Paraguai: Wahamiaji Wasimulia Visa Vyao

Ni jambo la kawaida katika Marekani ya Latini kwa wahamiaji kuondoka na kwenda kwenye malisho ya kijani zaidi kwenye nchi jirani au nchi za mbali. Hakuna tofauti kwa Waparaguai, ambao huwaacha marafiki zao na familia ili kufuata fursa nyingine ama katika nchi za Marekani ya Kusini au ng'ambo nyingine ya bahari kwenye bara la Ulaya. Baadhi ya simulizi hizo zinasimuliwa hivi sasa kwa kutumia uandishi wa kiraia. Blogu inayoitwa Somos Paraguayos [es] (sisi ni Waparaguai) inawakaribisha wahamiaji duniani kote kuwasilisha simulizi za uzoefu wao na kujibiwa na Waparaguai wengine katika safu za maoni.

Simulizi nyingi zimejaa machungu ya moyoni yanayohusu jitihada za kuzoea nchi mpya, na simulizi nyingine ni za mafanikio. Simulizi nyingi zina maudhui ya kutafuta fursa bora za kiuchumi. Gabriela anaandika kuhusu miaka yake 30 katika nchi ya Ajentina tangu alipoondoka Paraguai ili aweze kuwasaidia wazazi wake kutafuta pesa. Hata hivyo, kuiacha nchi yake halikuwa jambo rahisi [es]:

Uchungu uliotokana na umbali na uchungu mkubwa uliotokana na kutoweza kuwaona au kuwasikia ninaowapenda, kutoweza kuona anga la kibuluu au miti iliyositawi ya kijani na ardhi yenye rangi, ngoma, na lugha tamu ya Kiguarani viliamsha udadisi wa kutaka kujua yanayohusu nchi yangu, na pia kujilinda na maswali yanayoulizwa na wale walioing'amua na kuuliza juu ya lafidhi yangu.

Kuiacha nchi yako mara nyingi ni rahisi kuliko kuingia katika nchi mpya kutokana na vizingiti vya uhamiaji. Si wote wanaotaka kwenda nchi za nje ambao wanafanikiwa kufanya hivyo. Olinda alipewa kazi na familia moja huko Uingereza na anaandika jinsi alivyokataliwa kuingia baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow mjini London [es]:

Hatimaye nilifika kwenye dawati na kushughulikiwa na mtu ambaye alikuwa anaongea Kiingereza tu, na sikuelewa lolote, baadaye walimleta mkalimani na wakaniuliza kwa nini nimekuja na mambo mengine. Wakanipeleka kwenye ofisi ili waniulize mambo mengine zaidi, na hapo ndipo niliingiwa na hofu. Waliniuliza ni kiasi gani nilicholipia tiketi, jambo ambalo sikuwa nalifahamu, pia waliniuliza rafiki yangu na mumewe walikuwa na utaifa gani (familia iliyonipa kazi), nikawaambia kuwa walikuwa ni Waparaguai, lakini iliondokea kuwa alikuwa ni Muajentina na mumewe alikuwa ni Muitaliani kutokana na baba yake, lakini waliwahi kuishi Paraguai, lakini sikuwa nafahamu mambo mengine. Walimpigia simu yule mwanamke na wakamuuliza mambo mengine yanayonihusu, kadhalika naye hakuwa anafahamu mengi… na hivyo ndivyo walivyogundua kuwa nilikuwa pale kwa ajili ya kazi na wakanikatalia kuingia nchini.

Waliniambia kwamba kuna ndege siku inayofuata, na kwamba wangeniweka kizuizini pale uwanja wa ndege mpaka watakaponisafirisha asubuhi yake. Walinichuka mpaka kwenye chumba chenye kitanda, bafu na televisheni ambamo nilipumzika na kungoja mpaka kesho yake. Kwa kweli, Waingereza walinitunza vizuri siwezi kulalamika, ulikuwa ni ugeni wangu kwenye mambo haya na wafadhili wangu walidhania kuwa ingekuwa rahisi kuingia, lakini haikuwa hivyo. Pia waliniambia kwamba kama nitataka kurejea Uingereza, ninakaribishwa kwa kuwa sikuwawakera na wala sikulia kama wengine wengi wanavyofanya. Kwa kweli, sielewi ni kwa nini walisema vile, na kama ingelikuwa hivyo kwa nini hawakuniruhusu kuingia?

Nilirejea mjini Asuncion siku iliyofuata na miezi kadhaa baadaye niliamua kujaribu tena, lakini mara hii ilikuwa kuelekea Hispania. Nilikopa hela za kulipia tiketi, lakini sikuweza kuingia… kwa mara ya tatu na ya mwisho, nilikopa hela zaidi na kununua tiketi kuelekea Hispania na safari hii niliingia.

Pindi wanapoishi ng'ambo, wahamiaji wengi huanza maisha mapya na kujenga mahusiano na raia wa nchi hizo mpya. Katika ujumbe huu wa blogu, Angel, raia wa Hispania, anaeleza madhila yaliyomkuta na mke wake wa Kiparaguai [es]:

Nilikuwa katika ndoa na msichana wa Kiparaguai anayetokea San Lorenzo kwa miaka 2 na miezi 3 (miaka mitatu kwa ujumla tangu nilipokutana naye kwa mara ya kwanza). Ninasema kuwa nilikuwa katika ndoa kwa sababu hivi sasa mimi ni mjane ambaye nilimuacha mtoto siku nne kabla ya kufariki (mke wangu) pamoja na kijana wa miaka 10 ambaye kwa bahati mbaya alirejea kwa babu na bibi yake na ambaye hajaweza kutengana na mdogo wake wa kike kwa sababu za kisheria, na si kwa sababu ya mapenzi.

Matatizo ya kupasuliwa yalianzisha wiki mbaya kuliko zote katika maisha yangu, mtoto alizaliwa Jumatatu na mke wangu alifariki Ijumaa. Nina hakika kuwa katika Paraguai angefariki siku ile ile ya jumatatu, lakini siwezi kuangalia nyuma na kulijadili hilo.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.