Angola: MPLA Yashinda Zaidi Ya Asilimia 80 Ya Kura na Kutwaa Viti 191

Matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa bunge yalitolewa jana usiku na Tume ya Uchaguzi ya Taifa [pt] yamethibitisha kuwa chama tawala kijulikanacho kama Chama Maarufu kwa Ajili ya Ukombozi wa Angola (MPLA) kimeshinda kwa asilimia 81.64 (yaani kura 5, 266,216). Mshindi wa pili, chama kikuu cha upinzani cha Umoja wa Kitaifa wa Mapinduzi Kamili ya Angola (UNITA) kilipata asilimia 10.39 (yaani kura 670,363). Jumla ya Waangola 7,213,246 walipiga kura kati ya watu 8,256,584 waliojiandikisha kupiga kura – asilimia 87 walijitokeza.

Hii inamaanisha kwamba MPLA imepata wabunge 191 kati ya 220 waliochaguliwa, wakati UNITA watakuwa na 16, PRS 8 na ND pamoja na FNLA watakuwa na viti 2. (bofya hapa kwa ajili ya orodha nzima ya wale waliochaguliwa, kimikoa). Jorge Santos kutoka Leste de Angola [pt] alikuwa ni mmojawapo wa mabloga waliotangaza matokeo yafuatayo:

MPLA – 5.266.216 ( 81,64%)
UNITA – 670.363 (10,39%)
PRS – 204.746 (3,17%)
ND – 77.141 (1,20%)
FNLA – 71.416 (1,11%)
PDP-ANA – 32.952 (0,51%)
PLD – 21.341 (0,33 porcento)
AD Coligação – 18.977 (0,29%)
PADEPA – 17.509 (0,27%)
FPD – 17.073 (0,26%)
PAJOCA – 15.535 (0,24%)
PRD – 14.238 (0,22%)
PPE – 12.052 (0,19%)
FOFAC – 10.858 (0,19%)

Camara de Comuns [pt] amechapa mnyambulisho kutoka kwa msomaji Rui Miguel Menezez Vaz, aishiye huko Bie, mkoa ambao uliathirika sana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Anafafanua ni kwa nini anaamini kuwa matokeo yalikuwa kwa ajili ya fanaka ijayo:

Hakuna ya haja ya kwenda mbali ili kugundua kuwa MPLA, hata kama ni chama kinachotumia ujanja na ni chama chenye nguvu, ndiyo kilikuwa njia pekee kuelekea kwenye u-imara. UNITA haijawahi hata mara moja kuwakilisha muundo katika ngazi ya kiserikali, muundo wenye uwezo wa kusukuma vikosi. Na zaidi, wale wote wenye uwezo wa kuongoza waliondolewa katika mchakato huu wa uchaguzi, pia watu hawajasahau yaliyopita. Wakati wa uchaguzi iliweza kuonekana kiurahisi kwamba MPLA ilikuwa na haki zaidi katika vyombo vya habari na ilijitangaza zaidi. Lakini je, si chama hiki kilichoibadilisha nchi na kusababisha Angola kuvutia vitega uchumi?

Carlos Lopez [pt] alitoa maoni juu ya nini matokeo haya ya uchaguzi yanamaanisha kwa chama cha UNITA, ambacho kimepoteza zaidi ya viti vyake 50, alisema kuwa “kibaya zaidi ya kushindwa vita ni kushindwa uchaguzi”. Alisema kuwa matokeo katika jiji la Luanda yalikuwa ya kustaajabisha:

Tatizo halikuwa ujumbe wa ‘mabadiliko’, ujumbe ambao ulikubalika na ‘ulinasa’ kwenye masikio ya wapiga kura, bali tatizo nyeti lilikuwa kwenye kutathmini nguvu ya wapiga kura, yaani jumla ya kura ambazo chama kingeweza kukusanya katika jimbo hili, manispaa au kijiji. Viongozi waliwekeza na kupiga kamari katika sehemu ambazo wapiga kura hawakuweza kuoanisha ahadi zilizotolewa, kwa sababu wale walioongoza kampeni za UNITA, walitegemea takwimu zisizoaminika na hata takwimu ambazo hazikuwepo, walishindwa kuziba mapengo yaliyojitokeza, mara nyingi kutokana na kutokujua

Luciano Canhanga [pt] anachambua hali ilivyokuwa kwa vyama vidogo ambavyo havikujiongezea matumaini katika uchaguzi na ambavyo hivi sasa vimo mashakani:

Katika vyama vilivyoshindana na vikashindwa kupata viti, ni PDP_ANA pekee ambacho hakipaswi kujitoa, kwa sababu kiliweza kupata asilimia 0.5 ya kura ambazo zinatakiwa kisheria. Na vile vyama ambavyo havikushiriki katika duru hili vinatakiwa kwa lazima kushiriki uchaguzi wa mwaka 2012, ilhali vikiwa katika mashaka ya kuangamizwa. (…) Na vipi kuhusu vyama kama vile PRD, PPE na FOCAC ambavyo vinadai kuwa vimeweza kupata saini 15 elfu ambazo zimewawezesha kushiriki katika uchaguzi, vyama ambavyo baada ya uchaguzi viliishia na kura pungufu ya 15 elfu?

Koluki [pt] anachapa kiungo cha Ripoti ya Waangaliaji wa Haki za Binadamu (Human Rights Watch): Angola: Irregularities Marred Historic Elections’, iliyochapwa tarehe 15 mwezi Septemba ikionyesha kwamba hapakuwa na ‘uangalizi huru, na upendeleo wa habari’. Alitoa maoni yake binafsi juu ya ripoti hiyo na kuhitimisha kuwa:

Kwa kifupi, Ninaamini kuwa matokeo ya uchaguzi hayafikiwi wakati wa kampeni za uchaguzi au siku ya kupiga kura, hufikiwa kwa miaka na wapiga kura ambao hukusanya uzoefu wa kimaisha ambao hatimaye huamuru maamuzi yao ya kupiga kura, japokuwa kwa bahati mbaya, mchakato wa uchaguzi huwa hautokei katika njia ya wazi kama ambavyo tungependa iwe, kwa shauri ya wapiga kura, ambao tunaweza kusema kuwa ni watu na taifa kwa ujumla.

Uchaguzi wa tarehe 5 Septemba ulikuwa wa kwanza tangu mwaka 2002, ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 27 kati ya MPLA na UNITA vilikoma. Waangola watachagua Rais mwakani.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.