Mwangwi wa Sakata la Maziwa China katika Afrika

Nchini China inakadiriwa kuwa watoto 13,000 wameugua tangu sakata la maziwa yasiyofaa kuibuka.

Ushawishi na nguvu za China vimeongezeka Afrika, kama ulivyoongezeka uagizwaji wa bidhaa za kila namna, kuanzia viatu vya mazoezi mpaka chakula aina ya tambi. Mabloga hata wale walio mbali kama Kongo au Senegal, wanaguswa na usalama wa bidhaa za kutoka China katika nchi zao, na wanafuatilias habari hiyo (ya maziwa yasiyofaa).

Kutoka Dakar, Bloga Naomed wa Le Blog Politique du Senegal ameandika mchezo huu mdogo wa kuigiza kuhusu dawa ijulikanayo kama “melamine,” jina la hiyo dawa ambayo iliongezwa kwenye maziwa ili kudanganya ubora wa maziwa hayo. (“Melamine” inakaribiana sana kimatamshi na neno “melanine,” ambalo kwa Kifaransa ni neno linalomaanisha melanin):



Kushoto kwangu, mwanao mdogo mchangamfu, anayeonekana wa kawaida kabisa mwenye rangi ya chokleti aliyorithi kutoka kwa baba na mama yake.
Kulia kwangu, kuna bilauri ya maziwa, inayoonekana kama ni ya dhati. La hasha! Ni bilauri ya maziwa ya Kichina, kwa maneno mengine, imechanganyika mpaka chembe chembe ya mwisho ya casein. Lazima tuwe wakweli, siyo maziwa yote ya Kichina yalichanganywa na vitu visivyofaa, lakini ni kama kamari; wale wanaoshinda zaidi ni wale wasiocheza kabisa.

Jukwaa limekwisha tayarishwa, mtoto anatokwa na mate, akisubiri bilauri yake ya maziwa.

Fikiria nini kitakachotokea kama ungekuwa uliyokosa bahati na kununua maziwa kutoka China kwa ajili ya wanao. Naam Ndiyo, hilo linaweza kutokea bila kujali uangalifu uliokuwa nao; Wachina wana uwezo wa kuweka chapa kwenye bidhaa kama vile “Made in Brittany. France” ni watapeli wa namna hii. Basi fikiria kwamba unampa mwanao bilauri ya maziwa na kisha unaondoka chumbani ili kuendelea kujiandaa. Kama kawaida, unachelewa kazini – kama kawaida yako.

Kwa ghafla, yowe linatoka kwa mfanyakazi wa ndani, kutokea sebuleni. Kulikoni?

Pembeni ya mwanao kuna mtoto mwingine anayemalizia bilauri ile ya maziwa, huku analia. Siyo mwenye sura mbaya, huyu mtoto, lakini hana sura nzuri kama ya mwanao.

Itakuwa vigumu kuizoea rangi yake mpya, au kufafanua kwa majirani na wazazi wako ni nini kilichotokea. Watakuhisi tu kuwa wewe una hatia ya dhambi mbaya ili kuadhibiwa kiasi hiki. Maisha yako yatageuka kuwa ni yale ya kuzimu. Ninaelewa shida yako, kwa dhati.


Kuna hata wale wengine wanaosema, katika nyakati tofauti, kwamba watoto hubadilika kuwa wekundu, wekundu kama walivyo wakomunisti. Lakini katu mimi siamini hilo; huo ni uwongo wa watu wabaya na wapinga ukomunisti wasiostaarabika.

Kadhalika katika namna ya utani, msomaji mwingine, Thomas anajibu:
Hakuna hatari yoyote ya maziwa Senegal, kwa sababu yale tunayokunywa hapa siyo maziwa, ni unga mweupe ambao huchanganywa na maji… nimeshaambiwa mara nyingi kuwa ya ni maziwa ya unga, lakini kwa hakika, ninapoonja ladha yake, napatwa na mashaka :)

Bloga wa Le Blog Politique du Senegal amebandika ujumbe mwingine usio na utani kuhusu sakata hili la maziwa yasiyofaa, “Maziwa ya China kwa Ajili ya Watoto Weusi.” Naomed anaandika kwamba nchi fulani a kiafrika zinaagiza maziwa kutoka China, lakini, “tumezoea sana bidhaa za kutoka nchi za magharibi ambazo hudhibitiwa kiviwango na hukaguliwa mpaka tunasahau kuwa, kwingine duniani, kwa wale ambao hawaheshimu kawaida za kiusalama na walaji, ni sawa tu ilivyo Afrika [Fr].

Naomed anaendelea:

Sina maana kwamba nchi za magharibi hazina tamaa, kwamba mabepari hawatatushukia kwa hasira ikiwa watapata mwanya. Hapana. Lakini kwa kweli, huwa hawafanyi hivi. Nchi zao zimeweka viwango ambavyo hufuatwa wakishinikizwa na walaji au na wananchi.

Tunawageukia Wahindi na Wachina ili kuiga mifumo yao, lakini hatutaki kuangalia mazingira na mbinu wanazotumia. Tumetiwa upofu na kile kinachodaiwa kuwa ni miujiza ya kiuchumi ambayo hakuna mmoja, kwa chochote atakochopewa duniani, angependa kuipitia, tunaficha mbinu wanazotumia.

Naomed hadhani kwamba Afrika inapaswa kuiga mfumo huu:

Muujiza huu wa kiuchumi, ni muujiza wa utumwa, muujiza wa kinyonyaji, muujiza usio na uwajibikaji. Huo ndio muujiza wa kibepari.

Forum Realisance wa Kongo naye pia anablogu kuhusu sakata hilo la maziwa yasiyofaa. Munsengeshi Katata anaandika kuwa maziwa mabovu yalisambazwa siyo tu huko Asiakwenye nchi kama Bangladeshi, Taiwan, Hong Kong na Japani, lakini pia imeripotiwa kuwa yalisambazwa katika nchi kama vile Burundi na Gabon.

Na kwa kushangaza, hakuna neno linalonenwa na Waafrika, hakuna madai ya ufafanuzi ili kumjua ni nani aliyekosea, ili kuwasaidia kimatibabu watoto waliodhurika, na kudhibiti madhara kwa kukusanya bidhaa yote isiyofaa kutoka kwenye soko. Hakuna lolote. Na inanipasa niseme, kwamba ukimya huu unaniudhi na unathibitisha kwa mara nyingine tena, jinsi Afrika ilivyo dhaifu pale suala la kulinda watoto wake na maslahi yake linapojitokeza, ni wazi wamehatarishwa…

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.