliyopamba mfuko wa gurudumu la kipuri. Sura ngumu inayojulikana ya Che Guevara ikiwa imebanwa katika maneno makubwa yanayosomeka “T.N.T” na “Al Maafia”. Sikuweza kujizuia kuangalia nakala yangu ya Kitabu “Che Kijana: Kumbukumbu za Che Guevara”, kilichokuwa kimejiegesha kwenye kiti cha abiria, na kunifanya niwaze na kujiuliza ni jinsi gani mwanamapinduzi huyu amegeuka kuwa mzaha wa namna hii.
Katika ufahamu wangu wa wastani, nauliza: Maneno “T.N.T” na “Maafia” yana uhusiano gani na mwanajeshi huyu wa bara la Marekani?

Na kama umeshawahi kujiuliza kama kublogu ni namna fulani ya matibabu ya akili, hauko peke yako. Path2Hope anashiriki katika wazo hilo pia:

Na ikatokea, lile bwawa lililokuwa linazuia uwezo wa kuandika mawazo yangu kwenye karatasi likapasuka na kila kitu kikataka kumwagika mara moja. Mambo mengi ya kuandika, matukio mengi ya kuhusisha na unapoketi na tarakilishi yako ya mapajani na kujiuliza – ni nani anayejali?
Kila mtu ana mapambano yake – na nadhani kublogu ni aina ya matibabu na kisingizio cha ubinafsi.

Na kwa John Ackec, leo anatukumbusha juu ya hali ya kusikitisha ya elimu nchini Sudan.

Kukiwa na vyuo vikuu zaidi ya 30 nchini Sudan na kukiwa na maongezi ya kushuka kwa kiwango cha elimu na ongezeko la ukosefu wa ajira kati ya wale waliohitimu chuo kikuu, tunashawishika kuamini kuwa Vyuo Vikuu vimepoteza thamani yake na sasa vinakaribia kutokuwa na thamani yoyote. Hakuna lililo mbali na ukweli.

Katika furaha, Precious anawatakia kila mmoja siku njema ya wapendanao ya Matakatifu Valentino.

Japokuwa siamini tena katika mahaba na mapenzi mazito niliyokuwa nikiyatamani, na japokuwa siamini uongo wa wanaume wanaposema “nakupenda” wewe bado unaweza kuwa na matumaini kidogo. Haidhuru, Kwa dhati na taadhima nakutakia sikukuu yenye furaha ya Mtakatifu Valentino, ikiwa uko peke yako, una mpenzi, umechumbiwa au umefunga ndoa. Furahia siku hiyo, na usimruhusu yeyote pamoja na yeye, akuharibie siku yako!

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.